Wakati Ligi Daraja la Kwanza imepangwa kuanza Oktoba 15 mwaka huu, klabu saba kati ya 18 bado hazijalipa ada ili timu zao ziweze kushiriki katika ligi hiyo iliyogawanywa katika makundi matatu. Klabu ambazo hazijalipa ada ya kushiriki ya sh. 200,000 ni AFC ya Arusha, Majimaji ya Ruvuma, Polisi ya Iringa, Polisi ya Tabora, Rhino Rangers ya Tabora, Small Kids ya Rukwa na Transit Camp ya Dar es Salaam. Mwisho wa kuwasilisha usajili wa wachezaji na kulipa ada ya ushiriki ni Oktoba Mosi mwaka huu. Klabu ya Burkina Faso ya Morogoro imelipa nusu ya ada ya ushiriki ambapo imetakiwa kumaliza kiasi kilichobaki ifikapo Oktoba Mosi mwaka huu. Vilevile kuna klabu tatu ambazo bado hazijawasilisha usajili wa wachezaji wa timu zao kwa ajili ya ligi hiyo. Klabu hizo ni AFC ya Arusha, Morani ya Manyara na Temeke United ya Dar es Salaam. Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itakutana Oktoba 2 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine itaidhinisha timu zilizokidhi kanuni za kucheza ligi hiyo ili Kurugenzi ya Mashindano ya TFF ipange ratiba ya ligi hiyo. Timu 18 za Ligi Daraja la Kwanza ni Burkina Faso, Mgambo Shooting ya Tanga, Morani, Polisi ya Dar es Salaam, Temeke United na Transit Camp ambazo ziko kundi A. Kundi B lina timu za Majimaji, Mbeya City Council, Mlale JKT ya Ruvuma, Polisi ya Iringa, Small Kids na Tanzania Prisons ya Mbeya. Kundi C lina timu za AFC, Polisi ya Morogoro, Polisi ya Tabora, Rhino Rangers na Samaria ya Singida.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
No comments:
Post a Comment