Search This Blog

Monday, November 14, 2011

JAN POULSEN: BADO TUNA KAZI NGUMU SANA KWA CHAD


Head coach wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars), Jan Poulsen amesema bado wana kazi ngumu kuweza kuitoa Chad katika mchezo wa pili wa mchujo wa kuingia katika hatua ya makundi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 Brazil, hapo kesho.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa N’djamena Ijumaa iliyopita, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 kupitia kwa mshambuliaji Mrisho Ngassa na kiungo Nurdin Bakari.

Huo ni ushindi wa kwanza ugenini kwa kocha huyo aliyechukua nafasi ya kufundisha timu hiyo kutoka kwa Mbrazili Marcio Maximo zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Akizungumzia mchezo huo baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jana, Poulsen alisema Chad ni timu ngumu inayocheza mpira wa nguvu hivyo bado wana kazi ngumu kuweza kuiondosha mashindanoni.

“Nina furaha kwa sababu timu yangu imeshinda lakini tulikuwa na mchezo mgumu N’djamena,” alisema Poulsen.

Alisema wanapaswa kujituma katika mchezo wa kesho kama timu yake itataka kushinda mchezo huo na kujihakikishia nafasi ya kuingia katika makundi na kukiri kuwa kazi bado haijaisha.

Maneno hayo ya Poulsen yaliungwa mkono na kocha msaidizi wa timu hiyo, Sylvestre Marsh, aliyekiri kuwa bado wana kibarua kigumu kuitoa timu hiyo.

Alisema Taifa Stars inabidi kubadilika katika mchezo wa kesho, kwa sababu Chad wanacheza mpira wa nguvu na wanapenda mipira mirefu hali iliyoipa tabu timu yao.

Alisema inabidi timu ya taifa ibadilike na isiige aina ya uchezaji wa Chad ambao ni warefu, wenye nguvu na wanaopenda kucheza mipira mirefu.

“Waliifanya timu ya taifa iige aina yao ya mpira hali iliyowaweka katika wakati mgumu uwanjani,”alisema Marsh.

Marsh alisema kuwa wamefurahishwa na ushindi huo kwani hata hivyo unawaweka katika hatua nzuri ya kuingia katika hatua ya makundi ya kufuzu kwa fainali za kombe.

Mfungaji wa bao la kwanza la Taifa Stars, Mrisho Ngassa alisema kwamba wamefurahishwa na ushindi huo ambao ni muhimu kwao kwani waliupata ugenini.

Ngassa, ambaye muda mrefu hajaifungia timu hiyo bao na amekuwa akianzia benchi katika michezo kadhaa iliyopita, alisema kwamba watajitahidi kucheza kwa bidii ili waibuke na ushindi katika mchezo wa kesho.

“Mechi ilikuwa ngumu lakini tunashukuru tumeshinda, tutajitahidi kushinda mchezo wetu wa Jumanne (kesho),” alisema Ngassa.

1 comment:

  1. kaka Dauda, Mimi huyu kocha wa Taifa stars sijamwelewa kabisa, naomba unisaidie. Kama sikosei wakati taifa stars inaondoka alisema anahitaji sare tu, mungu saidia wakashinda.

    baada ya ushindi anakuja na sera mpya, oo! chad si timu ya kubeza bado kuna ugumu wa ushindi. Inabidi taifa stars ibadilike.

    Manaeno ya Kocha huyu yanaonesha kuwa hajiamini, ni mwoga na inaonekana alishinda kibahati bahati tu. Kwa maaana hiyuo basi huyu kocha hatufai. kauli kama hizo zinavunja moyo wachezaji na kushindwa kujiamini. kwa nini asiige mfumo kama wa Morihno full kuhamasisha hata kama anajuwa watapigwa na Barca. Kocha huyu kwa mtazamo wango anatu-lostisha.

    ReplyDelete