Search This Blog

Thursday, May 24, 2012

NCHUNGA ASISITIZA HATOJIUZULU - AMPONDA BHINDA, AMUITA KIGEUGEU

Chairman wa Yanga anayeandamwa na shinikizo la kutakiwa kujiuzulu, Lloyd Nchunga amewaponda baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliojiondoa na kusema uamuzi wao siyo dawa ya suluhu ya mgogoro uliopo, na kwamba katiba ya klabu hiyo inampa mamlaka ya kuteua wengine kuziba nafasi hizo.

Nchunga ambaye amekuwa gumzo kwenye vyombo vya habari kutokana kung'ang'ania kwenye mstari wa kukataa kuachia ngazi, amesema katiba ya Yanga inatoa mamlaka ya kuchagua watu wengine kuziba nafasi za wajumbe wa kuchaguliwa waliojiuzulu, na tayari amefanya hivyo.

"Kipengele cha 29, ibara ya (3) ya Katiba ya Yanga, kinaruhusu kuteuliwa kwa watu wa kuziba nafasi za wajumbe wa kuchaguliwa wa Kamati ya Utendaji waliojiuzulu," alisema kwa kujiamini Nchunga.

Aliongeza: "Kutokana na uteuzi huo wa watu wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na wajumbe wa kuchaguliwa waliojiuzulu, hakutafanyika uchaguzi mdogo. Wateule wapya tumeshawaandikia barua za kuwafahamisha.

Nchunga alisema kamati ya utendaji itawatangaza wajumbe wapya mwishoni mwa wiki hii na kuongeza: "Waliodhani kwamba kujiuzulu kwao kamati ya utendaji kungeweza kuwa kiini cha mimi pia kujiuzulu, watakuwa wameingia mlango siyo sahihi."

Alisema amegundua baadhi ya wajumbe kwenye kamati hiyo hawana msimamo na ndiyo hao ambao wamekuwa wakimshinikiza yeye kujiuzulu bila kufahamu kwamba uamuzi huo hauwezi kuwa suluhu ya mgogoro.

Amemtaja mjumbe aliyejiuzulu hivi karibuni, Mohamed Bhinda kuwa ni mmoja ya watu vigeugeu na waliokosa msimamo kutokana na kutoa kauli zisizo sahihi na zenye lengo la kupotosha ukweli.

Juzi, Bhinda alikaririwa na chombo kimoja cha habari akisema kikao cha kamati ya utendaji cha Yanga kilichokutana hoteli ya Protea ilimtaka Nchunga ajiuzulu kwa faida ya Yanga kwa vile mzani unaonyesha ndiye chanzo cha mgogoro wa Yanga.

Bhina alikwenda mbali zaidi na kusema, mwenyekiti wake baada ya kubanwa alikubali kujiuzulu muda wowote, lakini Nchunga alipinga kauli hiyo na kusema hakuna kikao kilichoitiswa akakubali kuachia ngazi.

"Bhinda ni dhaifu, kwanza aliyoyasema siyo tuliyoyazungumza, anatumika tu lakini ajue kutumika kwake anajidhalilisha, kamati ya utendaji tunakaa tena hivi karibuni tutamjadili na kumchukulia hatua kali za kinidhamu," alisema Nchunga.

Bosi Nchunga alitumia fursa ya kuzungumzia hali ilivyo Yanga kwa kuwaonya wazee wa klabu hiyo kwa kusema, angependa kuona mgogoro wa uliopo unaisha katika njia ya amani tofauti na hali inavyoonekana sasa.

"Hao wazee kama wameshindwa kunipindua kikatiba watulie, wasinione nimekaa kimya wakaniona mjinga, nawaheshimu ndiyo maana nimekaa kimya. Kama wanataka tuchafuane, mimi pia naweza kufanya hivyo.

"Ninawaheshimu wazee hawa, nisingependa kuingia nao kwenye matatizo, nawafahamu wote na kila mmoja anavyoishi. Nawaomba wapokee heshima yangu, wasinilazimishe kuivunja," alisema.

Kuhusu kuimarika shinikizo la kutakiwa kujiuzulu, Nchunga alisema: "Msimamo wangu uko wazi, nilishasema na narudia tena, haipo sababu ya kujiuzulu kwa shinikizo la wachache, lakini kama binadamu nitaeleza kila kitu Ijumaa."

No comments:

Post a Comment