Search This Blog

Friday, May 4, 2012

NGORONGORO UWANJANI KESHO

Ngorongoro Heroes inaikabili Sudan kesho (Jumamosi) kwa staili ya kushambulia ili kuhakikisha inapata
tiketi ya kusonga mbele katika michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri wa miaka 20. Mechi hiyo ya
marudiano itachezwa Uwanja wa Khartoum, jijini hapa kuanzia saa 2 kamili usiku kwa saa za Afrika
Mashariki.

Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo leo (Mei 4 mwaka huu), Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Kim
Poulsen amesema kikosi chake ambacho jana usiku (Mei 3 mwaka huu) kilifanya mazoezi kwenye Uwanja
wa Omdurman kiko katika hali nzuri na kitatumia mfumo wa 4-4-2.

"Nia yetu ni kushambulia toka mwanzo ili kuwafanya Sudan wawe pia na kazi ya kuzuia badala ya kufikiria
kushambulia tu. Nyumbani tuliwafunga mabao 3-1, hivyo hapa watacheza kwa kushambulia tu. Sisi
tutazuia mashambulizi yao kwa kushambulia pia.

"Angalia mechi ya Manchester United na Manchester City pale Etihad. Manchester United walikwenda pale
kujilinda zaidi kuliko kushambulia, hali iliyowafanya wasitengeneze nafasi yoyote ya maana ya kufunga.
Staili hiyo iliwapa mwanya City ambao hatimaye walishinda. Hivyo sisi hatuwezi kucheza kama United kwa
tunataka Sudan wawe na kazi mbili, kushambulia na kuzuia pia.

"Hiyo ndiyo njia ya kuwafanya wasifikirie kutushambulia kwa muda wote, na tukipata bao mapema bila
shaka tutakuwa tumemaliza mechi. Wachezaji wangu tayari nimewafahamisha hili," amesema Poulsen
ambaye timu yake itafanya mazoezi ya mwisho leo usiku (Mei 4 mwaka huu) kwenye uwanja utakaotumika
kwa mechi kesho (Mei 5 mwaka huu).

Ingawa atajua hali kamili ya wachezaji wake baada ya mazoezi ya mwisho leo usiku, lakini kocha Poulsen
amesema anatarajia kutumia kikosi kile kile kilichoifunga Sudan katika mechi ya kwanza iliyochezwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kikosi hicho kinaundwa na; Aishi Manula, Jamal Mroki, Issa Rashid, Samir Ruhava, Dizana Ramadhan,
Frank Damayo, Frank Sekule, Omega Seme, Thomas Ulimwengu, Simon Msuva na Ramadhan Singano.
Wachezaji wa akiba ni Saleh Malande, Hassan Dilunga, Ramadhan Khamis, Said Zege, Jerome Lambele,
Emily Mugeta na Atupele Green.

Mechi hiyo ambayo haitakuwa na kiingilio kwa watazamaji itachezezwa na Aden Abdi Djamal wa Djibouti,
na atasaidiwa na Wadjibouti wenzake Egueh Yacin Hassan, Bogoreh Salime Fahan na Aden Ali Farah.
Kamishna ni Patrick Naggi kutoka Kenya.

Ngorongoro Heroes itaanza safari ya kurejea nyumbani mara baada ya mechi hiyo. Itaondoka hapa saa 9
alfajiri kupitia Nairobi, Kenya na inatarajia kuwasili Dar es Salaam siku ya Jumapili saa 3.20 asubuhi.

No comments:

Post a Comment