Search This Blog

Tuesday, January 3, 2012

FIDIA YA KIMBANGULILE KWA SAMATA.

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya uenyekiti wa Alex Mgongolwa ilikutana Desemba 30 mwaka jana kupitia masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake ikiwemo taarifa ya uamuzi wa timu ya Kimbangulile kukata rufani Kamati ya Rufani kupinga uamuzi wake juu ya mchezaji Mbwana Samata.
Ikumbukwe kuwa Kimbangulile iliwasilisha malalamiko TFF ikieleza kuwa inastahili malipo baada ya Simba kumuuza Samata kwa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Kimbangulile ilitaka ilipwe fidia ya mazoezi (training compensation) na mchango maalumu (solidarity contribution) kwa mujibu wa Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Uamuzi wa Kamati ya Mgongolwa ulikuwa Kimbangulile imeshindwa kutoa vielelezo kuonesha kuwa iliingia gharama za mazoezi kwa mchezaji husika wakati akiichezea timu hiyo. Kwa upande wa solidarity contribution ambayo ni asilimia 5 ya mauzo ya mchezaji huyo TP Mazembe, fedha hizo zinatakiwa kulipwa na klabu yake hiyo mpya ambayo TFF itaitaka kufanya hivyo wakati Samata atakapoombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
Hivyo Kamati itatengeneza utetezi wake na kuuwasilisha kwenye Kamati ya Rufani itakaposikiliza rufani ya Kimbangulile.

USAJILI WA DIRISHA DOGO 2011/2012


Kwa upande wa Daraja la Kwanza, Kamati hiyo imetoa siku saba kwa klabu ambazo zimezidisha idadi ya wachezaji ili zipunguze, kwani kila timu inatakiwa kuwa na wachezaji wasiozidi 30. Klabu nyingi baada ya kufanya usajili wa dirisha dogo zimepitisha idadi ya wachezaji 30 wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni.
Hivyo kwa klabu ambayo itashindwa kupunguza wachezaji ndani ya muda huo, TFF itahesabu hadi 30 na wachezaji watakaokuwa wamezidi wataondolewa. Kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), klabu ya Villa Squad ndiyo imekutwa na kasoro katika usajili wake ambapo imetoa kwa mkopo wachezaji wanne na imepokea wengine watano kwa mkopo.
Kwa mujibu wa kanuni ya mkopo, klabu haitakiwi kuwa na wachezaji zaidi ya watano iliotoa au kuingiza kwa mkopo kwa wakati mmoja. Hivyo Villa Squad imetakiwa kuwaandikia barua za kuwaacha wachezaji wanne iliowatoa kwa mkopo ili wawe huru (free agents). Pia Kamati imeagiza viongozi wa juu wa Majeshi ambayo yanamiliki timu za mpira wa miguu kupewa elimu ya kanuni za usajili, kwani mafunzo ya kijeshi na uhamisho wa wachezaji ambao ni askari vimekuwa vikiathiri viwango vya timu zao kwenye ligi.



SIMBA KUMSIMAMISHA KOCHA BASENA



Malalamiko ya Kocha Moses Basena kwa TFF baada ya klabu yake ya Simba kusimamisha mkataba wake yaliwasilishwa mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji. Baada ya kupitia malalamiko hayo, uamuzi wa kamati ni kuwa suala hilo liendelee kuwa kati ya Simba na Basena na kuwataka wakae pamoja ili waweze kulipatia ufumbuzi.



Licha ya Basena kuwa na mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, Kamati imebaini kuwa hauwezi kufanya kazi (functional) kwa vile kocha huyo hakuwa na kibali cha kufanya kazi nchini (work permit).



Hivyo kisheria hakukuwa na mkataba kwa vile ili Basena aweze kuitumikia Simba ni lazima awe na kibali cha kufanya kazi nchini. TFF ilikataa maombi ya Simba kuiandikia barua Idara ya Uhamiaji kuthibitisha barua ya kumuombea work permit baada ya kocha huyo kushindwa kuwasilisha vyeti vyake vya ukocha.



Kwa vile Simba imeshaajiri kocha mwingine (Milovan) kwa mkataba wa miezi sita na kupatiwa kibali cha kufanya kazi nchini, ufumbuzi wa suala la Basena unabaki kuwa kati ya klabu hiyo na kocha huyo.

2 comments:

  1. kaka shafih mi nilijua 2 lakini ukweli samata kalelewa hapo kimbangulile kama unataka kujua hilo watafutekimbangulile saleh aka morighno wa kimbangulile au mzee samata mwenyewe.

    ReplyDelete