Search This Blog

Thursday, August 4, 2011

Roberto Baggio: Na.10 bora kutokea Italia

HII ILIKUWA NI BAADA YA KUPAISHA PENALTI KWENYE MCHEZO WA FAINALI YA KOMBE LA DUNIA 1994 DHIDI YA BRAZIL.

KWA watu wengi, anaonekana kuwa mtu wa ajabu kwa jinsi alivyoishika dini yake ya Budha, katika taifa la Kikatoliki, lakini kwa Wataliano, huwaambii kitu kwa shujaa wao huyu wa kombe la Dunia.

Roberto Baggio, alikuwa mtu tofauti; siyo tuu mchezaji aliyejaaliwa kipaji cha hali ya juu, lakini pia mtu wa mikasa. Maisha yake kama mwanasoka yalikuwa ya kushangaza sana.

Tunamzungumzia mchezaji ambaye uhamisho wake toka klabu moja kwenda nyingine ulikuwa ukigubikwa na migomo na vurugu toka kwa mashabiki wake waliokuwa hawaambiwi kitu juu ya mwanandinga huyo aliyependa sana wanyama.

Alikuwa hatulii kwenye timu moja, lakini ukizungumzia maisha yake ya kiimani, alikuwa na msimamo usiobadilika. Alijiunga na imani yake ya Kibudha tokea akiwa na miaka 15.

Kati ya mwaka 1982 na 2004, Baggio alifunga mabao 317 katika michezo 697, mengine akifunga toka katikati ya kiwanja kama alivyowafanya Czechoslovakia kwenye fainali za kombe la Dunia za mwaka 1990 ambayo yanabaki kuwa alama ya matukio ya kuvutia kati ya mchezo wa mpira wa miguu duniani.

Lakini mikasa yake ya kuvutia haikuwa kwenye mafanikio pekee, bali hata katika maanguko, kama pale alipokosa penati wakati wa mchezo wa fainali dhidi ya Brazil mwaka 1994. Historia inatuambia kwamba ilikuwa ni penati ile iliyoikosesha Italia kikombe, ingawa Franco Baresi na Daniele Massaro walipoteza mikwaju yao hapo awali.

Taswira ya Baggio akiwa ameweka mikono yake kiunoni na kichwa chini, wakati huohuo akionekana mlinda mlango wa Brazil, Claudio Tafarel akiwa amepiga magoti akinyoosha mikono juu kumshukuru Mungu; ni mojawapo ya taswira za kukumbukwa katika historia ya soka.

Taswira hii inaonyesha tofauti kati ya mafanikio na kushindwa, ushindi na kukata tama. Hii ni taswira ambayo Baggio ametumia maisha yake yote akijaribu kuifuta.

Lakini katika wakati huo wa upweke na mazingira magumu, baada ya mashindano ambayo twaweza kusema kuwa Baggio alitoa mchango mkubwa sana kuwafikisha fainali, kuna mengi ambayo yalikuwa yanavutia kuhusu Baggio.

Uchezaji wake mahiri, usiohitaji kutumia nguvu kama wachezaji wengi kipindi hicho, ndio uliokuwa ukiwavutia watu kwake. Alikuwa na uwezo wa kuwachezea mabeki wa timu pinzani kwa jinsi anavyotaka yeye. Hata ilifikia kipindi kuna waandishi wa vitabu nchini Italia walitunga vitabu vinavyoelezea nywele za Baggio kuwa ni “nywele zenye utukufu”.

Katika miaka yake 22 ya kisoka, Baggio alichezea timu ya taifa ya Italia mara 56 akipachika mabao nyavuni katika fainali tatu mfululizo za kombe la Dunia. Aliwahi kuchezea vilabu saba: Vicenza, Fiorentina, Juventus, AC Milan, Bologna, Inter Milan na Brescia.

Alifanikiwa kubeba vikombe viwili vya ubingwa wa ligi ya Italia, kombe moja la UEFA na kombe moja la ligi nchini Italia. Kuna wachezaji wengi wa Kiitaliano wenye CV kali kupita hii, lakini wako wachache waliopendwa kama Baggio.

Muulize Muitaliano yoyote kuchagua mchezaji wa Kiitaliano mwenye kipaji kuliko wote na wengi watakwambia kuwa ni Baggio. Wazee wa zamani wachache watamchagua kiungo wa zamani wa Kiitaliano aliyecheza soka huko miaka ya sitini aitwaye Gianni Rivera. Wale waliokula chumvi zaidi watakwambia Giuseppe Meazza mtaalamu wa miaka ya 30 an 40 huko. Lakini kuna mwandishi mmoja wa soka ambaye alipata bahati ya kuwaona wachezaji wote hawa watatu wakisakata kabumbu na yeye alikubali kuwa Baggio yuko mstari mmoja na kina Rivera na Meazza.


Katika misimu yake mitano akichezea Juventus, kuanzia mwaka 1990 hadi 95, Baggio alikuwa akifananishwa na Michel Platini kila mara. Ingawa ufananisho huu haukukubalika na Platini mwenyewe. Baggio naye alikuwa akivaa jezi namba kumi mgongoni kama Platini na mastaa wengine wa soka.

Lakini cha kufurahisha, Platini alinukuliwa akisema, Baggio si namba kumi halisi bali ni namba tisa na nusu. Platini anasema hakutamka hivyo kumkashifu Baggio bali alikuwa akijaribu kuelezea staili ya uchezaji wa Baggio ambayo alikuwa akicheza kama namba tisa lakini mwenye uwezo wa kutafuta kumiliki mpira kitu ambacho alikuwa sahihi.

Katika historia yake ya maisha, Baggio alitamka kuwa anajiweka katika orodha moja na Pele na Maradona, lakini akisisitiza kuwa Pele na Maradona wako katika dunia nyingine, ila yeye yuko katika mstari unaowafuatia.

Na hii ilithibitishwa mnamo mwaka 2000 wakati FIFA walipoendesha zoezi la mtandaoni la kupata maoni kuhusu nani mchezaji bora wa karne ya 20; Baggio alikamata nafasi ya nne nyuma ya Maradona, Pele na Eusebio.

Mwaka 1993 wakati akichezea Juventus, Baggio alifanikiwa kuwa mchezaji wa Kiitaliano wa tatu, baada ya Rivera na Paolo Rossi, kupata tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya; na baada ya hapo Waitaliano ilibidi wasubiri miaka 13 baadae ndipo Muitaliano mwingine aitwaye Fabio Cannavaro, alipochukua tuzo hiyo baada ya kuiongoza timu yake kubeba kombe la Dunia mwaka 2006.

Ila kitu kinachowauma wapenzi wa mchezaji huyu zaidi, ni kuwa hawakuweza kujua fika kiwango cha juu zaidi anachoweza kufikia jamaa huyu, kwani alikuwa akipata majeraha mara kwa mara. Unaweza kusema kuwa maisha ya kisoka ya Baggio yaliisha kabla hata hayajaanza.

Wakati Fiorentina walipomnasa mwaka 1985 tayari alikuwa akichukuliwa na wengi kama nyota wa miaka ya mbele. Vilabu vya Italia vilikuwa vikimvizia toka akiwa na miaka 11 akichezea timu ya kijijini kwao katika mji wa Vicenza.

Akiwa na miaka 13 alijiunga na klabu ya Vicenza katika ligi ya vijana ambapo alifanikiwa kufumania nyavu mara 110 katika mechi 120. Baada ya hapo alihamia timu ya wakubwa, lakini hata kabla hajakaa vizuri, Fiorentina waliwapiku Juventus, kupata saini ya kijana huyu baada ya kumwaga dau lililokuwa na thamani ya paundi milioni 1.5.

Hata hivyo, siku mbili tu kabla mkataba haujasainiwa, Baggio alichanika msuli katika mguu wake wa kulia akiwa katika mechi dhidi ya Rimini, maumivu ambayo yalilazimu madaktari kumfuma na nyuzi 220 ili aweze kupona.

Kwa bahati nzuri, Fiorentina waliheshimu mkataba na kumsajili akiwa majeruhi, hali ambayo ilimuweka nje kwa takriban kipindi cha misimu miwili; na hata baada ya hapo aliendelea kupata maumivu ya goti mara kwa mara.


Baggio alitambulishwa katika dini ya Kibudha na rafiki yake wa Kiitaliano Mbudha aitwaye Maurizio Boldrini. Katika dini hii ndipo Baggio alipofanikiwa kupata maana ya mateso ambayo alikuwa akiyapata.

Baada ya kupona, Baggio alikjikita katika timu ya Fiorentina kama mmojawapo wa wachezaji bora katika timu hiyo haswa katika msimu wa mwaka 1987 -88 ambapo alicheza mechi 27 akifunga mabao 6. Katika msimu uliofuata alifanikiwa kufumania nyavu mara 15 katika michezo 30 aliyocheza. Kilichokuwa kikiwagusa watu wengi ni kuwa si idadi ya mabao tu bali ubora wa mabao aliyokuwa akifunga.

Mnamo mwezi wa tano mwaka 1990, Fiorentina walimuuza Baggio kwa mahasimu wao wa jadi Juventus. Habari za kuuzwa kwa Baggio zilipotoka, mashabiki walianzisha vurugu na balaa mji mzima wakivunja vioo, maduka na magari. Ilichukua idadi ya askari wa kutuliza ghasia 350 kuwatuliza mashabiki hawa waliokuwa na hasira.
Baggio alicheza chini ya makocha 18 tofauti katika maisha yake ya kisoka. Hadi leo hii jamaa huyu ana maneno mazuri ya kuzumgumza juu ya makocha hawa wakiwemo kina Carlo Mazzone (Brescia), Gigi Maifredi (Juventus) na Sven Goran Erricson (Fiorentina).

Lakini katika makocha wote, Baggio hatokuja kumsahau Marcelo Lippi, kwani huyu alikuja kuwa kocha aliyemchukia kuliko wote. Akiwa katika msimu wake wa pili katika timu ya Inter Milan Baggio anaelezea kuwa Lippi alikuwa akijaribu kila aliloweza kummaliza mwanasoka huyu sababu ya kupendwa kwake na mashabiki tofauti na Lippi ambaye hakuwa kipenzi cha mashabiki nchini Italia.

Baggio anakumbuka siku moja akiwa mazoezini na timu ya Inter alicheza pasi moja ndefu iliyomkuta Bobo Vieri, ambaye aliutia mpira kimiani. Baada ya hapo kila mchezaji alimpongeza kwa kupiga makofi akiwemo Cristian Panucci. Lakini Lippi alipandisha mashetani na kuwafokea Pannucci na Vieri huku akiwaambia kwa lugha ya Kiitaliano, “Nyie washenzi mnafanya nini? Hapa hatuko maonyeshoni, hapa tuko kufanya kazi!”
Ndio maana hakuna aliyeshangaa wakati Lippi alipokuja kufukuzwa kazi miezi kadha baadae.

Baggio alistaafu kucheza soka katika msimu wa 2003 -2004 na kwa asilimia kubwa akapotea kabisa katika rada ya soka. Siku hizi hutoa ‘intavyuu’ kwa waandishi mara chache sana na huonekana mitaani kwa nadra.

Siku hizi, Baggio hutumia muda wake mwingi akiwinda katika ranchi yake nchini Ajentina na kusafiri nchi moja hadi nyingine ‘akipromoti’ masuala ya kibinadamu huku akiwa mfuasi thabiti wa dini yake ya Kibudha. Anatumia muda wake mwingi zaidi kusaidia kupigana na umasikini duniani akiwa kama balozi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa, (FAO).

Nywele zake ndefu nyeusi zimeshabadilika rangi na kuwa na mvi nyeupe. Anaonekana mzee zaidi kuliko miaka 41 aliyonayo hivi sasa; na soka pekee analocheza ni akiwa na watoto wake nyumbani.

No comments:

Post a Comment