Search This Blog

Sunday, July 10, 2011

COUNTDOWN KAGAME CASTLE CUP FINAL: SIMBA vs YANGA.


MASHABIKI wa soka nchini hawakuwa na imani kabisa na timu zao, Simba na Yanga kama zinaweza kufika hata Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Castle, kutokana na sababu tatu kubwa, ambazo ni; kukurupushwa kuingia kwenye michunao hiyo, maandalizi duni na pia kushuka kwa viwango vya timu zetu katika miaka ya karibuni.
Lakini hali imekuwa tofauti, miamba hiyo ya soka ya Tanzania miaka nenda, rudi leo inakutana kwenye fainali ya michuano hiyo, baada ya kufanya kazi ngumu kuanzia mechi za makundi hadi Robo Fainali na Nusu Fainali.
Simba iliyokuwa Kundi A, ilifuzu kama kinara wa kundi hilo, baada ya kujikusanyia pointi nane kutokana kushinda mechi mbili na kutoka sare mbili, utamu zaidi kipa Juma Kaseja akiweka rekodi ya kuwa mlinda mlango pekee ambaye hakuruhusu nyavu zake kutikiswa hata mara moja katika hatua ya makundi.
Simba ikakutana na mabingwa wa Uganda, Bunamwaya FC katika Robo Fainali na wakafanikiwa kushinda mabao 2-1, shukrani kwake kiungo Mkenya, Jerry Santo Evans aliyefunga bao la ushindi dakika ya 84, katika mchezo ambao dhahiri ulikuwa mgumu kwa Wekundu wa Msimbazi.
Baada ya hapo, Simba ikakutana na timu ngumu, tena sana kulingana na timu zote zilizokuwa kwenye michuano hii, El Merreikh ya Sudan, wengi miongoni mwa wachambuzi wa soka wakiipa timu hiyo kura chache mno za kukata tiketi ya kucheza mechi ya mwisho.
Mchezo ulianza vibaya kwa Simba, wakitanguliwa kufungwa bao na mabingwa wa Sudan, dakika ya 12 mfungaji akiwa ni Adiko Rime, kabla ya mshambuliaji mkongwe Ulimboka Alfred Mwakingwe kuisawazishia timu hiyo bao tamu kwa kichwa cha mkizi, dakika ya 24.
Dakika 90 zilitimu matokeo yakiwa 1-1 na dakika 30 za nyongeza pia hazikubadilisha matokeo na ndipo mchezo ulipohamia kwenye mikwaju ya penalti, Simba ikashinda 6-5, shujaa wa michomo hiyo Juma Kaseja akicheza penalti ya Mzambia Jonas Sakuwaha.
Sasa Simba leo watamenyana na watani wao wa jadi, Yanga katika fainali, hii ikiwa ni mara ya tatu kihistoria timu hiyo kukutana katika hatua hiyo ya michuano hii, kwanza mwaka 1975 na pili mwaka 1992, mechi zote zikipigwa visiwani Zanzibar na kila timu ilishinda mechi moja.
Mabao ya Sunday Manara na Gibson Sembuli (sasa marehemu) mwaka 1975 yaliipa Yanga ushindi wa 2-0 dhidi ya Simba waliokuwa mabingwa watetezi na kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza- wakati ushujaa wa kipa Mwameja Mohamed kupangua mikwaju ya penalti uliipa Simba ushindi wa penalti 5-4 dhidi ya Yanga na kutwaa tena taji hilo.
Kwa Dar es Salaam Simba na Yanga hazijawahi kukutana kwenye michuano ya Kagame, ingawa mwaka 2008 zilipaswa kumenyana katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu, lakini Watoto wa Jangwani ‘wakapotea’ njia ya kuelekea ulipo Uwanja wa Taifa, na Wekundu wa Msimbazi wakapewa ushindi wa mezani.

SIMBA ILIVYOTWAA MATAJI SITA YA AWALI:
Simba ndio bingwa wa kihistoria wa michuano hii, ikiwa imetwaa taji hilo mara sita, ikifuatiwa na AFC Leopards na Tusker za Kenya, ambazo zote zimetwaa taji hilo mara tano kila moja, wakati Yanga sawa na APR FC ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, SC Villa ya Uganda zimetwaa mara tatu kila moja taji hilo.
Luo Union, El-Merreikh zimechukua mara mbili kila moja, ATRACO, Rayon Sport za Rwanda, KCC na Polisi FC za Uganda kila moja imetwaa mara moja.

ZANZIBAR MWAKA 2002:
Michuano ya mwaka huo, ilianza Februari 16, ikishirikisha timu za Prince Louis ya Burundi, Mebrat Hail ya Ethiopia, Oserian Fastac, Tusker FC za Kenya, waliokuwa mabingwa watetezi, APR ya Rwanda, Elman ya Somalia, Simba SC, SC Villa na wenyeji Forodha na Mlandege za Zanzibar.
Simba ilipangwa Kundi B pamoja na Tusker, Forodha, Prince Louis na Elman na mechi ya kwanza Februari 8, ililazimishwa sare ya bila kufungana na Elman, kabla ya Februari 21 kutoka nyuma kwa bao 1-0 lililofungwa na Seleman Nsabah dakika ya 14 na kuifunga 2-1 Prince Louis, Emmanuel Gabriel akisawazisha dakika ya 27 kabla ya Yussuf Macho ‘Musso’ kufunga la pili dakika ya 78.
Febaruari 23 katika mchezo wa tatu, Simba iliitandika Forodha mabao 3-1, Joseph Kaniki akitangulia kufunga dakika ya 22, Steven Mapunda ‘Garrincha’ akifunga la pili dakika ya 65 na Macho kupiga la tatu dakika ya 90 na Februari 25, Wekundu hao wa Msimbazi walihitimisha mechi zao za Kundi B kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya 1-0, waliojifunga wenyewe dakika ya 88, Kevin Malumbe akimfunga kipa wake katika harakati za kuokoa.
Kwa matokeo hayo, Simba iliongoza Kundi hilo kwa pointi zake 10, na kwenye Nusu Fainali Machi Mosi, iliifunga Mlandege mabao 2-0, wafungaji
Macho dakika ya 37 na Sheikhan Rashid kwa penalti dakika ya 90, kabla ya kuifunga Prince Louis Machi 3 kwenye fainali, bao pekee la Nteze John Lungu dakika ya suita ya mchezo.
Siku hiyo, kikosi cha Simba SC kilikuwa; Mohamed Mwameja, Said Sued, Ramadhani Wasso/ Majuto Komu dk 35, Amri Said, Boniface Pawasa, Suleiman Matola, Stephen Mapunda/Joseph Kaniki dk 74, Shekhan Rashid, Yusuf Macho, Nteze John/Emmanuel Gabriel dk 61 na Mark Sirengo.

DAR ES SALAAM MWAKA 1996:
Michuano ya mwaka huo, Simba ikiwa bingwa mtetezi ilipangwa Kundi A pamoja na Al Hilal ya Sudan, APR ya Rwanda na Small Simba ya Zanzibar.
Ilianza kwa kuifunga 2-0 Small Simba, kabla ya kufungwa 1-0 na APR na baadaye kuibwaga 1-0 Al Hilal.
Simba ikafuzu kuingia Nusu Fainali kama mshindi wa pili wa Kundi hilo,na kukutana na Gor Mahia ya Kenya na kufanikiwa kushinda 1-0, bao pekee la Bitta John.
Katika fainali, Simba ilikutana na APR na bao pekee la beki mahiri enzi hizo George Magere Masatu dakika ya 115, baada ya kutimu dakika 90 bila timu kufungana, liliipa Simba ubingwa wa tano wa michuano hiyo.

DAR ES SALAAM MWAKA 1995:
Michuano ya mwaka huo pia ilifanyika Dar es Salaam na Simba walipangwa Kundi A tena pamoja na Express ya Uganda, Morris Supplies ya Somalia na Adulis ya Somalia.
Katika mchezo wa kwanza ililazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Express, kabla ya kuifunga Morris Supplies 3-1 na Adulis 4-1, hivyo kuongoza Kundi hilo kwa kufikisha pointi saba na kutinga Nusu Fainali, ambako ilikutana na El Mourada ya Sudan Februari 9 na kushinda 1-0, hivyo kujikatia tiketi ya fainali.
Ilikutana na Express ya Uganda katika fainali na dakika 120 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1, Hussein Amaan Marsha akitangulia kuwafungia waganda katika harakati za kuokoa dakika ya 51, lakini swahiba wake George Masatu akasawazisha dakika ya 53.
Dakika 120 zikamalizika timu hizo zikiwa zimefungana 1-1 na ndipo kwa mara nyingine, umahiri wa kipa Mwameja Mohamed ukainufaisha Simba kwenye mikwaju ya penalti na ikashinda 5-3.

ZANZIBAR MWAKA 1992:
Wakiwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, walikutana na watani wao wa jadi, Yanga katika fainali.
Kwa kuwa mwaka 1975 Yanga iliifunga Simba mabao 2-0 visiwani Zanzibar, wengi waliamini historia itajirudia na mwaka 1992, ila mambo yakawa tofauti.
Ikitokea Kundi A, Simba ilizipiga Bata Bullets ya Malawi na Small Simba ya Zanzibar na kutinga Nusu Fainali, ambako iliifunga Rivatex Eldoret ya Kenya mabao 2-0.
Katika fainali, dakika 120 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1 na mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti na kwa mara nyingine kipa wa zamani wa Reading ya England, Mwameja Mohamed akaonyesha umahiri wake kwa kucheza penalti ya Abubakar Salum ‘Sure Boy’ na baadaye ya David Mwakalebela hivyo kuipa Simba ubingwa wa mwaka huo.

DAR ES SALAAM MWAKA 1991:
Kombe hilo halikuwahi kukanyaga tena Tanzania, tangu Yanga waende kuliacha Kenya mwaka 1976 na michuano ya mwaka 1991 ilikuwa mkombozi wa taifa letu.
Ikishirikisha timu za Gor Mahia ya Kenya, Limbe Leaf Wanderers ya Malawi,
El-Maorada ya Sudan, SC Villa ya Uganda na wenyeji Simba SC na Coastal Union ya Tanga, ilifanyika katika vituo vya Dar es Salaam na Tanga.
Simba iliongoza Kundi A mjini Dar es Salaam na kutinga Nusu Fainali ambako iliifunga Gor Mahia na kukata tiketi ya kuingia fainali ilipokutana na SC Villa ambako ilishinda mabao 3-0, wafungaji Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ aliyefunga mawili na Hassan Afif moja.
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba kilichorejesha Kombe hilo nchini kilikuwa; Iddi Pazi, Raphael Paul, Twaha Hamidu, Jamhuri Kihwelo ‘Mrema’, Method Mogella (sasa marehemu), Iddi Suleiman ‘Meya’, Issa Kihange, Bakari Iddi, Ayoub Mzee/Hassan Afif, Zamoyoni Mogella na Itutu Kigi ‘Road Master’.
Ambao hawakushirikii mechi hiyo walikuwa ni Mackenzie Ramadhan, Khalfan Ngassa, Gebo Peter, Hasan Banda, Mavumbi Omar, Hamisi Gaga, Frank Kasanga Bwalya.
Mambo mawili ya kukumbukwa kwenye michuano hii; kipa Iddi Pazi ‘Father’ alicheza mechi zote za Simba bila kuruhusu bao hata moja, lakini pia kocha Abdallah Kibadeni ‘King’ alimfukuza beki tegemeo wa timu hiyo wakati huo Frank Kasanga ‘Bwalya’ kwa utovu wa nidhamu na akaamua kumtumia kama sentahafu kiungo Method Mogella badala ya kiungo.

DAR ES SALAAM MWAKA 1974:
Hii ilikuwa michuano ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kufanyika na ilichezwa kwa mtindo wa Ligi mjini Dar es Salaam ikishirikisha timu za Simba SC, Navy FC ya Zanzibar, Simba ya Uganda na Abaluhya FC ya Kenya.
Simba ilianza kwa sare ya 2-2 na Navy FC, kabla ya kuifunga Abaluhya FC 1-0 na badaaye kutoka sare ya bila kufungana na Polisi Uganda.
Kwa matokeo hayo, Simba ikachukua ubingwa kwa kufikisha pointi tano, ikifuatiwa na Abaluhya iliyofikisha pointi tatu, Navy pointi mbili sawa na Simba ya Uganda.
Hivyo ndivyo Simba ilivyotwaa mataji yake sita, vipi kwa watani wao wa jadi, Yanga walichukuaje mataji yao matatu?





YANGA ILIVYOTWAA MATAJI MATATU YA AWALI:
Yanga iliyokuwa Kundi B la michuano ya mwaka huu, ilifuzu kama kinara wa kundi baada ya kujikusanyia pointi saba kutokana na kushinda mechi mbili na kutoka sare moja.
Katika Robo Fainali, Yanga ilikutana na Red Sea ya Eritrea na kushinda kwa penalti 6-5, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za mchezo huo.
Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na St George ya Ethiopia na kushinda tena kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120. Sasa leo inacheza fainali na watani wao wa jadi, Simba SC, hii ikiwa ni mara ya tatu kwao kukutana kwenye fainali ya michuano hiyo. Yanga tayari ina mataji ya michuano hiyo na leo inasaka la nne, je hayo matatu ilichukuaje?

ZANZIBAR MWAKA 1975:
Iliingia kama bingwa wa Tanzania baada ya kuifunga Simba SC katika fainali ya Ligi mwaka 1974 Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, wakati watani wao hao waliingia kama mabingwa watetezi wa michuano.
Yanga ilipangwa Kundi B pamoja na Express ya Uganda na Mufulira Wanderers ya Zambia. Yanga ilianza kwa kuifunga Express FC mabao 4-0 na baadaye kutoka sare ya 1-1 na Mufulira, hivyo kuongoza Kundi hilo na kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Yanga iliifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 na kukata tiketi ya kuingia fainali Janauri 13, mwaka huo ilipokutana na watani wao wa jadi, Simba SC.
Mabao ya Sunday Manara ‘Computer’ na Sembuli yaliipa Yanga ushindi wa 2-0 na taji la kwanza la michuano hiyo.

KAMPALA, UGANDA MWAKA 1993:
Ilikwenda kama bingwa wa Bara na watano wao, Simba walikwenda kama watetezi wa taji na huko Yanga walipangwa Kundi A pamoja na wenyeji SC Villa na Malindi ya Zanzibar.
Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilifungwa 3-1 na Villa, siku hiyo kabla ya kuibuka na kuifunga Malindi mabao 2-1, yote yakitiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’, sasa marehemu, hivyo kukata tiketi ya kuingia Nusu Fainali.
Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na Express FC na kushinda mabao 3-1, hivyo kutinga fainali ambako ilikutana tena na SC Villa.
Kwa kuzingatia matokeo ya mchezo wa awali kwenye Kundi A, Yanga haikupewa nafasi kabisa ya kufurukuta mbele ya SC Villa, lakini mambo yalikuwa tofauti, mabao ya Said Mwamba na Edibily Lunyamila, yaliipa timu hiyo ushindi wa 2-1 pamoja na taji la pili la michuano hiyo.
Marehemu Kizota aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo.

KAMPALA, UGANDA MWAKA 1999:
Ilikwenda kama bingwa wa Bara, ikiwa mwakilishi pekee na ilitua huko, huku mashabiki wengi wa soka Uganda wakiwa na kumbukumbu ya kile kilichofanywa na klabu hiyo mwaka 1993.
Timu zilizoshiriki michuano hiyo ni Vital'O ya Burundi, Mebrat Hail ya Ethiopia, AFC Leopards ya Kenya, Kiyovu Sport, Rayon Sport za Rwanda,
Naadiga Dekedaha ya Somalia, KMKM ya Zanzibar, Al Hilal ya Sudan, Yanga, wenyeji Express na SC Villa za Uganda wakati Red Sea ya Eritrea ilijitoa dakika za mwishoni.
Kwa matokeo hayo, Kundi D ilimokuwa Yanga lilibakiwa na timu mbili tu, yaani mabingwa hao wa Bara na mabingwa watetezi.
Mechi ya kwanza, Yanga ilifungwa 3-0 na Rayon Januari 4 na ziliporudiana siku mbili baadaye, Yanga walilipa kisasi kwa ushindi wa 3-0 pia, mabao ya
Sekilojo Chambua dakika ya 23 na 57 na Kali Ongala dakika ya 59.
Katika Robo Fanali, Yanga ilikutana na Al Hilal Januari 10 na kushinda mabao 2-1, wafungaji Salvatory Edward dakika ya 14 na Edibily Lunyamila dakika ya 89 kwa penalti.
Katika Nusu Fainali, Yanga ilikutana na Vital’O ya Burundi Januari 13 na kushinda mabao 3-2, wafungaji Kally Ongara dakika ya 16, Bakari Malima dakika ya 78 na Said Mhando dakika ya 90.
Hivyo kwa mara ya pili, Yanga ilikutana na SC Villa kwenye fainali kukumbushia vitu vya mwaka 1993 na safari hii mambo yalikuwa mazito zaidi, kwani dakika 120 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1 Lunyamila akiisawazishia Yanga dakika ya 42, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kufunga dakika ya saba tu ya mchezo huo.
Mchezo ukahamia kwenye mikwaju ya penalti na Manyika Pater akaingia kwenye orodha ya makipa hodari wa kupangua penalti baada ya kupangua mikwaju miwili, Yanga ikishinda kwa penalti 4-1, Uwanja wa Nakivubo.
Hivyo ndivyo Yanga ilivyotwaa mataji yake matatu na leo inashuka dimbani kuwania taji la nne, je mambo yatakuwaje? Hapana shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona mambo yatakuwaje Uwanja wa Taifa jioni ya leo.

No comments:

Post a Comment