Search This Blog

Monday, January 2, 2012

Iko wapi ile kasi waliyoanza nayo BMT mpya?


Imani Makongoro
NI saa 24 zimepita tangu watu wa mataifa mbalimbali ikiwamo Tanzania waliposherehekea Sikukuu ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2012 na kuuaga ule wa 2011.
Tunamshukuru Mungu kwa kukufikisha kuona mwaka mpya najua ni wengi walitamani kuiona, lakini kwa mapenzi yake yeye muumba Mbingu na Ardhi hawakufanikiwa kuiona.
Kama kawaida nao mwaka 2011 umemalizika bila mabadiliko yoyote katika sekta ya michezo ambayo uwezo kwenda kokote ulimwenguni lazima utakutana nayo isipokuwa kama; hautaki michezo na utamaduni, haupendi michezo na utamaduni, haujui maana ya michezo na utamaduni, unafanya makusudi kukataa michezo na utamaduni, hauoni faida ya michezo na utamaduni na mengi mengineyo.
Wakati mwingine huwa nafikiria kwamba viongozi wa michezo na utamaduni wameingia madarakani hapa nchini wakati siyo wapenzi wa michezo na utamaduni kwa dhati na wanaangalia zaidi maslahi yao binafsi badala ya kuendeleza michezo na utamaduni nchini.
Mfumo wa michezo na utamaduni uliopo nchini unaonyesha wazi maendeleo ya michezo na utamaduni ni wajibu wa Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Elimu, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) pamoja na vyama vya michezo.
Kama mtakumbuka vizuri Oktoba 5 mwaka jana Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emannuel Nchimbi alizindua rasmi Baraza jipya la Michezo la Taifa kutoka lile la zamani lililokuwa chini ya Kanali mstaafu Idd Kipingu.
Baraza hilo likiongozwa na mwenyekiti Dioniz Malinzi, Katibu Mkuu, Henry Lihaya na wajumbe wengine 11 walioteuliwa na Wizara hiyo ambao wangeshirikiana bega kwa bega na vyama vya michezo hapa nchini siku hiyo walitema cheche zao na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kuinusuru michezo ya Tanzania.
Malinzi alitoa ahadi mbalimbali ikiwamo kufanya mabadiliko ndani ya mwaka mmoja tofauti na ile mitatu aliyopewa na Waziri Nchimbi ambapo angeshirikiana na vyama vya michezo vilivyowakilishwa na Makatibu wakuu wake ambao ni wajumbe wa Baraza hilo.
Wakati Malinzi akikabidhiwa rungu hilo la kuendesha gurudumu la BMT kwa ajili ya maendeleo ya michezo yetu moja ya mikakati yake ilikuwa ni vyama kuwa na mipango endelevu huku akiahidi yeye kusimama kidete ili kuhakikisha hilo linafanyika ndani ya muda mfupi.
Mbali na hilo mwenyekiti huyo kwa kushirikiana na wajumbe wa BMT walipeana mikakati mbalimbali sambamba na kugawana majukumu yaliyonekana kuleta ahueni kwa taifa katika kuokoa sekta yetu ya michezo iliyopoteza dira.
Kuna msemo usemao, 'Mbio za Sakafuni Uishia Ukingoni,' ndivyo ilivyokuwa kwa mikakati ya Baraza hilo jipya wakati ule na sasa unaweza usinielewe namaanisha nini, lakini ukweli ni kwamba BMT ile ya ahadi imegeuka 'bubu' katika utekelezaji.
Leo ni Januari 2, siku zinazidi kukatika tangu ile ahadi ya Mabadiliko katika michezo itolewe na siku tatu zimesalia ili ahadi hiyo itimize miezi mitatu ya maneno bila utekelezaji.
Unaweza kuona ni muda mfupi, lakini ukweli ni kwamba miezi mitatu ni mingi sana na Watanzania wengi tulitarajia kuona cheche za BMT ndani ya muda mfupi tu ambazo zingevikumbusha vyama vinatakiwa kufanya nini kutokana na ule moto iliyoanza nao mara baada ya Baraza hilo jipya kuzinduliwa.
Lakini moto BMT waliouwasha Oktoba 5, umekuwa ni wakifuu kwani kila siku zinavyokwenda hakuna mabadiliko yoyote ya maana yaliyotokea katika kipindi hiki cha miezi mitatu.
Mwaka mmoja wa BMT wa kuleta mabadiliko katika sekta yetu ya michezo umegeuka mwaka wa viongozi wa vyama kurumbana bila sababu za msingi yote ikiwa ni uchu wa madaraka bila kuzingatia maadili na umuhimu wa kuleta maendeleo ya kweli katika mchezo.
Hivi viongozi wakurumbana kisa madaraka tena si kwa manufaa ya michezo bali kwa maslahi yao binafsi tunategemea kitu gani zaidi ya kujichimbia shimo ambalo tutatumbukia wenyewe.
Sidhani kama Baraza letu lenye dhamana ya kusimamia michezo hapa nchini haya ndiyo mliyotuahidi awali yanatekelezwa kwa sasa, ile mikakati yote imeishia pale uwanja wa Taifa ilipokuwa ikipangwa huku uozo katika vyama ukizidi kila siku inapokwisha na kuanza siku mpya.
Nilitegemea uozo huo ungekuwa wa kwanza kuvumbuliwa katika vyama sambamba na kuchukuliwa hatua ili iwe fundisho, lakini ni kama mmenyeshewa na mvua mara tu baada ya kuanza kazi rasmi kutokana na ukweli kwamba yote mliyotuahidi hakuna hata moja lililotekelezeka.
Imekuwa ni kawaida ya viongozi wa vyama vya michezo kutokuwa wakweli hasa katika masula ya mapato na matumizi, lakini yote hayo yamefumbiwa macho na BMT ambayo tuliitegemea kama mkombozi wetu katika michezo.
Uozo ndani ya vyama umekithiri ili hali wanaoathirikia ni wanamichezo imefikia mahali hata misaada inayotolewa na wahisani kwa ajili ya kusaidia timu zetu inaishia mikononi mwa wachache ambao wanajiita viongozi wa michezo, lakini hadi leo hii yale tuliyoahidiwa kwamba yatakomeshwa hata mfano wake haujaonekana.
Kwa bahati nzuri Malinzi alikuwa kiongozi wa Gofu kabla ya kuwa mwenyekiti wa BMT hivyo anaelewa vizuri yanayotendeka nyuma ya pazia.
Mwaka mmoja mlioahidi kwa ajili ya mabadiliko inazidi kuyoyoma na sasa mmebakiwa na miezi tisa kwa ajili ya ile ahadi ya michezo ya manufaa kwa taifa ndani ya vyama zaidi ya 40.
Tunahitaji kutimiza zile ahadi kama tunataka kuona watanzania wanapata kile walichotarajia katika michezo yetu, suala la kujuana na kuoneana aibu limepitwa na wakati tufanye kazi kwa kuzingatia maslahi ya taifa na wanamichezo wetu kwa kutimza ile ahadi mliyoitoa.
Pia, waziri Dk Nchimbi anatakiwa kuhakikisha BMT, inapewe nguvu zaidi kifedha ili liweze kuvisaidia vyama hivi, lakini pia liwe na nguvu ya kutengua mamlaka ya viongozi ambao siyo waadilifu katika vyama hivi vya michezo.
BMT ni kama ipo haipo kwa kuwa haijaving'ata vyama, BMT haijakwenda ndani ya vyama kuona matatizo ni nini, na kubakia ofisini kulinda mafaili ya vyama.
Ninaamini hatutaweza kupata maendeleo ya kweli ya michezo nchini kama serikali haitaliboresha BMT iwe na ofisi za kisasa na kuliwezesha kuwa chombo kikuu cha kusimamia michezo kiutendaji kwa kulipa fedha za kutosha katika bajeti ya kila mwaka.

No comments:

Post a Comment