Search This Blog

Friday, October 28, 2011

VITA KUBWA YANUKIA KATI YA T.F.F NA VILABU VYA LIGI KUU


Mgogoro mkubwa unakaribia kuikumba Ligi Kuu ya Tanzania baada ya viongozi wa vilabu kusema hawatoitambua kamati itakayoteuliwa na Rais wa Shirikisho Soka nchini TFF, Leodegar Tenga na kutishia kugomea kushiriki mzunguko wa pili iwapo TFF hawatawalipa fedha zao.

Makamu mwenyekiti wa Simba na Mwenyekiti wa kamati ya kuratibu mchakato wa Kampuni ya Ligi, Geofrey Nyange 'Kaburu' ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah kusisitiza kwamba wao wanatambua kamati ya ligi ikiwa ni utekeleza makubaliano ya mkutano mkuu na si vinginevyo.

Katika kushikilia msimamo huo, Osiah aliweka wazi kuwa Rais Tenga anatarajiwa kuwasilisha majina ya watu ambao amewateua kuunda kamati huru ya kusimamia Ligi Oktoba 27, jana kwenye kikao cha kamati ya utendaji ya TFF.

Lakini jana Kaburu alisema wameshawasilisha barua TFF ya kuwataka kusitisha uteuzi wa kamati hiyo na kwamba kama TFF itaendelea kung'ang'ania kuundwa kwa kamati hiyo klabu kama wadau wakuu wa soka hawataitambua na wanaendelea na mchakato wao wa kuanzisha kampuni.

Kaburu alisema pia wameitadharisha TFF isithubutu kufanya mazungumzo yoyote na mdhamini wa Ligi msimu wa 2012/2013 kwa kuwa ule wa Vodacom unamalizika mwishoni mwa msimu huu, hivyo mikataba yote itasimamiwa na kampuni ambayo itakuwa tayari imeshaanzishwa.

"Klabu nyingi za Ligi Kuu zinaidai TFF fedha nyingi ambazo tayari zilikwishatolewa na wadhamini wa Ligi Kuu na madeni haya yanatokana na utoaji wa hundi hewa na TFF kutumia fedha za klabu kwa matumizi tofauti yaliyodhamiriwa.

"Klabu 13 za Ligi ambavyo ziliudhuria kikao chetu kilichofanyika JB del-monte ukiondoa Kagera Sugar ambayo ilikosa mwakilishi tuliazimia kutocheza mzunguko wa pili wa ligi hii inayoendelea hadi hapo TFF itakapolipa madeni hayo."

"Tumefanya utafiti wa kile kilichoelezwa na rais Tenga kwamba Bundesliga ya Ujerumani inaendeshwa na kamati, kitu ambacho hakina ukweli, Bundesliga ipo katika mfumo wa kampuni," alisema Kaburu.

"Suala la uendeshwaji wa Ligi huru ni maelekezo ya FIFA ambayo yameshatekelezwa na nchi nyingi duniani na mfumo bora wa uendesaji wa ligi yenye tija..."Tanzania suala hili lilishajadiliwa kwenye azimio la Bagamoyo mwaka 2007, lakini cha kusikitisha hadi FIFA wanarudi tena mwaka 2011 kupitia azimio hilo hakuna lolote lililofanyika.

"Viongozi wa klabu tulitarajia mara baada ya kikao chetu cha Aprili mwaka huu na Rais Tenga alitakiwa kuunda kamati mara moja na kuanza kazi kabla ya msimu huu wa ligi kuanza, cha kusikitisha mpaka leo hii kamati haijaundwa na hakuna taarifa rasmi kwa klabu.

Katibu wa TFF, Osiah akijibu madai hayo alisema jana usiku kamati itakaa na kujadili majina ya wajumbe ambao wataunda kamati ya kusimamia ligi.

"Klabu zote za Ligi Kuu ni wajumbe wa mkutano mkuu na tulishakubalia kwenye mkutano mkuu kuwa tuwe na kamati ya mpito itakayokuwa ikisimamia ligi kwa muda wa miaka miwili baada ya hapo kutakuwa na uchaguzi."
Osiah aliongeza kuwa klabu kutishia kugomea kucheza ligi kwa sababu kutolipwa madeni yao na kukataliwa kwa kampuni huko ni kuchanganya ajenda.

No comments:

Post a Comment