Search This Blog

Saturday, September 17, 2011

MATCH PREVIEW: BLACKBURN VS ARSENAL.

Arsenal wanapata nafasi ya pili ya kuwafurahisha mashabiki wao na kujenga ‘confidence’ muhimu kwenye timu yao wikiendi hii wanapokutana na Blackburn Rovers .

Kikosi cha washika bunduki kinaingia kwenye mchezo huu kikiwa kimesheheni kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kuwakosa nyota wake kwa sehemu kubwa ya michezo minne ambayo imeshachezwa hadi sasa .

Gervinho na Alex Song wanarejea baada ya kuwa nje wakitumikia adhabu huku wachezaji wapya waliosajiliwa wakiendelea kuzoea mazingira ya timu yao mpya wakiwa wamekaa na kikosi cha washika bunduki kwa wiki mbili tangu waliposajiliwa.

Kikosi cha Blackburn bado hakijaa vizuri na imani ya wengi ni kuwa watafungwa na Arsenal tena kirahisi.

Mchezo wa kwanza kwa Arsenal kushinda ulikuwa mwishoni mwa wiki iliyopita walipoifunga timu iliyopanda daraja ya Swansea City tena kwa bao ambalo lilikuja kutokana na boko la kipa wa Swansea.

Kuna mengi ambayo yamefanana kwenye viwango vya timu hizi mbili hadi kufikia wiki ya tano ya ligi kuu ya England . Blackburn wameshinda mchezo mmoja kati ya michezo tisa iliyopita na Arsenal wana rekodi kama hiyo tofauti ikiwa kwenye ukweli kuwa kwao ni rekodi ya michezo ya ugenini na kwa Rovers ni michezo yote.

Kocha wa Blackburn Steve Kean bado ana wakati mgumu sana kwenye kipindi chake kama kocha.

Wakati akiandaa timu ya kucheza na Arsenal, mitaani kuna mashabiki wanaanda maandamano ya kuwashinikiza wamiliki wa timu hii wamfukuze kazi kwa kushindwa kuipa mafanikio timu yao.

Tatizo kubwa linalotazamwa na wataalamu kwa Blackburn ni kwa kocha Steve Kean kuwa na uzoefumdogo.

Kumbuka Steve Kean alikuwa kocha msaidizi kwa Sam Allardyce na alipofukuzwa bosi wake ndipo alipopewa jukumu la kuwa kocha mkuu .

Tayari baadhi ya wachezaji tegemeo wa Blackburn walieleza kukerwa na uamuzi wa kumuondoa kocha Sam Allardyce na mfano mzuri alikuwa nahodha Christopher Samba .

Hapo moja kwa moja utagundua kinachoisibu Blackburn na ndio maana wanaingia kwenye mchezo dhidi ya Arsenal wakiwa kwenye hali mbaya ambayo huenda ikaendelea kwenye mchezo huu.

Kwa jinsi ambavyo michezo yao miwili ya mwisho ilivyoenda unaweza kusema kuwa Rovers hawana bahati .

Wiki iliyopita walicheza na Fulham wakatoka sare 1-1 na kabla ya hapo walicheza katika mchezo ambao wangeweza kuchukua pointi zote tatu kwani walikosa penati mbili na bao lililowaua lilikuwa kwenye dakika ya mwisho ya mchezo lilikuwa bao la penati pia ambayo iliwekwa wavuni na Mikael Arteta mtu ambaye watakutana naye kesho akiwa na timu nyingine .

Bahati mbaya ya Blackburn ina kila dalili za kuendelea unapotazama orodha ya wachezaji watakaokosa mchezo wao dhidi ya Arsenal.

David Hoilett,David Dunn,Morten Gamst Pedersen na Ryan Nelsen wote wataukosa mchezo huu huku beki na nahodha Christopher Samba akiwa na shaka japo kuna uwezekano mkubwa wa kumuona .

Bado mshambuliaji mpya Mauro Formica hajapata muda wa kutosha kuzoeana na wenzie na ndio maana hadi sasa bado ameonekana kupata wakati mgumu kwenye timu yake mpya.

Tegemeo pekee walilo nalo Rovers ni kwa beki mpya Scott Dann aliyesajiliwa toka Birmingham City ambaye anatrajiwa kucheza pembeni ya Christopher Samba .

Katikati ya uwanja Steve Nzonzi atakuwa muhimu sana kwa jinsi anavyoweza kuunganisha sehemu mbili za beki na safu ya viungi wa mbele na washambuliaji na atakuwa msaada mkubwa kwa Mauro Formica ambaye atacheza shimoni.

Rubben Rochina pamoja na Goodwillie watakuwa mbele kusaidiana na Nzonzi na Formica kujaribu kuivuka ngome itakayokuwa chini ya mjerumani Per Mertersecker.

Mashabiki wa Arsenal kwa vyovyote watakuwa na mawazo kuwa timu yao imevuka kipindi cha mpito na matatizo yake yameisha lakini ukweli ulioonyeshwa na mchezo wa wiki iliyopita dhidi ya Swansea ambapo Arsenal walishinda kwa bao la ‘kidizaini’ kama wasemavyo vijana wa mtaani ni kwamba bado hali sio nzuri kama ambavyo wangependa iwe.

Kikosi cha Arsenal kitawakosa Thomas Vermaelen ambaye amerudi kwenye meza ya wagonjwa na kiungo Abou Diaby pamoja Jack Wilshere bado wataendelea kuwa nje .

Nafasi zao zitachukuliwa na watu wale wale ambao wamekuwa wakijaza mashimo yaliyopo kina Thomas Rosicky na Aron Ramsay endapo atakuwa amepona haraka kama inavyotaarifiwa kuwa .

Viungo Gervinho na Alex Song watarudi kuungana na kinda Emanuel Frimpong ambaye ametokea kuwa tegemeo kwa Arsenal lakini faida iliyopo ni kwamba wachezaji wapo na washika bunduki hawatalazimika kutumia vijana kama walioonekana kwenye kipigo cha bao nane toka kwa Man United.

Mikael Arteta atakuwa kwenye sehemu ya kiungo kuendeleza kazi iliyomleta Emirates ya kujaza nafasi ya Cesc Fabregas na pia inaweza kuwa nafasi ya wachezaji wapya kina Yossi Benayoun na Andre Santos na hata mshambuliaji Park Chu Young kuonyesha uwezo wao.

Timu hizi zote mbili kwa pamoja zinaweza kusema kuwa huu ndio mwanzo mbaya wa msimu kuliko misimu yote katika historia zao ambapo Rovers wanashika mkia wakiwa na pointi moja tu waliyoipata wiki iliyopita mikononi wa Fulham na Arsenal wako kwenye nafasi ya 12.

Katika michezo minne iliyopita Blackburn wameruhusu wavu wao kutikiswa mara 7 na Arsenal wameruhusu wavu wao kutikiswa mara nyingi zaidi .

Blackburn wana rekodi mbaya sana katika michezo yao dhidi ya Arsenal na wamefungwa michezo 21 huku wakishinda mechi 17 kati ya mechi 53 ambazo zimechezwa kwenye uwanja wao.

Arsenal wao wamefungwa na Blackburn mara moja katika michezo 10 iliyopita na Arsenal wameshinda mara saba mfululizo huku wakifunga mabao 212 katika michezo yote waliyocheza kwenye historia ya ligi ya England huku Blackburn wao wakifunga mara 145.

Endapo Arsenal itafungwa katika mchezo huu itakuwa mara yao ya 100 kupoteza mchezo kwenye ligi kuu ya England .

Hadi sasa hakuna mchezaji yoyote wa Arsenal ambaye amefunga zaidi ya bao moja na pia hakuna mchezaji ambaye ametoa pasi ya bao zaidi ya moja .

No comments:

Post a Comment