Search This Blog

Thursday, December 15, 2011

Mechi 6 kubwa zinazoweza kushuhudiwa kwenye hatua ya mtoano wa Ligi ya mabingwa.


Hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani ulaya kwa msimu wa mwaka 2011-12 imekamilika na msisimko kwa sasa umehamia kwenye michezo ya hatua ya 16 bora . Hatua ya 16 bora itashuhudia michezo mikali ambayo ratiba yake itapangwa siku ya ijumaa .
Mashindano ya mwaka huu yamekosa huruma kwa washindi wa pili wa msimu uliopita Manchester United ambao wametolewa kwenye hatua ya makundi baada ya kuwa na kawaida ya kupita hatua hiyo kwa wepesi kwa miaka mingi na sasa wamebakia na Ligi ya UEFA Europa kama michuano pekee mikubwa ya kujaribu kutwaa.
Sambamba na United ni mahasimu wao toka jiji la Manchester Man City chini ya Roberto Mancini

Huku timu zilizofuzu raundi inayofuata zikiwa tayari zinafahamika , ijumaa hii timu hizo zitagawanywa katika michezo nane ya hatua ya 16 bora ambapo shughuli itakuwa kufuzu hatua ya robo fainali michezo itakayopigwa mwezi Februari 2012.

Kama zisemavyo sheria za hatua ya mtoano , timu nane zilizoongoza makundi husika zitakuwa kwenye sanduku moja huku washindi wa pili wakiwa kwenye sanduku lingine . Timu zitapangwa kucheza katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini huku timu zilizongoza makundi zikiwa na faida ya kucheza michezo ya marudiano kwenye viwanja vya nyumbani.

Vigezo vinavyozingatiwa katika upangwaji wa ratiba za michezo ni kama timu zinazotoka kwenye shirikisho au chama kimoja cha soka haziewezi kukutana kwenye mchezo katika hatua hii na timu zilizokuwa kwenye kundi moja pia haziwezi kukutana.
Kwa maneno rahisi Chelsea haiwezi kucheza na Arsenal kwa kuwa zote zinatoka England na Bayern Munich haiwezi kupangwa na Napoli kwa kuwa timu hizi zilikuwa kundi moja.
Baada ya kuyaona hayo tuone baadhi ya michezo ambayo inaweza kushuhudiwa katika hatua hii.


Internazional Milan vs. Olympique Marseille

Inter Milan na Olympique Marseile zimewahi kutwaa ubingwa wa ulaya miaka ya nyuma . Inter wametwaa mara tatu na wametwaa hivi karibuni msimu wa mwaka 2010 baada ya kuwafunga Bayern Munich na Marseile wametwaa mara ya mwidho mwaka 1993 wakati waliwafunga Ac Milan .
Safari hii, Marseile wanaonekana kupata tabu kwenye michuano ya nyumbani na ukitazama wanaweza kuonekana wana nafasi ya kuwatoa Wataliano Inter Milan. Ushindi katika mchezo huu unaweza kuirejeshea Marseile Morali yao ambayo imepotea hususan kwenye ligi ya nyumbani pamoja na kampeni yao ya kurejesha ufalme wao wa ulaya uliopotea miaka ya 90.Inter kwa upande wao wamekuwa na msimu wa tabu sana kwenye ligi ya Serie A kama wenzao wa Marseile na hii ndiyo nafasi yao kubwa ya kuijenga upya klabu yao katika miezi hii ambayo Claudio Ranieri anahangaika kurejesha hali ya kujiamini kwa wachezaji wake.

SL Benfica vs. Bayer Leverkusen

Benfica ni moja ya timu zenye mafanikio makubwa sana toka nchini Ureno hususan kwenye michuano ya ulaya . Timu hii imetwaa ubingwa wa ulaya mara mbili huku ikimaliza kwenye nafasi ya pili mara tano . Hata hivyo mataji yao yote yalikuja kwa kufuatana kwenye misimu ya mwaka 1961 na 62 . Wapinzani wao wa nyumbani Fc Porto wametwaa mataji mawili ya ligi ya mabingwa katika miaka ya 1987 na 2004 lakini bado hawajapata nafasi ya kuwazidi wapinzani wao Benfica.
Nao Bayer Leverkusen wamewahi kufika fainali mara moja tu mwaka 2002 walipofungwa na bao la mwaka huo la Babu Zizou.

Arsenal vs. Napoli

Arsenal wameonekana kufanya vyema kwenye michuano ya ligi ya mabingwa na wanaonekana kuamka usingizini pia kwenye ligi ya England tofauti na mwanzoni walipoonekana kuwa na kwikwi kwenye miezi ya kwanza .
The Gunners wamekuwa na bunduki ya hatari inayofahamika kwa jina la RVP na ‘perfomance yake msimu huu inaonekana kumfanya astahili kuwemo kwenye orodha ya wachezaji watakaowania tuzo mbalimbali mwisho wa msimu.
Napoli wanajivunia silaha tatu za maangamizi , Marek Hamsik, Ezequiel Lavezzi na Edinson Cavani. Mechi kati ya timu hizi inaweza kuwa mechi yenye mashambulizi kuliko zote katika hatua hii ya mtoano.

Chelsea vs. CSKA Moscow

Chelsea haijawahi kutwaa ubingwa wa ulaya katika historia yake. Nafasi yao pekee ilikuwa kwenye mchezo wa fainali mwaka 2008 wakati walipofungwa na Man United kwa penati katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Luzhnikhi nchini Urusi.
Mechi kati ya Chelsea na CSKA Moscow inaweza kuwashuhudia Chelsea wakirudi kwneye uwanja walikolitazama Kombe la Ligi ya mabingwa likiwapita pembeni hivi hivi. Hali ya hewa ya mwezi februari nchini Urusi ni baridi kali na hiyo huwa sababu ya timu nyingi kushindwa zinapoenda kucheza nchini urusi kwenye miezi hiyo.
Chelsea wamekuwa wakipata tabu kutatua tatizo la safu ya ushambuliaji . Huku kukiwa na miezi miwili ya maandalizi kabla ya mchezo huu matatizo ya Chelsea yanaweza kuwa yamepatiwa ufumbuzi na hujui nini kitatokea Chelsea itakapokuwa imekamilika.

CSKA Moscow ilimaliza kwenye nafasi ya nne kwenye msimu wa ligi ya Uurusi iliyoisha miezi ya karibuni , na hii inamaanisha kuwa mwakani hawatacheza kwenye ligi ya mabingwa na badala yake watacheza kwenye ligi ya Europa . Walimaliza kwa sare moja na wakafungwa michezo miwili ndio sababu ya timu hii toka Moscow kumaliza kwenye nafasiya nne wakishushwa toka nafasi ya pili waliyokuwa kwa muda mrefu.Wakati The Blues wakiwa na miezi miwili ya michezo mbeleni mwao , CSKA Moscow wana miezi miwili ya kupumzika , jambo ambalo linaweza kuwafanya waondoke mchezoni hadi kufikia mwezi februari . Vijana wao Kina Seydou Doumbia na Keisuke Honda watakuwa muhimu sana kwa tmu yao kwenye hatua hii.
Mechi kati ya timu hizi inaweza kuwa na ushindani wa hali ya juu huku warusi wakiwa na hamu ya kumuumiza mrusi mwenzao Roman Abramovic ambaye kwa upande wake angependa kuishuhudia Chelsea ikitwaa ubingwa wa Ulaya.

FC Bayern Munich vs. AC Milan

Kwa kuwa Inter Milan na Bayer Munich zote zimeshika nafasi za kwanza kwenye makundi yao hatutashuhudia fainali ya mwaka 2010 ikirudiwa . Hata hivyo kuna uwezekano mkubwa sana wa mchezo kati ya wapinznai wakubwa wa Inter , AC Milan na Bayern Munich . Huu utakuwa mchezo kati ya mabingwa wa kihistoria wa Ulaya huku Milan wakiwa na mataji 7 na Bayern wakiwa na mataji 4.
Bayern ndio timu bora toka Ujerumani kuwahi kushiriki kwenye michuano ya ulaya na mafanikio yao yanadhihirisha ukweli wa hili . Msimu huu wametawala vyema ligi ya ujerumani japo wamekuja kupunguzwa kasi hivi karibuni .
Milan wako nyuma ya vinara wa Serie A kwa pointi mbili na wanaonekana kuelekea kuzuri . Perfomance ya Zlatan Ibrahimovic kwenye ligi ya mabingwa imekuwa ya wasiwasi kidogo lakini bado anayo nafasi ya kuipa mafanikio timu yake kwenye mchezo kama huu.

Real Madrid vs. AC Milan

Mchezo kati ya AC Milan na Real Madrid ni aina ya mechi ambazo watu wanaota kuzishuhudia , kama ilivyoelezwa hapo awali Milan wana mataji 7 ambayo yamezidiwa na timu moja tu nayo Ni Real Madrid wenye mataji 9.
Mafanikio ya hivi karibuni ya Milan yalikuwa mwaka 2007 baada ya kuwafunga Liverpool waliokuwa na kumbukumbu ya miujiza ya mwaka 2005 kule Istanbul.
Madrid hawajatwaa taji lingine tangu walipotwaa mara yao ya mwisho mwaka 2002 baada ya kuwafunga Bayer Leverkusen kule nchini Scotland . Wahispania hawa hawajawahi kurejea kwenye utawala wao wa kawaida kwenye michuano ya ulaya tangu utawala wa wapinzani wao Barcelona ulipoanza , hata hivyo mchezo kati ya Milan na Madrid unaweza kuwa wa kiistoria hasa ukizingatia ukweli kuwa timu hizi zina hasira kama mbogo aliyejeruhiwa zikisaka kurejesha falme zao zilizotekwa na wapinzani wao Inter Milan na FC Barcelona katika miaka ya hivi karibuni.

Mwisho.

Huku kukiwa na michezo mingine mikubwa inayoweza kuibuka kwenye hatua hii kama vile FC Barcelona na Napoli au Apoel FC na FC Basel , michezo hiyo iliyotajwa hapo juu ndiyo mikubwa inayoweza kushuhudiwa kwenye hatua ya mtoano , tungoje kuona itakavyokuwa.

1 comment:

  1. Ars8nal. Vs. Basel. Chelsea vs. Napoli. Wako. James

    ReplyDelete