Search This Blog

Friday, April 13, 2012

TANGA CEMENT WAIPA BASI COASTAL UNION

Basi walilopewa Coastal Union

MABINGWA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, 1988, Coastal Union ya Tanga, maarufu kama ‘Wagosi wa Kaya’, wamekabidhiwa basi lenye thamani ya Sh Milioni 45 na kampuni ya Tanga Cement.
Akikabidhi basi hilo kwa viongozi wa Coastal, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Cement, Erick Westerberg, alisema, basi hilo wamelitoa kutokana na juhudi zilionyeshwa na timu hiyo katika Ligi Kuu msimu, inayoelekea ukingoni.
Hata hivyo, Westerberg, alitoa rai kwa viongozi wa klabu hiyo watambue kuwa, basi hilo ni kwa matumizi ya timu tu na sio mengine binafsi, huku akiwataka kulitunza kwa maendeleo ya timu yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Coastal Union, Ally Ahemed ‘Aurora’, alisema, msaada kampuni hiyo waliyoutoa, ni wa kwanza katika kipindi hiki na hiyo ni kutokana na kikosi hicho kufanya vizuri katika ligi.
Aurora, aliomba kampuni nyingine zenye moyo wa kizalendo, kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri zaidi katika mechi za ligi ijayo, kwani hii ya sasa iko mwishoni.
Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo, Said Sued, aliwahakikishia mashabiki wao kuwa, watahakikisha wanabaki nafasi ya nne mwishoni mwa ligi kuu, huku akisisitiza umoja na mshikamo kwa viongozi na wachezaji wenzie, kuwa ndio siri kubwa ya mafanikio.
Timu hiyo, kwa sasa inaendelea na mazoezi kwenye uwanja wa Mkwakwani kwa maandalizi ya mchezo wake unaofuata dhidi ya Villa Squad utakaochezwa jijini Dar es Salaam wiki hii.

No comments:

Post a Comment