Search This Blog

Wednesday, July 13, 2011

MICHEZO YA AFRIKA (ALL AFRICA GAMES)


Timu ya Taifa ya wanawake ya mpira wa miguu (Twiga Stars) imepangwa kundi B katika Michezo ya Afrika (All Africa Games). Michezo hiyo ya Kumi itafanyika kuanzia Septemba 3-18 mwaka huu jijini Maputo, Msumbiji.

Upangaji makundi kwa ajili ya michezo hiyo kwa upande wa wanawake na wanaume ulifanywa jana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Hicham El Amran.

Rais wa CAF, Issa Hayatou pia alishuhudia upangaji huo wa makundi uliofanyika makao makuu ya shirikisho hilo jijini Cairo, Misri wakiwemo pia wawakilishi wa timu zilizofuzu kwa ajili ya michezo hiyo.

Twiga Stars imepangwa pamoja na timu za Afrika Kusini, Zimbabwe na Ghana. Kundi A lina wenyeji Msumbiji, Cameroon, Algeria na Guinea. Mabingwa wa mwaka 2007 Nigeria wameshindwa kufuzu kwa ajili ya michuano ya mwaka huu.

Wiki iliyopita Twiga Stars ilikuwa Harare, Zimbabwe kwenye mashindano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA). Ilishika nafasi ya tatu ambapo ilicheza na Zimbabwe na Afrika Kusini. Zimbabwe ‘Mighty Warriors’ ndiyo walioibuka mabingwa wakati Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ ilikuwa makamu bingwa.

Twiga Stars inayofundishwa na Charles Mkwasa akisaidiwa na Nasra Mohamed inatarajia kuingia kambini mwezi mmoja kabla ya kuanza michuano hiyo inayoshirikisha timu nane.

Kwa upande wa wanaume kundi A lina wenyeji Msumbiji, Afrika Kusini, Libya na Madagascar wakati kundi B ni Cameroon, Uganda, Ghana na Senegal.

No comments:

Post a Comment