Magomamoto (kushoto ) akiwa na Maximo na mheshimiwa Mohamed Dewji.
NAIPENDA Simba toka moyoni kwangu, wala si kwa sababu mtu fulani anaipenda timu hii nami kumuiga”
Zamani alikuwapo shabiki mmoja wa soka wa timu ya Reli ya Morogoro, huyu si mwingine bali ni Yamungu. Unapofika uwanjani siku ya mchezo wa timu yake na nyingine, bila shaka utapata burudani zaidi ya mpira wa miguu.
Yamungu alikuwa na aina za ushangiliaji wake ikiwemo kujichora, kunyoa na hata kuvaa ili mradi kuwahamasisha wachezaji wa timu yake waweze kujituma ili kupata ushindi.
Katika klabu ya Simba yupo shabiki anayefanya vitu vya ziada jukwaani ili kuwahamasisha wachezaji wa timu hiyo kuweza kupata ushindi.
Huyu si mwingine bali ni Togolan Salum, lakini anafahamika zaidi kwa jina la Magomamoto, ndiyo ana vitu vya ziada uwanjani hasa kwa ushangiliaji wake wa ghafla awapo jukwaani.
Aliitwa jina la Magomamoto kutokana na bar (baa) aliyokuwa akiimiliki katika mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam iliyokuwa ikiitwa Magomamoto Bar, hiyo ilikuwa mwanzoni mwa miaka ya 1980.
Utakapofika katika jukwaa jekundu sehemu ya watu mashuhuri (VIP) kabla ya mchezo wowote wa Simba kuanza, utamkuta Magomamoto (61) akiwa amekaa kimya huku mwilini mwake akiwa amevaa nguo zenye rangi nyekundu na nyeupe.
Mpira unaanza, bado yupo kimya lakini ghafla Simba inakosa bao la kufunga lililoonekana kuwa la wazi, hapo ndipo utakapomfahamu Magomamoto, moja kwa moja atatoa ishara kwa kikundi cha uhamasishaji cha Simba kiitwacho Muchacho Group (Kidedea).
Atachukua filimbi yake nyekundu na kuanza kuipiga kufuatisha midundo ya Kidedea na kuanza kucheza huku akiimbiwa nyimbo za kuwaamasisha wachezaji, ghafla watazamaji kama 100 wa sehemu ya karibu wanaacha kufuatilia mchezo na kumtazama Magomamoto.
Alipozungumza na number ten kuhusu upenzi na uhamasishaji wake kwa timu ya Simba, Magomamoto anasema kuwa tofauti na wapenzi na mashabiki wengine wa timu hiyo kubwa hapa nchini, yeye hakulazimishwa kuipenda klabu hiyo.
“Ilitokea tu mimi kuipenda Simba katika miaka ya 1970, na moja kwa moja nikawa bega kwa bega kuhakikisha timu inafanya vizuri siku zote,” anasema Magomamoto.
SIMBA ILIMFILISI:
“Nakumbuka mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Al Hilal ya Sudan uliochezwa Mwanza uliweza kunitia hasara ya katika biashara yangu ya baa (bar) baada ya kuipa fedha ya zawadi timu yangu na kundi la uhamasishaji.
Ilikuwa mwishoni mwa miaka ya 1980 ambapo kwa mapenzi yangu nilitoa Sh. Milioni 2 kuizawadia timu baada ya ushindi wa bao 1-0, mara baada ya kutoa fedha hizo biashara yangu ikayumba na kufilisika,” anasema Magomamoto.
Anasema pamoja na kuonekana kama ‘alikosea’ mwenyewe aliona kama jambo la fahari kuizawadia timu anayoipenda toka moyoni.
MAGOMAMOTO KUMBE KIDEDEA ‘ORIJINO’
Kama nilivyoeleza hapo awali, kuna wakati Magomamoto hupigiwa ngoma na kundi la Kidedea kisha hucheza kwa mtindo wa aina yake, Naye ni mmoja kati ya wasanii wa kundi hilo.
“Ninazo sare maalum za Kidedea, mimi ni mmoja wao lakini huwa sijichanganyi nao uwanjani kutokana na mambo mbalimbali,” anasema Magomamoto.
MAGOMAMOTO NDANI YA NGUO ZA YANGA:
Ni jambo la aghalabu kutokea kwa mchezaji, shabiki au kiongozi wa Simba kuvaa nguo za kijani na njano zinazotumiwa na watani zao Yanga, lakini Magomamoto alivunja mwiko huo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Etoile d’Or Mirontsy uliochezwa Januari 31 mwaka huu katika uwanja wa Uhuru.
“Nilivaa nguo za kijanina njano kwa sababu Yanga ilikuwa ikiwakilisha nchi, hapa utafa ulitangulia lakini sina uhusiano wowote na watani zetu hawa wa jadi., ni linalotokea kwa nadra sana.
Kama utakumbuka katika fainali ya kombe la CAF mwaka 1994 kati ya Simba na Stella Abidjan, tuliwavalisha Yanga khanga za timu yetu, lakini baada ya kufungwa wakaanza kutuimba wakisema uzalendo umewashinda, ” anasema Magomamoto.
SOKA LA BONGO:
“Wachezaji wengi wa sasa hawajitumi ipasavyo uwanjani, anachofahamu ni fedha pekee tofauti zamani ambapo mapenzi binfasi kwa timu yalileta soka safi,” anasema Magomamoto.
ALIVYO:
Alizaliwa mwaka 1949 na kusoma katika shule ya msingi Kwamshita huko Same huko Kilimanjaro, hapo aliweza kucheza soka lakini si la ushindani.

No comments:
Post a Comment