Search This Blog

Saturday, April 21, 2012

UCHAWI AKA MISUMARI HAUPO TU KWENYE SOKA BONGO - BALI MPAKA KWENYE MASUMBWI - CHEKA , MATUMLA NA WENGINEO WAFUNGUKA.



Mbabe wa wababe katika ngumi za kulipwa Tanzania, Francis Cheka

LIMEKUWA ni jambo la kawaida kwa wanamichezo kuhusishwa na imani za ushirikina, ambazo zimezoeleka hasa katika mchezo wa soka, na zimeonekana kushamiri kwenye klabu, mchezaji mmoja mmoja na hata timu za taifa.
Hali hiyo haiko katika soka peke yake, kwani hata kwenye masumbwi imani hizo za ushirikina zimeshamiri huku mabondia, hasa wa ngumi za kulipwa, wakibainisha kwamba kurogana kupo katika mchezo huo.
Huenda wangekuwa wakilipwa baada ya pambano tungesema wanafanya hivyo kwa ajili ya maslahi, lakini mabondia hawa hupewa chao mapema hata kabla ya kupanda ulingoni ili wakikung'utwa wajihudumie vizuri. Lakini, je, ni kwanini hali hiyo inajitokeza.
Francis SMG Cheka
"Ushirikina upo, mimi mwenyewe niliwahi kurogwa mwaka 2009 katika pambano lililofanyika jijini Dar es Salaam na bondia (alimtaja), katika pambano hilo mpinzani wangu alimwaga madawa 'live', lakini nashukuru niliweza kustahimili na kucheza licha ya kwamba mashabiki wake walianzisha fujo baadaye na kuvunja pambano," alisema.
Cheka, anayeshikilia usukani wa ubora Tanzania, alisema mtu anayefanyiwa ushirikina kama alivyofanyiwa hujisikia mzito ulingoni na pumzi kukata.
Hata hivyo, anasema 'mchawi wake' alishindwa baada ya yeye Cheka kufika raundi ya sita ya pambano hilo kwa sababu 'alikuwa fiti'.
Rashid Matumla Snake Boy
"Hizo ni imani tu na mambo ya Kiswahili, kama mtu una mazoezi lazima utashinda na kama huna mazoezi usitarajie kushinda," alisema bondia huyo namba tano kwa ubora Tanzania.
Matumla alisema yeye binafsi hajawahi kupigwa misumari licha ya kwamba amekuwa akisikia mabondia wakizungumzia hali hiyo ingawa haamini kama vitu hivyo vipo.
Karama Nyilawila
Karama, ambaye aliwahi kuvuliwa ubingwa wa Shirikisho la Ndondi za kulipwa la Dunia (WBF), anasema anapocheza huwa haelewi kama amepigwa misumari ama la.
"Huwa nacheza tu lakini sielewi kama wanapiga misumari ama vipi kwa kuwa sijui mtu aliyefanyiwa hivyo anakuwaje, huenda nikawa napigwa misumari bila kujijua," alisema bondia huyo anayezichapa katika uzani wa Middle.
Ashraf Suleiman
Huyu ni bondia mbishi pengine kuliko wote Visiwani Zanzibar, ubishi wake ulianzia pale alipompiga Awadh Tamim na kuwa bingwa wa Afrika Mashariki na Kati na kucheza naye pambano la kutetea mkanda huo.
Katika pambano hilo lililofanyika mwaka 2010, Suleiman alicheza vizuri raundi nne za mwanzo licha ya kwamba upepo ulimbadilikia na kupigwa kwa KO katika raundi ya saba huku mashabiki wake wakidai alirogwa na mpinzani wake.
"Kila mmoja ana imani yake, kuna anayemwamini Mwenyezi Mungu na yule anayeamini ushirikina. hata hivyo, sielewi kama wenzangu wanakwenda kwa 'Karumanzira' ili washinde," alisema bondia huyo.
Mada Maugo
Sifa kubwa ya bondia huyo ulingoni ni kucheza na mashabiki na mara nyingi amekuwa akitoka mchezoni akizongwa na kuzomewa na mashabiki hali inayomlazimu kucheza kwa hasira pasipo mipango, hivyo kutos mwanya kwa wapinzani wake kumshambulia kirahisi.
Maugo anasema; "Sisi wenye dini hatuna mambo hayo, ukifanya hayo ina maana hutapigana vizuri, lakini ukifanya mazoezi na kumwamini Mwenyezi Mungu kwa hakika utafanya vizuri."
Maugo anasema hajawahi kupigwa misumari na mabondia wenzake, lakini akasema kwamba kushindwa kwake kunatokana na majaji kwa kumbania huku akisisitiza ishara hizo za majaji ni dalili pia za kupigana misumari.
Maneno Oswald 'Mtambo wa Gongo'
Mbali na Matumla, bondia huyo ndiye mkongwe anayeendelea kupanda ulingoni, enzi zake alikuwa akipanda ulingoni mashabiki wake wakijua tayari mbabe wao ameshinda.
Je, hali hii ilikuwa inahusiana na mambo ya ushirikina? Anajitetea kwamba hajawahi kufanya hivyo na wala haamini kama mambo hayo yapo.
"Ingekuwa mtu anajua atapiga misumari ili ashinde kusingekuwa na haja ya kufanya mazoezi kwa kuwa anajua tayari ameroga, lakini tunafanya mazoezi ili kuhimili ushindani, hakuna mambo hayo," alisema.
Japhet Kaseba
Bondia huyo aliwahi kutangaza kustaafu masumbwi kabla ya kurejea na kupigwa na Mada Maugo ingawa sasa amejikita zaidi kwenye mchezo wa ngumi na mateke (kick boxing).
Kaseba anasema kupigana misumari kunafanyika na si kwenye ngumi tu, hata katika michezo na mambo mengine ya kisiasa na kijamii.
Hata hivyo, anaeleza kwamba mambo hayo yanafanywa na wale wanaoyaamini.
"Mambo haya pamoja na kufanywa, lakini hayasaidii, kwani anayetendewa kama haamini imani hizo za kishirikina hawezi kudhurika," alisema.
Kaseba alisema yeye binafsi hafanyi mambo kama hayo ulingoni na mara zote anapopanda ulingoni humtanguliza Mwenyezi Mungu huku akiamini mazoezi ndiyo mchawi tosha wa mafanikio ulingoni.

No comments:

Post a Comment