Search This Blog

Wednesday, February 29, 2012

Jan Poulsen hawezi kukwepa lawama za kutomuita Mbwana Samatta


 Timu ya taifa ya Tanzania kwa mara nyingine imeshindwa kuwapa raha mashabiki waliofurika uwanjani kuushuhudia mchezo baina yake na The Mambas ambao ni timu ya taifa ya Msumbiji.
Kwa mtu ambaye alikuwa anatazama mchezo huu kwa jicho la kawaida anaweza kusema kuwa ameshangazwa na matokeo yake lakini si kwa mtu aliyekaa na kutazama mazingira ya timu hii kuelekea kwenye mchezo huu. Ukirejea nyuma kwenye mchezo dhidi ya timu ya taifa ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo kwa uhalisi kabisa unaweza kupata taswira ya mchezo dhidi ya The Mambas.
 Hakuna asiyejua kuwa soka la Tanzania lina tatizo sugu la uhaba wa wafungaji na ndio maana wafungaji wakuu kwenye vilabu vikubwa vya hapa nchini wote wanatoka nje ya nchi.
Mchezo dhidi ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo ulionyesha uhaba wa wafungaji kama ambavyo imekuwa ikionekana kwa muda mrefu. Ukosefu wa mtu ambaye anabeba jukumu la ufungaji wa mabao muhimu umeendelea kuonekana hata kwenye mchezo wa Msumbiji ambapo nafasi chache zilizotengenezwa hazikuweza kutumiwa kwa ufasaha.


 Kocha Jan Poulsen alichagua kumpanga John Bocco kama mshambuliaji pekee huku akisaidiwa na Vincent Barnabas aliyekuwa akisaidia mashambulizi toka pembeni na Abdi Kassim ambaye alikuwa nyuma kama mshambuliaji wa pil yaani ‘second striker’.

John Bocco ni mchezaji mzuri kwa soka la hapa Tanzania na ndio maana anaongoza kwenye chati ya ufungaji kwa kiwango cha soka la Tanzania. Unapozungumzia ‘calibre’ ya mchezaji wa timu ya taifa John Bocco bado hajafikia kiwango cha kuwa mshambuliaji wa kuiongoza timu ya taifa.
 Rekodi yake katika michezo mbalimbali inamhukumu katika hili.Tanzania inaye mshambuliaji ambaye angeweza kuwa na msaada kwenye mchezo huu lakini hakuitwa kwenye timu.
 Upande wa pili Msumbiji walikuwa na mtu ambaye kwa timu yao ni kama Samatta, Elias Palembe ambaye anacheza Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Huyu ndiye aliyefunga bao la Msumbiji.Ukiachilia mbali Palembe timu hii ina wachezaji wengi wenye umri mdogo ambao kimsingi wengi wanaanza safari yao ya soka la kimataifa na aina ya mchezo waliouonyesha ilidhihirisha faida zilizopo kwenye kuwachezesha vijana.Ukiutazama mchezo kuanzia safu ya ulinzi, beki mkongwe Shadrack Nsajigwa alicheza katika kiwango cha kawaida. Mchezo wake uliingia dosari kutokana na balaa alilokumbana nalo toka kwa Elias Palembe aliyekuwa anacheza upande wake. Palembe alimlazimu Nsajigwa kucheza kwa asilimia kubwa sana upande wake wa uwanja na si kupandisha mashambulizi kama ilivyo kawaida yake.
Beki wa pembeni kwa upande wa kushoto alikuwa Stephano Mwasika . Masika alicheza vizuri kwa walau asilimia 45%. Alikuwa akisaidia vizuri sana kuipandisha timu mbele. Tatizo kubwa kwa upande wake lilikuwa jinsi ya kujipanga wakati timu ikiwa inashambuliwa . Mwasika alikuwa anajisahau sana wakati wapinzani walipokuwa na mpira mpaka kufikia hatua ya mabeki wa kati kutoka kwenye maeneo yao kwenda kuziba pengo linaloachwa wakati alipokuwa akipanda.
Wachezaji wa Msumbiji walimsoma vyema na walikuwa wakinasa mipira na kukimbilia upande wake kwa haraka kwani walikuwa wanajua kwa kufanya hivyo wanawavuta mabeki wa kati ambao walikuwa wanaacha maeneo yao wazi.Mabeki wa kati ambao walikuwa Juma Nyoso na Aggrey Morris walicheza vyema pia kwa kiasi chao japo ukosefu wa umakini na uwezo mdogo wa kuusoma mchezo na kufanya maamuzi kabla ya mshambuliaji wa timu pinzani yaani “danger anticipation” ilikuwa tatizo.

Juma Nyosso almanusra awape wapinzani bao wakati wa lala salama baada ya pasi yake fupi kunaswa na washambuliaji wa Msumbiji na kama isingekuwa umahiri wa Kaseja hali ingekuwa tofauti.Eneo la kiungo kuanzia kwa Shaban Nditi kwa kawaida huwa hakuna matatizo mengi kutokana na wachezaji walioko kwenye eneo husika kuwa wanatimiza majukumu yao vyema pengine kuliko maeneo mengine ya uwanja .
Shaban Nditi mara nyingi hujitolea kwa asilima zote akifanya kazi kubwa ya kuzima moto pale unapotaka kuwaka . Kitu kinachomtatiza ni kitu ambacho kinawatatiza wachezaji wote wanaocheza Tanzania nalo ni kudumazwa na mazingira ya soka la hapa nyumbani. Wanakosa ujanja wa ziada na pia hawana vitu vingi vya msingi ambavyo mchezaji anapaswa kuwa navyo .Kiungo mwingine aliyecheza katikati ya uwanja alikuwa Mwinyi Kazimoto. Alicheza kawaida lakini alama nyingi alizipata kutokana na juhudi zake binafsi na goli alilofunga . Ubora wa Kazimoto haukuonekana kwa sababu ya kukosekana kwa partnership kwenye timu hasa kwenye eneo la kiungo ambako kila mmoja anaonekana anacheza kivyake na hakuna rhythm yaani ule muunganiko wa kitimu ambao unapaswa kuwepo kwenye timu yoyote na ndio maana wachezaji wenye uwezo kama wa Mwinyi Kazimoto mara nyingi uwezo wao hauonekani. Viungo waliokuwa wanacheza kama ‘Maforward wa ziada toka pembeni walikuwa Vincent Barnabas alicheza upande wa kushoto na Nizar Khalfan aliyecheza upande wa kulia . Jinsi ambavyo Stars walikuwa na umiliki mdogo wa mpira uliwafanya viungo hawa washambuliaji toka pembeni waonekane kukosa umuhimu hali iliyomfanya kocha kumtoa Nizar na kumuingiza Mrisho Ngassa na baadaye alimtoa Vincent na kumuingiza Husein Javu , baadaye pia ilifanyika ‘sub’ ya Abdi Kassim ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Salum Abubakar. Salum Abubakar na Ngasa walileta uhai kidogo lakini ukosefu wa umakini wa mshambuliaji John Bocco ulimfanya apoteze nafasi nyingi sana za wazi ambazo ingekuwa mtu mwingine angeweza kuleta uhai.Mwisho wa siku haikuwa ‘perfomance nzuri kutokana na matokeo ya mwisho ambayo yanaiweka Stars pabaya . Kocha Jan Poulsen hawezi kukwepa lawama za kutomuita Mbwana Samatta ambaye wengi wanajua uwezo wake na alistahili kuitwa kwa kuwa anafanya vizuri akiwa na timu yake Tp Mazembe.

Picha kwa hisani ya Fullshangwe.blogspot.com

4 comments:

  1. Pole mwandishi. Lakini usisahau kuwa soka letu ni lakiwango hiki hiki, wala kukosekana kwa mtu mmoja isiwe sababu ya matokeo haya. sidhani kama Samata ni mtu wa kutumainiwa kwa kiwango hicho wewe unata kutuambia hapa. Mwandishi wa michezo nitamuelewa sana atakapowabana TFF kuwa na program za watoto wadogo walau kwa kipindi cha miaka kumi hivi halafu ndiyo tuhoji kwa nini timu haijashinda. Utashangaa utapata watotot ambao ukimuacha mmoja ndiyo umechochea hamasa ya ushindi zaidi kwa walioitwa. Huwezi kulazimisha Corolla ikimbie speed ya Range lover wakati speedometer ya corolla inaishia 180 km/h na ya Range ina 280 km/h. Wakati Maximo akiwepo waandishi hawa hawa mliwahi kumpigia debe sana mshumbuliaji mmoja akiitwa Athumani Machupa, Maximo alimaliza ubishi kwa kumuita alichokifanya Machupa uwaja wa taifa kama ni wafautiliaji wazuri wa performance za wachezaji mtakuwa mnakumbuka.

    Ninachoshauri mimi ninyi waandishi wa habari za michezo muwe na mitazamo huru na inayozingatia hali halisi ya timu nzima. Huwezi kuwa na timu ya wachezaji ambao walipokuwa wakisoma shule za msingi waliambiwa hakuna michezo mashuleni halafu baadaye wakawa wa kiwango cha wachezaji wa ki-ghana au ki-cote! never. Muache kuandika kwa mitazamo ile munayoipanga kule kwenye nanihii munakoambiana ukimuona mwenzio uvute kwa namna yoyote ile. Kwa nini hamjahoji Thomas Ulimwengu yuko wapi maana hao wote ni vijana wanaotakiwa kuendelezwa. Kwa mitindo hii ya kibaguzi mtafungwa sana. Kuna wacheza wazuri chungu nzima nchi hii lakini mkishagundua siyo mwenzenu hata kumutaja jina tu ni nongwa.

    ReplyDelete
  2. habari kaka shaffih mimi napenda sana soka, imi ni mdada napenda sana sana sana namizwa na viongozi, mackocha na wachezaji wenyewe, tufike mahali tuseme asante kwa maximo, japo halaiki ilimponda sana, nimekuwa nikikata tamaa hata kwenda kuangalia mechi za Taifa starz kwa sababu kubwa kuogopa kuumia kwa kufungwa, naona bora kesho yake niblog kwako nione, hii ni kwasabu hawana au hawatoi mvuto kwa mashabiki,na wapenzi wa soka. jamani vijana wadogo wanaochipukia wapo waitwe waunde timu ya taif nzuri na imara. tujifunze hata kwa hawa tuliocheza nao leo, wamepikwa tangu 2006 leo ije kuwa sisi tunakurupuka tu kutoka huko tutokako na kupasha siku 2 au 3 tu kisha tunawavaa jamii iliyoandaliwa vizuri, si vizuri jamani kocha pamoja na wadau wengine wakae waone huyu ibilisi anayetushikilia sisi kila mara anaitwa nani katokea wapi na wamkemee nasi siku moja tuone timu yetu kwenye nusu au robo fainali ya World cup jamani, kaka natamani sana kuongea mengi maana ninauchungu sana na timu yangu. kwa upande mwingine kama tumeshindwa kumkeamea huyu ibilisi kwa wakaka basi tumzibiti kwa wadada nao asiwaharibu pia, maana hao kidogo nyota inang'aa huenda tukaona neema kupitia wao, KAKA NAUMIZWA SANA NA MATOKEO MABOVU YA TIMU YETU HASA YA TAIFA STARS.

    Ndimi mpenzi, mdau na shabiki wa timu zetu za TANZANIA, NAITWA LUCY IZENGO,

    MUNGU IBARIKI TANZANIA,
    MUNGU IBARIKI TAIFA STAZ NA TWIGA STAZ AMINA.

    ReplyDelete
  3. Kaka shafi napingana na wewe.

    Kwa muda mrefu kumejengeka tabia ya waandishi ya habari za michezo kutoa uchambuzi wa michezo kwa kutegemea matokeo ya mechi husika.Mathalani ikitokea siku timu imeshinda, mchambuzi atatoa uchambuzi wenye kuonyesha ubora au uimara wa timu iliyoshinda huku mapungufu yakiwekwa kapuni (hata kama mapungufu yalikuwepo mengi tu). Wachezaji watapambwa na kusifiwa pasipo kifani utafikili walicheza mpira kama ule tunaoushuhudia ukichezwa na timu bora barani ulaya! Vilevile, wachambuzi hawa wamekuwa na mtazamo wa kuangalia performance ya mchezaji mmoja mmoja zaidi, wakati mpira wa kisasa unategemea zaidi timu kucheza pamoja yaani teamwork. Kuna timu zina wachezaji hawana majina makubwa lakini zinaogopwa kwa mchezo wao wa pamoja. Mfano mmoja ni Napoli ya italia! Kwa bongo si ajabu kusikia timu haikushinda kwa sababu mchezaji fulani alikosekana!

    Lately kumekuwa na habari kwenye media eti national team jana haikushinda kwa sababu mbwana samatta hakuwepo. Napingana na hoja hii. Hiyo ni short sight, huyo ni mtu mmoja na sio kweli kama ana uwezo kama inavyoelezwa. Waandishi na wachambuzi hawa wanapaswa kuwa makini na wanayoyaongea. Wakati wa maximo wananchi wakisukumwa na waandishi/wachambuzi hawahawa walikuwa wakimshinikiza kocha kuchagua wachezaji fulanifulani. Leo hii watu haohao wanamponda mzungu pulsen wanasema afadhali ya maximo!. Jamani huyo mzungu habahatishi! hiyo ni taaluma yake kaisomea! Huyo ni mtaalam wa ngazi ya juu haitaji wiki nzima kumtazama mchezaji na kujua kama anamfaa au la!. Kwa mtazamo wangu, mwalimu alipata fursa ya kumwona samatta na naamini hata maamuzi ya kumwacha yalizingatia uchambuzi wake wa kitaalam kama mwalimu. Siamini kama angeweza kumwacha tu pasipo na sababu ya msingi, kwani timu ikishinda ni sifa kwake pia!.


    Kwa upande mmoja tunatambua kuwa waandishi/wachambuzi wanapaswa kuandika au kusema! Kwao hii ni kazi! Na naamini wanalipwa kwa kazi hiyo! Hivyo ni lazima waseme au waandike! Lakini kwa upande wa pili naamini waandishi wana jukumu la kutoa taarifa sahihi pasipo kupotosha umma. Na ili waweze kutoa taarifa sahihi wanapashwa wajielimishe ili wajenge ‘competence’ kwenye eneo hili. Kwani si kila mtu anaweza kuandika habari za michezo, ni lazima awe amepata taaluma ya michezo! Jamani michezo ni taaluma inasomewa kama zilivyo taaluma zingine. Nimesema hivi kwa sababu ni rahisi kwa mwananchi wa kawaida kuamini kile anachokisoma au kukisikia kwenye media.

    Mtazamo wangu kuhusu michezo hapa nchini ni kuwa tunahitaji kufanya uchambuzi mpana zaidi wa mfumo mzima wa mpira nchini na kuufanyia kazi. Mfano Je kuna Sera na Mkakati na Programu kuhusu michezo? Je kuna mfumo wa kitaasisi wa kutekeleza sera, mkakati na program? Je mfumo unakidhi au unahitaji maboresho? Je sera, mkakati na program vinatafsiriwa vipi kivitendo? Je mfumo unatoa fursa ya utambuzi, ukuzaji na uendelezaji wa vipaji? Muundo wa timu zetu ukoje? Je mfumo wa timu zetu unatoa fursa ya utambuzi, ukuzaji na uendelezaji wa vipaji?
    Vinginevyo hizi hadithi za kulaumu makocha na wachezaji hazitaisha NG’O!

    Mdau wa Michezo,
    George

    NB;nilituma habari hii kwenye email yako info@shaffihdauda.com nikaambiwa hiyo email haipo.

    ReplyDelete
  4. Asalam alaykum wadau,
    Nakushkuru sana kaka Shaffih kwa kutupatia maelezo/maoni/ushauri wa kina kuhusu soka la Tanzania. Hii ni faraja kwangu binafsi na baadhi yetu kwani tunapata sehemu ya kuanzia ama kuongezea pale ulipopaacha wewe.
    Sikuweza kuiona mechi hii lakini kutoka na malezo yako nimepata picha fulani na mimi sasa naendeleza kidogo kama ifuatavyo:
    Sijui pattern or system or formation waliyocheza lakini ki uhalisia kama walikuwa beki wa kati wanakwenda pembeni kuficha nafasi ya Mwasika nadhani huu ni utaratibu hasa pale timu inapomtumia beki kama winger ama kiungo, na hapo ilitakiwa viungo wa kati (Nditi/Kazimoto)na/au mawinger (Nizar/Barnabas) kuingia kati kuficha nafasi iliyoachwa na beki wa kati aliyekwenda kumfichia makosa beki wa pembeni huku Mwasika (beki wa pembeni) akirudi kwa style ya kuingia kati. System hii huchezwa zaidi timu inapocheza 4-4-2 au 4-4-1-1.

    Kwa suala la timu kufanya vibaya naweza kusema inatokana na wachezaji kutokujiami, wachezaji wetu hawajiamini hata kidogo, wamezidiwa na papara kuanzia mabeki mpaka wafungaji isipokuwa kwa wachache sana ambao nathubutu kuwataja kuwa ni Shaaban Nditi, Mbwana Samatta na Shomari Kapombe. Wadau wanapiga kelele Samatta Samatta Samatta nawaunga mkono japo kuwa hawajui undani na ukweli wa Samatta. Uzuri wa Samatta ni utulivu anapokuwa na mpira ambao unamjengea kujiamini, kitu ambacho asilimia kubwa ya wachezaji wanakikosa. Chukulia mfano mechi ya nyumbani tulipocheza na Algeria, goli alilofunga Samatta ni kutokana na utulivu na kujiamini. Tunahitaji wachezaji wa namna hii na ndio maana wadau wanataja Samatta.
    Wachezaji wenye utulivu na kujiamini wanaweza kupatika kuanzia soka la yosso (vijana wa umri mdogo), mchezaji anapoanza kucheza soka la ushindani akiwa mdogo anajijenga kujiamini, sio leo mtu ana miaka 27 (ya ukweli 35)ndio anaanza kucheza timu ya Taifa kwa mara ya kwanza, hivi unadhani kutakuwa na kujiamini hapo?
    Wakati umefika kwa TFF (kamati ya ufundi/kocha) kuwaamini vijana, hii namaanisha kwa vile hivisasa wapo vijana wengi walioibuliwa kutoka michuano mbali mbali, kama vile Uhai Cup, Coca cola n.k inapotokea mashindano basi tusilenge kwamba lazima tuchukue kombe, badala yake watumiwe vijana ili kuwajengea kujiamini na utulivu, hii itasaidia kwa michuano ya baadae ambapo tutakuwa na timu nzuri na imara yenye kujiamini, wenzetu ndivyo wanavyofanya hivyo, wachezaji kama Henderson,Sturridge, Welbeck, Walcott na wengineo ndivyo wanavyokomazwa. Kama tunakumbuka mchezo wa kirafiki kati ya Stars na Zambia uliochezwa Morogoro na matokeo yalikuwa 1-1, Zambia walichezesha vijana wengi ambao kimsingi walikuwa wanawapa ukomavu, na ndio vijana wale leo walioiletea heshima nchi yao. Lakini kwetu ikitokea hata Stars inacheza mechi ya kirafiki hakuna sura mpya za vijana wanaokomazwa. Hapo ndio tunamkumbuka Marcio Maximo pamoja na lile la kuhamsisha wachezaji na wananchi kuipenda timu yao.

    Maasalaam.

    Bebeto.

    ReplyDelete