Search This Blog

Tuesday, December 27, 2011

Uteuzi huu ni kwa ajili ya Nishani za Uhuru?

Na Fred Mwakalebela
TANZANIA Bara iliyokuwa ikifahamika kama Tanganyika kwa sasa ina umri wa miaka 50 na siku kama 10 hivi, umri ambao kwa hakika ni wa mtu mzima kabisa.

Jina la Tanganyika kwa mujibu wa historia lilianza kutumika kama miaka 100 tu iliyopita likiunganisha sehemu ya mwambao mwa Bahari ya Hindi na ukanda wa misitu (nyika) magharibi mwa pwani hiyo.

Wakati wa utawala wa kikoloni chini ya Mjerumani, eneo hili lilijulikana kama ‘German East Africa (Deutsch-Ostafrika)’ likijumuisha pia nchi za Burundi na Rwanda likiwa na ukubwa wa karibu mara tatu ya Ujerumani ya sasa.

Ni hapo ndipo wadau wa soka wanaposhangaa iweje mkoloni wetu wa zamani, Ujerumani, nchi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 384,170 tu, leo hii ni miongoni mwa miamba wa soka duniani huku sisi tukiendelea kung’aa macho?

Jibu ni rahisi sana, hatuna vipaumbele. Na kama tunavyo, vina baki midomoni na kwenye makaratasi tu, havitekelezwi na wala wanaopaswa kuvitekeleza hawajali.

Wiki iliyopita anga la soka nchini lililokuwa likitarajiwa kugubikwa na mijadala kuhusu kiwango cha soka lilichoonyeshwa na timu zetu za taifa, Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes kwenye michuano ya CECAFA Challenge Cup, lilibadilika na kuanza kujadili uteuzi wa makocha watakaoshiriki mafunzo ya wiki moja ya CAF.

Kila mmoja, shabiki na hata kiongozi wa soka, anafahamu namna gani soka la vijana nchini limekuwa likipigiwa kelele na jinsi lilivyozibeba nchi kadhaa duniani zilizotilia maanani maendeleo ya vijana.

Ujerumani (wakoloni wetu hawa) ni moja kati ya mifano hai. Kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka jana, wachezaji wa Ujerumani wakifuatiwa na wa Ghana ndio waliokuwa na wastani mdogo zaidi wa umri, ikimaanisha kuwa nchi hizo zitaendelea kutesa katika soka la kimataifa kwa muda mrefu ujao.

Nilitumaini kabisa kuwa inapotokea nafasi ya mafunzo kama haya ya CAF, makocha vijana, au hata kama si vijana, wale wanao ‘practice’ kazi hii kila kukicha, ndio walipaswa kupewa nafasi ya kushiriki ili kuwabeba wachezaji wadogo (watoto) na vijana kwa manufaa ya baadaye ya nchi yetu.

Lakini cha ajabu mengi miongoni mwa majina ya washiriki hao ni wale wanaokaa maofisini wakiwa na shughuli nyingine kabisa mbali na soka, au hata kama wanajishughulisha na soka, si lile soka hasa la kwenye ‘field’.

Mifano ni wazi, Leodegar Tenga kwa sasa ni Rais wa TFF na Mwenyekiti wa CECAFA na huenda hajafanya kazi za ukocha tangu alipofanya hivyo miaka ya mwanzoni ya 1980 akiifundisha Pan African.

Mwingine ni Kassim Majaliwa. Yeye ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI. Sina uhakika kwa majukumu aliyonayo kwenye wizara nyeti kama TAMISEMI atakuwa na nafasi ya kufanya kazi ya ukocha kwa kipindi hiki hadi 2015.

Joel Bendera, mmoja wa makocha wenye heshima kubwa nchini naye atakuwamo kwenye kozi hiyo, lakini kwa majukumu aliyonayo sasa ya ukuu wa mkoa wa Morogoro, mkoa unaokumbwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji; ajali za barabarani; ujambazi na nyakati nyingine mafuriko, atapata nafasi ya kuendeleza soka la vijana uwanjani?

Sidhani, labda majukwaani na huko hakuna haja ya kupewa mafunzo ya wiki nzima na CAF. Hata akina Salum Madadi na Mshangama kwa sasa wamekuwa ni viongozi wa kisera zaidi, hivyo walipaswa kuwapa nafasi makocha waliopo kwenye ‘field’.

Eugene Mwasamaki, bosi wa chama cha makocha naye amejiweka kwenye orodha ya watakaopata mafunzo hayo bila kuwaeleza Watanzania ni vigezo vipi walitumia kuteua washiriki, naye ananishangaza kwa kiasi kikubwa.

Jamani, tunalipeleka wapi soka la Tanzania? Timu ya vijana majuzi imerejea kutoka Gaborone, Botswana ilikokuwa imealikwa kushiriki mashindani ya vijana ya COSAFA Castle Cup na kuonyesha kiwango bora, kweli miongoni mwa waheshimiwa hawa kuna atakayerejea kuifundisha tena timu hiyo? Labda… lakini sina uhakika hata kwa hili.

Kwa muda sasa, NMB imekuwa ikisaidia mafunzo kwa makocha wa soka na tayari zaidi ya makocha 2,000 wamehitimu mafunzo hayo na wapo tayari kuendeleza soka la vijana. Ni nani kati ya watakaoshiriki kozi ya CAF imetokana na mafunzo hayo ya NMB?

Kweli tunawaacha akina Kenny Mwaisabula (TEFA Technical Director), Joseph Kanakamfumu (kocha kijana mwenye shahada) na Salum Mayanga wa Kagera Sugar kwenye kozi hii, kama si kujitakia lawama ni nini?

Wasiwasi wangu ni kwa waheshimiwa hawa walio na majukumu mengi ya kitaifa kama kweli watapata nafasi ya hata kushiriki kozi yenyewe kwani sina uhakika kuwa ‘sitting allawance’ (kama ipo) italingana na ile waliyoizoea.

Na ndio maana mimi niliposikia majina haya redioni na kwenye runinga sikuamini. Kwanini? Kwa kuwa nilidhani na kuamini kabisa kuwa huenda majina haya yalikuwa ni kwa ajili ya kutunukiwa Nishani za Miaka 50 ya Uhuru.

Nilipoamka kesho yake na kuyakuta gazetini na kuhabarishwa kuwa ni kwa ajili ya kozi ya ukocha, nilichoka kabisa. Nikajiuliza, hivi waheshimiwa hawa, kabla ya kutangazwa, walikuwa wamewasiliana na waliowateua na kukubaliana? Wanadhani kushiriki kwao kutakuwa na tija kwenye soka letu, hasa la vijana?

Hakika hawa walipaswa tu kuwamo miongoni mwa watunukiwa wa Nishani za Uhuru zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete Desemba 9 mwaka huu. Bado tuko pamoja… ila tutekeleze kwa vitendo vipaumbele tulivyo navyo.

2 comments:

  1. Nilikuja kushangazwa na kauli ya TFF, Kenny alipohoji juu ya uteuzi wa washiriki, walisema kwa ufupi 'wangoje wakati wao ukifika utateuliwa'.

    Kwa hali hii hata kuvunja kikosi cha stars haito saidia kulinusuru soka letu bro.

    ReplyDelete
  2. Mwakalebela kwa makala hii nakupa pongezi sana, tena zaidi.

    Hii nchi bwana mimi nafikiri kuna mahali (wakati) yalifanyika makosa tena makubwa kwelikweli! Kuna butch ya umri fulani miongoni mwa Watanzania ni kizazi kibovu kabisa. Matatizo ya maamuzi ya hovyo hovyo sasa hivi yako kila sekta, iwe kwenye siasa, michezo, uongozi nk.

    Sijui ni tamaa au uvivu wa kufikiri!

    Aliyehusika na kuwateua hao VIP alifikiri watamuona wa maana kumbe wanamshangaa.

    Ndiyo maana kuna siku moja katibu mkuu wa TFF alikuwa kwenye kipindi fulani cha michezo radio one akasema timu zetu hazifanyi vizuri eti kwa sababu zinakosa bahati tu! Ni kichekesho kabisa! Kama kiongozi wa ngazi ya juu namna hii anaamini hivyo unategemea kutakuwa na mipango madhubuti ya kuinua viwango vya michezo?.

    We are lost in the bush.

    ReplyDelete