Search This Blog

Thursday, July 14, 2011

KWANINI MATOLA ASIWE NA MAJUKUMU KAMA YA ZIDANE NDANI YA SIMBA?

Mchezo wa soka ni mchezo ambao unachezwa na watu kumi na moja uwanjani ambao wana idara tofauti na majukumu tofauti ya kufanyia kazi, mfano kuna makipa ambao kazi yao ni kuzuia mpira usitinge wavuni.
Kuna mabeki ambao kazi yao ni kuhakikisha kipa hadhuriki na mchezaji wa timu pinzania hapati upenyo wa kuja kukwamisha mpira wavuni , kuna viungo ambao wengine huwa na kazi ya kuwalinda mabeki na wengine wanasaidia idara ya ushambuliaji na kuna washambuliaji ambao kazi yao ni kufunga ,wachezaji hawa kama ulivyoona wana idara tofauti ila kwa pamoja wanaunda timu ambayo ina lengo moja tu nalo ni kupata ushindi iwe ni kwenye mechi ya ligi, kombe na kadhalika .
Wachezaji wanacheza ndani ya uwanja ila kuna wachezaji wengine ambao wako nje ya uwanja ambao wanaanzia kwa kocha mkuu.
Kuna mifumo mbalimbali ambayo makocha wanafanyia kazi, kuna makocha ambao kazi yao ni kufuatilia kila kitu kinachohusu timu na wanasimamia mazoezi wao wenyewe kama vile Arsene Wenger,Fabio Capello na wengineo ambao wanafanya kila kitu mpaka kupanga koni wakati wa mazoezi hadi kuipanga “first eleven” na kuna wengine ambao wanafanya mambo kwa ujumla huku wakisaidiwa na timu ya watu mfano mzuri ni Harry Redknapp, Sir Alex Fergusson, Jose Mourinho na Kenny Dalglish.
Hawa wanasaidiwa na watu kama makocha wa makipa ambao ukienda Old Trafford utamkuta mtu anaitwa Luke Steele ambaye ni kocha wa makipa wote wa Manchester United , pia wanasaidiwa na makocha wa wachezaji kwa nafasi zao kama unakuta kuna kocha wa viungo mfano Tim Sherwood ambaye anawanoa viungo pale White Hart Lane na hata makocha wa mabeki na washambuliaji halafu kuna kocha wa timu ya kwanza yaani “first team coach” kama Joe Jordan wa tottenham, steve Clarke wa Liverpool na Mike Phelan pale Old Trafford .
Wote hawa ndio hapa wanaitwa wachezaji wa nje ya uwanja ila kuna eneo lingine ambalo kuna wachezaji wa nje ya uwanja nalo ni eneo la chumba cha mikutano ambapo kwa lugha ya kigeni “board-room”. Hili ni eneo muhimu sana ambalo pengine ndio kiini kabisa cha mafanikio ya timu . Nchi mbalimbali zina mifumo mbalimbali ya kuwapa watu madaraka ambayo ni kiungo cha uwanjani , benchi la ufundi na chumba cha mikutano ambako kuna wakurugenzi wa timu .



Ukienda Italia na Hispania Sporting directors na ukienda England kuna technical directors . Watu hawa kama ingekuwa uwanjani wangeweza kucheza eneo la namba sita ile ya kizamani ambayo falsafa yake ni kuwa mchezaji wa kila nafasi .
Miezi michache iliyopita Real Madrid ilikuwa na mtu anayeitwa Jorge Valdanao , mtu huyo hakuwa na uhusiano mzuri na kocha wake Jose Mourinho na ilifikia hatua ya kuwa mmojawapo ilibidi aondoke na hapo Valdano alionyeshwa njia kupitia kwa Rais wa timu Florentino Perez ambaye ni mtu wake wa karibu , alimwambia kuwa unaondoka hapa lakini wewe ni mwanangu na nitakupa shavu sehemu nyingine na maisha yanaendelea .
Mlango aliotokea Jorge Valdano akaingia mtu mmoja ambaye si mgeni machoni pa watu , si mgeni machoni pa walimwengu wa mchezo wa soka na zaidi ya yote si mgeni pale Real Madrid, Zinedine Zidane .
Hili lilikuwa pendekezo la Jose Mourinho ambaye kama anavyofahamika hajatazama karibu kwenye hili , hakika macho yake yametazama mbali kuliko watu wengi . Ukirejea nyuma kwenye msimu ambao Inter Millan ililiteka bara la ulaya Mourinho alimuita kwenye benchi mkurugenzi wa mawasiliano na mambo ya kimataifa wa Inter Milan Luis Felipe Madeira Figo . Kwa haraka unaweza usione mchango wa mreno huyu lakini amini usiamni , kubali ukatae Figo alichangia mawazo mengi kuiua Barcelona kwenye mchezo wa nusu fainali kama ilivyokuwa kwa Mourinho, kina Eto’o ,Militto na kina Sneijder. Baada ya hapo Mourinho anataka kurudia hayo kwa kumpa nafasi muhimu ya ‘ukurugenzi wa soka ‘ gwiji wa zamani wa Real na timu ya taifa ya Ufaransa Zinedine Zidane .
Zidane ni mtu ambaye anaheshimika ulimwenguni kote . Unakumbuka wakati kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa Laurent Blanc a.k.a “le president” au rais kwa Kiswahili alipojikuta katikati ya skendo ya ubaguzi wa rangi pamoja na shirikisho la soka la ufaransa , aliyemuokoa machoni pa watu hakuwa Nicolas Sarkozy rais wa ufaransa wala hakuwa rais wa shirikisho la soka la ufaransa bali alikuwa mtu ambaye neno lake kwa wafaransa ni kama sheria inayotungwa bungeni Zinedine Zidane .
Hiyo ndiyo heshima aliyo nayo Zidane , waandishi wa habari hawamuandiki vibaya mtu huyu , kumbuka alipomtwanga kichwa materazzi na kuinyima nchi yake ubingwa wa dunia , hakuna mwandishi aliyemuandika vibaya , wote walimuandika vibaya materazzi kwa kumdhihaki na kumfanya zizzou apandwe na hasira kiasi kile .



Na kubwa kuliko yote ni ukweli kuwa Zidane ni mtu ambaye anachukuliwa kama mfano wa kuigwa na wachezaji wote , ametwaa mataji yote unayoyajua ulimwenguni , Serie A, La liga,ligi ya mabingwa , kombe la dunia , kombe la ulaya, kombe la mabara na ametimiza ndoto ambazo wachezaji wengi nyota wametimiza na hiyo ni changamoto tosha kwa wachezaji wa Real Madrid ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawana kitu cha kuwa mshawasha na mzuka wa kupata ushindi kama wenzo Barcelona ambao wanae Zidane wao Pep Guardiola ambaye anajua jinsi ya kuwapa “inspiration” wachezaji wake.
Hapa nchini kwetu wapo kina Zidane ambao wanaweza kuwekwa kwenye maeneo muhimu ya mchezo wa soka katika ngazi ya vilabu na hata timu za taifa .
Klabu ya Simba ina mtu anayekwenda kwa jina la Selemani Matola , wenyewe Msimbazi enzi zake walikuwa wakimuita “veron”. Matola amekuwa Simba kwa muda mrefu na ndiye nahodha wa klabu hiyo ambaye ana historia nzuri inayong’aa . Katika wakati wake ametwaa mataji mengi sana ambayo hakuna nahodha mwingine sio tu Simba hata kwa watani wao Yanga anayeweza kumfikia , Matola ni mtu ambaye Simba inaweza kumfanya kama Madrid walivyomfanya Zidane . Wachezaji wa Simba wanaweza kufaidika kwa Matola kwani anaweza kuwapa vitu vingi sana vya msingi kwani amekuwa hapa walipo na amefanya wanayofanya wao na zaidi .
Super sports United walimwona Matola kwenye mchezo mmoja tu na ulitosha kuwashawishi kuilipa Simba fedha na kumchukua “Veron” kwenda naye ‘sauzi’ ambako kama isingelikuwa umri angecheza mpaka leo hii, na huko si kwamba alikuwa akisugua benchi , Matola alikuwa anaanza mechi karibu zote .
Kwa bahati mbaya hakuwahi kuwa na historia nzuri kwenye timu ya taifa lakini Matola ni gwiji pale Simba na klabu hii inahitaji mchango wake .
Ana mengi ambayo yanaweza kuisaidia klabu hii na kama viongozi wake ni watu makini wanaojua mpira wanaweza kufuata mfano wa Florentino Perez ambaye alimsikiliza Mourinho na kutimiza alichohitaji nacho ni kumpa Zizzou nafasi ya Mkurugenzi wa michezo, vivyo hivyo nafasi kama hii inaweza kumfaa Selemani Matola kwenye klabu ya Simba .

No comments:

Post a Comment