Search This Blog

Wednesday, December 14, 2011

TFF: SIMBA ISINGEACHANA NA BASENA SISI TUNGEMSIMAMISHA



Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema lilikuwa mbioni kumsimamisha aliyekuwa kocha wa Simba, Mganda Mosses Basena kwa madai ya kutokuwa na vyeti vya taaluma vya kazi hiyo.

Akizungumza kwenye makao makuu ya shirikisho hilo jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema waliwasiliana na Simba zaidi ya mara tatu kuwaomba wawasilishe vyeti vya
kocha huyo, lakini walishindwa kufanya hivyo.

“Tuliwaomba watuletee vyeti vya kocha wao zaidi ya mara tatu lakini hawakufanya kama tulivyowaagiza,” alisema Osia.

Alisema wakiwa mbioni kumsimamisha kocha huyo, ndipo uongozi wa Simba ukatangaza kumtupia virago kocha huyo.

Osiah aliongeza huwa hawana utaratibu wa kukimbilia kutoa adhabu na badala yake wanaanza kufanya mawasiliano na upande unaohusika kuhusiana na jambo lenyewe ikishindikana ndipo hutoa adhabu.

Kocha huyo kutoka Uganda aliweza kufanya kazi zaidi ya miezi mitatu bila kuwa na vyeti vya kazi ya ukocha, ambapo Simba ilimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa inaongoza ligi hiyo.

Hivi karibuni uongozi wa Simba ulimleta kocha Milovan Cirkovic kutoka Serbia wakati bado una mkataba na Basena.

Viongozi wa Simba walidai Basena bado kocha wao na kuwa walifikia uamuzi huo kwa vile kocha huyo Mganda hakuwa amewasilisha vyeti vyake na kwamba walichokifanya ni kusitisha mkataba wake, huku kocha huyo akisisitiza Simba imlipe fungu lake kwa kuvunja mkataba.


No comments:

Post a Comment