Search This Blog

Saturday, January 14, 2012

KIIZA AWAFUNIKA AKINA OKWI NA OCHAN UGANDA - ABEBA TUZO


Straika wa kimataifa wa Yanga, Hamis Kiiza alichaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Mwaka wa nchini kwao Uganda na kuwapiku nyota wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya na pia Emmanuel Okwi wa klabu ya Simba yenye uhasama wa jadi na timu yake, ‘Wekundu wa Msimbazi’, Simba.

Kiiza alishinda tuzo hiyo inayoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Uganda (USPA) baada ya kupigiwa kura nyingi kutokana na kiwango cha juu alichoonyesha katika msimu wa 2010/2011.

Mbali na Okwi ambaye hakukaribia hata 3-bora, wengine waliofunikwa na Kiiza katika kuwania tuzo hiyo ni Dennis Onyango anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini, Andy Mwesigwa anayeichezea klabu ya Ordabasy ya nchini Kazakhastan na David Obua anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Heart ya nchini Scotland.

Akizungumzia tuzo hiyo, Afisa Habari wa klabu ya Yanga, Luis Sendeu, alisema kuwa wao wamefurahia tuzo aliyotwaa Kiiza na wanaamini kuwa mafanikio yake yametokana na juhudi anazoonyesha uwanjani wakati akiitumikia timu ya taifa lao, ‘The Cranes’ na pia mchango anaoutoa wakati akicheza katika ngazi ya klabu.

"Mashabiki wa Yanga wamefarijika na tuzo hii ya Kiiza. Tunaungana naye kusherehekea tuzo hiyo ambayo ina heshima kubwa kwani amewashinda nyota wengi wa soka nchini kwao," alisema Sendeu.

Kiiza alifanya vizuri akiwa na timu ya URA katika msimu wa 2010/2011 ambapo aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uganda baada ya kufunga mabao 14.

Pia aliibuka kuwa mchezaji bora katika mashindano ya Bell yanayofanyika kila mwaka nchini mwao.

Baada ya mafanikio hayo akiwa URA, Kiiza alijiunga na Yanga na kuisaidia kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’ na pia aliisaidia 'The Cranes' kutwaa ubingwa wa Kombe la Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Chalenji) lililoshindaniwa Desemba jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment