Search This Blog

Friday, May 11, 2012

Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’-Nilifunga safari hadi Kinshasa, nikalala nje ya geti la Nonda,

Na Saleh Ally
*Baridi ilinipiga usiku kucha bado sikumpata
*Kabla, nilikamatwa na polisi kwa dawa za kulevya
MWAKA 2006 ndiyo Bakari Malima maarufu kama Jembe Ulaya aliamua kutundika daruga na kustaafu soka la ushindani, baada ya hapo yakaanza mambo mengine ya maisha.

Kabla ya hapo, Malima anajulikana kutokana na uwezo wake mkubwa wakati anaichezea timu ya Yanga na Vaal Professionals ya Afrika Kusini pamoja na timu ya taifa, Taifa Stars.
Sifa kubwa ya Malima, ilikuwa ni uwezo mkubwa katika ulinzi na kufunga mabao ya vichwa. Kila mshambuliaji aliyekabana na Malima alijua kazi aliyonayo, mwisho akabandikwa jina la Jembe Ulaya.
Baada ya kustaafu soka, pamoja na biashara ndogo ndogo, Malima aliamua kufanya kazi, aliajiriwa kuendesha mitambo na magari makubwa katika machimbo ya Barrick huko mkoani Shinyanga.
Maisha ya Malima, yamejaa misukosuko mingi nje ya uwanja na huenda akawa mmoja mchezaji mwenye simulizi za kusitikisha. Kupitia ukurasa huu wa Maisha Baada ya Soka, Malima anasimulia mambo yaliyowahi kumkuta.
Nonda Shaaban:
Nonda alikuwa alikuwa rafiki yangu mkubwa, wakati tukicheza wote Yanga alikuwa akiishi nyumbani kwangu kwa kipindi kirefu. Tuliishi vizuri sana na maisha yetu yalikuwa ni mazuri tu.
Wakati tulipokwenda Vaal Professionals kule Afrika Kusini, mwenzangu alifanikiwa kupata kibari cha kucheza soka na mimi nikakosa. Nitaelezea baadaye, labda nianze na mwishoni halafu nitarudi mambo yalivyokuwa mwanzo.
Maana nimewahi kukutana na misukosuko mingi sana, nakumbuka nikiwa nimebakiza mwaka mmoja kustaafu soka wakati huo nachezea timu ya Twiga, nilipata taarifa kuwa Nonda angerudi kwao Congo kwa ajili ya mechi ya kimataifa.
Wakati huo Nonda ambaye nilikula naye msoto Dar es Salaam na Afrika Kusini alikuwa amefanikiwa kimaisha. Alikuwa anaichezea Monaco ya Ufaransa na alishakuwa mshambuliaji tegemeo.
Nikaona itakuwa ni vizuri niende kumuona, maana baada ya kujaribu sana maisha tena kwa juhudi lakini mambo yalikuwa ni magumu na wakati huo soka lilikuwa linaenda ukingoni.
Unajua kuna wakati niliwahi kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (DIA), kwa tuhuma za madawa ya kulevya. Nayo ikanirudisha nyuma sana, nitahadithia baadaye namna mambo yalivyokuwa.
Hivyo nilianza safari ya kumfuata Nonda, nilipofika Lubumbashi, hakukuwa na namna, ilikuwa ni lazima nipande ndege hadi Kinshasa ambako mechi ilikuwa inachezwa. Nakumbuka Congo walitoka sare katika mechi hiyo.
Baada ya hapo, nilianza kazi ya kuhakikisha nakutana na Nonda kwa kuwa kulikuwa kuna mambo mawili yalinitia hofu. Kwanza, sikuwa na fedha za kutosha, mfukoni nilikuwa na dola 50 tu.
Pili sikuwa na miadi na Nonda, halafu baada ya kufika Kinshasa nikagundua alikuwa ni staa mkubwa. Kila mtu aligombania kumuona na ulinzi wake ulikuwa mkali sana, hivyo kumuona ilikuwa ni mbinde.
Nilianza kutafuta alipokuwa anaishi, lakini ilikuwa ni kazi kubwa watu kukubali kunionyesha. Mtu mmoja alinielekeza hoteli aliyokuwa anaishi na nilipofika pale wakanieleza huwa analala nyumbani kwake.
Hivyo nilianza kutafuta watu wa kunielekeza wapi anakoishi, pia ilikuwa ni kazi kubwa wao kukubali. Niliwaeleza kuwa nilicheza naye soka Tanzania na baadaye Afrika Kusini, walikubali kunielekeza baada ya kuwaonyesha picha zangu na Nonda ambazo tulipiga pamoja.
Baada ya hapo, mmoja wao akanielekeza na kuniambia nisiseme kama yeye alinielekeza kwa kuwa hawakuruhusiwa kufanya hivyo. Basi nikaenda hadi sehemu niliyoelekezwa na nilipofika pale nikamkuta mlinzi.
Kukawa na tatizo kubwa limeibuka, yule mlinzi alikuwa hazungumzi Kiswahili wala Kingereza, alizungumza Kifaransa na Kilingala. Tukawa hatuelewani, ukazuka mzozo mkubwa kati yetu.
Mzozo huo ulisababisha majirani watoke, mmoja wao alisogea karibu na kutaka kujua kilichokuwa kinaendelea. Nikamueleza kuwa mimi ni Mtanzania na nilicheza soka na Nonda, shida yangu ilikuwa ni kukutana naye.
Basi akazungumza na yule mlinzi ambaye alizidi kuonyesha ni mkorofi, akasisitiza nikae pembeni. Yule jirani akaingia ndani na kutoka na kiti, geti lake lilikuwa karibu kabisa na pale kwa Nonda. Akaniambia nimsubiri pale.
Akaniambia kuna gari aina ya Range Rover Vogue ndiyo anatumia akiwa pale Kinshasa, hivyo niliona basi nijitambulishe. Lakini akasisitiza kama nitakuwa simjui Nonda, nitaingia matatizoni.
Nikakaa kwenye kiti pale nje, ilikuwa ni baridi kali sana, nilitetemeka usiku kucha hadi ilipofika muda kama saa tisa usiku, nikaona taa za gari. Nilipoangalia kweli ilikuwa ni Vogue inakuja. Nikaona nikizubaa tu, nitamkosa jamaa. Nikasimama katikati ya geti.
Yule mlinzi alikasirishwa na kitendo change, akataka kunitoa lakini taratibu vioo vya gari vikateremshwa na nikashituka baada ya kuona aliyekuwa kwenye gari ni mdogo wake na Nonda na si yeye mwenyewe.
Alihoji sababu ya mimi kusimama katikati ya geti, nilianza kumuelezea na nilishukuru alipoanza kuzungumza Kishwahili. Alionekana kunielewa, lakini akasisitiza kwa kuwa haniamini maana hanijui vizuri, nirudi na kulala tena pale nje hadi asubuhi.
Alisema akiamka, tutaongozana kwenda kwa Nonda ambaye alikuwa amelala hotelini na aliniambia ingekuwa vigumu kuruhusiwa kumuona bila ya kwenda naye.
Sikuwa na ujanja, nilirudi pale kwenye kiti nilichopewa na jirani. Dakika chache jirani akatoka na kuniuliza imekuwaje, nikamueleza mambo yalivyokwenda. Akaniambia niendelee kusubiri.
Nikalala pale hadi alfajiri, yule jirani wa Nonda aliyenipa kiti akatoka na kunishauri. Alinieleza kwamba huenda yule mdogo wake Nonda akalala hadi saa nne asubuhi, hivyo ingekuwa vizuri kama mwenyewe ningeondoka na kwenda hotelini kujaribu kumpata.
Niliona ni wazo zuri, nikarejesha kiti chake na kumshukuru, wakati huo nilikuwa sijala siku ya pili. Nikaanza safari ya kwenda kumtafuta Nonda. Nilipofika hotelini, bado hawakukubali nimuone, wala hawakutaka kumpigia simu.
Mhudumu mmoja akanishauri nizunguke nyuma ya hoteli kwa kuwa lazima angepitia huko. Niliamua kufunya hivyo na huko niliwakuta waandishi kibao wa habari ambao walikuwa wanasubiri kuzungumza na Nonda.
Hofu ya Malima ni kama kweli ataweza kumuona mshikaji wake, Nonda Shaaban Papii. Akimkosa, ataishi vipi au atarudi vipi Tanzania wakati amebaki na dola 50 pekee ambayo ugenini ni matumizi ya siku moja tu? MKASA ZAIDI, TUENDELEE KUWA PAMOJA!

10 comments:

  1. oya habari njema hiyo sasa muendelezo wake tunaupata lini na wapi, chazbee ifm

    ReplyDelete
  2. TP MAZEMBE WANA SHAMBULIWA NA MASHABIKI SUDAN
    WAKO SAFE,CHECK KWENYE MTANDAO WAO

    ReplyDelete
  3. Duuh! Story ya Malima inavutia kinoma mi nadhan aandike kitabu cha maisha yake itakuwa poa sana, mpen ushauri atafute mwandish mzur wa vitab atakaeweza kuipangalia poa story ya maisha yake atauza sana hicho kitabu chake.!

    ReplyDelete
  4. Daaah hii story umeikatishia pabaya kweli... sasa umenipa kazi ya kucheck na facebook account yangu kama utakuwa na any updates. Lakini mi nadhani kingekuwa kitu kizuri zaidi kama kupitia sports bar tungeiona hii hata kama itachukua zaidi ya wiki 2 au 3 kumuona jembe ulaya mwenyewe akitoa huu mkasa kutaongeza msisimko.... tena kama inawezekana wakati anarekodi mbwiga ndio awe anamhoji mambo ya udambwidambwi na nini najua atakuwa na ya kuongezea na ndio story itazidi kunoga ukizingatia ni true story.

    ReplyDelete
  5. asante shaffih kwa story hii,je itaendelea lini?

    ReplyDelete
  6. Usikose kuimalizia,ni bonge la story.

    ReplyDelete
  7. shaffii please hii ni blog ambayo naichukulia serious sana kuliko blog zote, sasa haya mambo ya kuweka vitu nusu nusu maana yake nini?

    Hebu malizia story

    ReplyDelete
  8. Story nzuri ya kusikitisha, tuko pamoja we cant wait for the next episode.

    ReplyDelete
  9. Naungana na mdau aliyesema jamaa anaweza weka historia yake hiyo kwenye kitabu na walau akapata vijisenti na kuweka kumbukumbu pia kwa kizazi chake kijacho.
    Story nzuri nilipofika katikati ikabidi niangalie kwanza ni ndefu kiasi gani kwani sikuwa natamani iishe, looking forward for the next episode
    Mdau
    Mike

    ReplyDelete
  10. ebwaa shafi maizia tory ya jembe ni poa na ni ya kujifunza

    ReplyDelete