Search This Blog

Friday, August 12, 2011

PAZIA LA LIGI KUU YA ENGLAND LAFUNGULIWA RASMI

Msimu mpya wa ligi kuu ya England umebakiza masaa pungufu ya 89 kabla ya kurudi tena baada ya kumalizika kwa msimu uliopita . Mashabiki kwa muda wamekuwa wakipata burudani ya soka kwa kufuatilia mechi za “pre-season” ambazo kwa baadhi ya mashabiki zimewapa sababu ya kutabasamu na kuna baadhi zimewapa wasiwasi kwa kile walichoshuhudia .
Kwa kurejesha kumbukumbu mara ya mwisho Manchester United ndio waliomaliza kama mabingwa wakiweka historia ya kutwaa ubingwa wa 19 ambao hatimaye uliwazidi mahasimu wao wa muda mrefu Liverpool .



Kwa bahati mbaya kwa mashabiki wa Manchester United huwezi kuzungumzia taji la 19 la ligi bila kurejea “dhahma” ya Wembley. Huku wengi wakiamini kuwa United watafuta makosa ya mwaka 2009 na kuwafunga mabingwa wa Hispania ambao wengi wanawatazama kama timu inayocheza soka bora kuliko timu zote kwenye historia ya mchezo huu , Manchester United walikumbana na kipigo cha mabao 3-1 na kumaliza msimu wao kwa machungu yasiyosahaulika.


Kwa wale wanaotazama mchezo wa soka kwa jicho la tatu , la nne mpaka la tano walitambua moja kwa moja kuwa kipigo ilichokipata United pale Wembley lazima kingekuwa na athari Fulani kwenye kikosi cha United kwa msimu uliofuata( yaani huu unaoanza kesho ).
Na ndiyo kilichotokea Sir Alex Fergusson hakupoteza muda kwenye shughuli ya usajili huku akili yake ikiwa kwenye kulipa kisasi kwa Barcelona kwa jinsi “walivyomtetemesha” pale Wembley .United walianza kwa kumsajili kipa ambaye ndiye atakayekuwa mrithi wa Edwin Van Der Sar ,


walimnasa Mhispania David De Gea toka Atletico Madrid , baada ya hapo United walikamilisha Usajili wa beki chipukizi Phil Jones halafu wakamaliza na Ashley Young . Baada ya hapo United wakaanza kupunguza idadi ya wachezaji ambapo John O’shea , Wesley Brown na Gabriel Obertan waliuzwa kwa Sunderland na Newcastle United .


United bado wanaonekana kuwa kwenye soko la usajili baada ya kauli ya mkurugenzi mtendaji David Gill kusema kuwa bado kuna nafasi moja ya kujaza . Nafasi hii ni nafasi ambayo imekuwa gumzo kwa karibu wakati wote wa mapumziko ya kabla ya msimu kuanza .


Kama utakuwa umetazama kwa makini De Gea , Ashley Young na Phil Jones wamekuja kuziba mapengo ya kina Van Der Saar, Gary Neville na Ryan Giggs atakayestaafu mwishoni kwa msimu ujao .


Lakini bado kuna nafasi ya Paul Scholes ambayo bado iko wazi . Hapo linakuja jina la Wesley Sneijder mtu ambaye amekuwa akihusishwa na kurithi nafasi ya Scholes hasa baada ya tetesi za kuwasajili kina Luka Modric na Samir Nasri kuisha kimya kimya.Msimu huu utakuwa wa maadiliko makubwa kwa United ambayo inakuja na sura mpya ikiwa na vijana wengi huku wakongwe wakiwa wameendelea kupungua taratibu .


Kwa upande mwingine Chelsea timu iliyomaliza msimu ikiwa nafasi ya pili ilimaliza kwa kumfukuza kocha wake Carlo Ancelotti na wakati timu zingine zikifanya usajili Chelsea “walisajili” kocha Andre Villas Boas”, kocha ambaye ametokea kuliteka soka la ulaya akiwa na kikosi chake cha Fc Porto .

Andre Villas Boas alianza wakati wake akiwa na Chelsea kwa habari mbaya za kumkosa kiungo muhimu wa Chelsea Michael Essien ambaye alipata jeraha baya la goti ambalo litamuweka nje ya dimba kwa zaidi ya miezi sita . Villas Boas alijibu pigo hilo kwa kumsajili kinda wa Barcelona Ariel Romeu .

Baada ya hapo Chelsea imemsajili Romelu Lukaku , mshambuliaji mwenye umri wa miaka 18 toka Anderletch ya Ubelgiji . Lukaku anatajwa kama Didier Drogba mpya . Inavyoonekana kuna kila dalili kuwa Chelsea bado hawajamaliza usajili kwani kuna jina la Luka Modric ambalo limekuwa likihusishwa na jezi za bluu za London kwa muda mrefu .

Andre Villas Boas ana kazi kubwa sana ya kufanya kwenye kikosi chake ch Chelsea . Hakuna nayejua kwanini amemsajili Romelu Lukaku ilhali anao watu kama Drogba , Anelka, Torres na Daniel Sturidge .

Sawa unaweza kusema kuwa kwa umri wa miaka 33 alio nao Drogba na mwenzie Anelka Villas Boas anatazama mbali zaidi ya walipo washmabuliaji hawa wawili lakini vipi kuhusu Sturidge mtu ambaye alidhihirisha uwezo wake kwa mabao aliyofunga akiwa na Bolton alikokuwa kwa mkopo msimu uliopita .

Una maana gani kwa kijana huyu unaposajili mshambuliaji mwenye umri sawa na wake (sturidge) yaani Lukaku tena kwa fedha nyingi namna hii . Suala linguine muhimu ambalo litakuwa tatizo kwa sasa kwa Boas ni mbinu ya kuwachezesha Drogba na Torres kwenye uwanja mmoja .

Tatizo kubwa la Chelsea halijawahi kuwa kocha , bali mmiliki wa timu Roman Abramovich ambaye hajawahi kuwapa makocha muda wanaohitaji kujenga timu na kama hataiacha tabia ya kuwaajiri na kuwafukuza basi ni dhahiri mafanikio atakuwa akiyasikia kwa timu zingine .




Washindi wa tatu kwenye msimu uliopita walikuwa Manchester City . Kuna vitu ambavyo timu hii inayomilikiwa na mabilionea wa kiarabu inacho kama Baraka na wakati huo kama laana .


Vitu hivyo ni mshambuliaji toka Argentina Carlos Tevez na mwenzie toka Italia Mario Balotelli. Baloteli na Tevez kwa vipaji walivyo navyo ni kama baraka kwa timu yoyote itakayokuwa nao lakini ni laana pia kwani kwa nyakati tofauti wamekivuruga mno kichwa cha kocha wao Roberto Mancini .


Tevez ameonyesha dhamira yake kuwa hataki kuendelea kucheza soka kwenye klabu hii na Mario Balotelli mara kwa mara amekuwa akiudhihirishia ulimwengu kuwa yeye ni mwendawazimu kwa matendo yake anyoyafanya ndani na nje ya uwanja . Kwa tatizo la Tevez kocha Roberto Mancini ameonyesha kulipatia ufumbuzi kwa kumsajili mwenzie na Tevez kwenye timu ya taifa ya Argentina Sergio Aguerro . Kabla ya hapo Mancini alimsajili mchezaji Stefan Savic aje kusaidiana na mabeki wengine na pia amemsajili Gael Clichy toka Arsenal na kuna kila ishara kuwa anaweza kurejea Emirates kumnyakua mchezaji mwingine Samir Nasri.


Manchester City wanauanza msimu huu kama walivyouanza ule uliopita kwa kuonyesha kuwa wanakuja kuleta mapinduzi na tayari wameyaleta kwani leo hii haizungumzi kama top 4 bali top 5 au top 6 ukiwajumuisha na Tottenham , lakini bado safari ndefu ya kutwaa mataji ipo kwa kuwa Kocha Roberto Mancini bado hajapata “chemistry” muhimu ambayo itampa mataji .


Alicho nacho kwa sasa ni kundi kubwa la wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu lakini wachezaji hawa wanabaki na vipaji vyao na kwa pamoja hawana uhusiano muhimu ambao unaunda umoja unaoleta timu inayoweza kucheza kwa mafanikio uwanjani .




Arsenal ambao kwa miaka ya hivi karibuni wametokea kuwa Academy ya Manchester City wana matatizo makubwa . Imepita misimu sita tangu washika bunduki watwae kombe lao la mwisho . Sababu zinazoinyima Arsenal makombe ni zile zile , kipa , beki na kiungo .


Hakuna anayejua kinachoendelea kichwani mwa Arsene wenger zaidi yake yeye mwenyewe . Hadi sasa hajafanya usajili wa kuzingatia matatizo yanayoinyima Arsenal mafanikio na badala yake amemsajili kiungo mshambuliaji Gervinho toka Lille ya Ufaransa .


Labda amekuwa mzito kusajili beki kwa kuwa anajua kuna beki mmoja ambaye kurejea kwake ni kama mchezaji mpya aliyesajiliwa naye ni Thomas Vermalen . Zaidi ya hapo Arsene Wenger ametumia msimu wa usajili akijibu na kuondosha tetesi za kuondoka kwa Cesc Fabfergas na Samir Nasri .


Fabregas ni mtu ambaye ulimwengu mzima unatambua kuwa ana ndoto ya kurudi kwao Bracelona ambako anatazamwa kama mrithi wa Xavi Hernandez . Nasri ameshasema kuwa anataka kwenda kwingine ambako atapata mataji .


Tetesi za hivi karibuni zimekuwa zikimhusisha Arsene Wenger na majina ya watu kama Gary Cahill na Christopher Samba watu ambao kiukweli Arsenal inawahitaji ili kutibu ugonjwa wa muda mrefu lakini hadi sasa dalili zinaonyesha kuwa wameshawakosa na Arsene wenger amegeukia kwa Scott Dann wa Birmingham ambaye inasemekna mazungumzo yanaendela .


Hadi hapo ambapo Arsene Wenger atakapogundua kuwa kina Johan Djorou , Abou Diaby na vijana wengine wepesi wepesi ambao hawaiwezi mikikimikiki ya soka la England basi Arsenal wataendela kuwaumiza mashabiki wao kwa muda mrefu.




Mabingwa wa zamani Liverpool wameonekana kumaanisha biashara safari hii . Ukirudi nyuma wakati dirisha dogo la usajili lilipofunguliwa msimu uliopita King Kenny Dalglish alifanya usajili wa kumuuza Fernando Torres na kuwanunua Luis Suarez na Andy Caroll .


Kennya hajaishia hapo na wakati huu amenza kazi kwa kuwasajili Jordan Henderson , Charlie Adam, Stewart Downing , Alexander Doni , na pia wako mbioni kumnasa beki wa kushoto wa kihispania toka Newcastle United Jose Enrique . Kimsingi Liverpool wamekuja kurejesha zama zao za ufalme wa England ambao umepotea kwa muda mrefu na chini ya King Keny Daliglish kuna kila sababu na uwezo wa kutimiza azma hiyo .

No comments:

Post a Comment