Search This Blog

Thursday, June 30, 2011

ESTHER CHABRUMA: TFF ANZISHENI LIGI KUU YA WANAWAKE


Naibu Mkurugenzi Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Juliana Yassoda
akimkabidhi bendera ya taifa nahodha wa timu ya taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’
Sophia Mwasikili wakati wa kuiaga timu hiyo inayokwenda Zimbabwe kushiriki
michuano ya COSAFA



CHENGA za maudhi, kasi na uwezo wa kumiliki mpira uwanjani vilimwezesha kupata umaarufu mkubwa katika muda mfupi kupitia soka la wanawake.

Mwonekano wake, mfupi na mwenye mwili wa wastani, pia ulisaidiwa kubatizwa jina lililozoeleka kama utambulisho wake kwa mashabiki wengi ndani na nje ya uwanja.

Huyu si mwingine bali ni Ester Chabruma, kiungo mshambuliaji wa timu ya soka ya Sayari FC na ile ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’.

Wengi hupenda kumuita Lunyamila wakimfananisha na mshambuliaji wa zamani wa Yanga Edibily Lunyamila ambaye alijizolea sifa kubwa wakati akisakata kabumbu.

Kwa sasa Ester ndiye mchezaji pekee mkongwe wa kikosi cha sasa cha Twiga Stars inayojiandaa kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake Oktoba mwaka huu, ameweza kuwamo katika kikosi hicho kwa miaka nane mfululizo tangu mwaka 2002.

Ester alizaliwa Julai 21, mwaka 1987, na kuanza kucheza soka akiwa na umri wa miaka nane katika timu ya watoto ya Sayari kisha ya wakubwa na kuendelea na timu hiyo hadi sasa, akiwa hajawahi kucheza klabu nyingine yoyoye hapa nchini.

"Tangu nilipojiunga na Sayari mwaka 1995 baada ya kuletwa na kaka yangu, sijaihama timu hiyo na sitarajii kuihama labda niende nje ya nchi," anasema Ester.

Akielezea maisha yake ya soka, Ester anasema kuzaliwa akiwa wa katikati ya kaka zake wawili ndicho kitu kikubwa kilichomfanya hadi akawa anapenda kucheza mpira wa miguu kwani alikuwa akienda na kaka zake katika michezo yao, huku mchezo mkubwa ukiwa wa mpira wa miguu.

"Kutokuwa na dada wa kucheza nae, kulinifanya niwe kila mahali na kaka zangu wakienda sehemu nami nimo wakicheza mpira wa miguu nami nimo, tangu hapo nikawa nacheza nao sambamba hadi kaka aliponileta Sayari," anasema Ester.

Katika historia yake ya soka, Ester alipata timu ya kucheza soka la kulipwa nchini Sweden ambako alicheza kwa misimu mitatu, kabla ya kurejea nchini.

"Nilipokuwa Sweden nilicheza katika ligi daraja la tatu nikiwa na klabu ya soka ya wanawake inayoitwa Kotodara FC katika misimu mitatu tangu mwaka 2003-06, maisha katika klabu ile yalikuwa mazuri sana ukilinganisha na hapa nchini," anasema.

Anasema Sweden ina mfumo mzuri wa ligi ya wanawake, ina ligi kuanzia Daraja la Nane hadi kufikia ligi kuu, ina timu nzuri ya taifa ya wanawake yenye wachezaji ‘professional’ kutoka klabu mbalimbali za ligi hiyo.

Anaongeza kuwa Sweden hata klabu za wanawake zinakuwa na viwanja vyao vya mazoezi na kuchezea mechi za ligi, kuliko hapa kwetu timu hazina viwanja hata vya kufanyia mazoezi.

"Nimejifunza mengi kupitia timu ile ndiyo maana hadi sasa sijaacha mpira, nikiwa kule nilipata mafunzo ambayo yananisaidia katika maisha ya mpira hadi sasa, yameniongezea kujiamini zaidi katika kazi yangu," anasema Ester.

Akielezea ilikuwaje hadi akarudi nchini Ester, anasema mkataba wake wa kuendelea kucheza katika timu hiyo uliisha, hivyo akarejea nchini Septemba, 2006 na kurudi tena katika timu yake ya Sayari hadi sasa.

Ester mmoja wa wachezaji wa kikosi kilichoundwa kwa mara ya kwanza cha Twiga Stars mwaka 2002 kwa ajili ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake mwaka huo.

Ester alikuwa ni mmoja kati ya wachezaji walioiokoa Twiga Stars kufuzu kucheza hatua ya pili ya michuano hiyo kwa kufunga bao la ushindi katika dakika ya 89 ya mchezo dhidi ya Eritrea kwa kuwa na ushindi wa 3-2 huku mechi ya kwanza wakiwa wametoka sare ya mabao 2-2, hivyo Twiga ilifanikiwa kuingia hatua ya pili kwa jumla ya mabao 5-4 lakini walitolewa na Zimbabwe katika hatua hiyo.

"Ushindi ule ulikuwa muhimu kwetu, ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki katika michuano mikubwa kama hiyo, najivunia mpaka sasa kwa kutumia nafasi ile vizuri," anasema Ester.

Akizungumzia tofauti iliyopo katika Twiga Stars ya mwaka 2002 na Twiga ya mwaka 2010, Ester anasema timu ya kipindi kile ilikuwa ikiundwa na wachezaji wengi wa klabu moja ya Sayari na wachezaji walikuwa na umri mkubwa lakini Twiga ya sasa inaundwa na wachezaji wadogo wanajua kucheza mpira pia wametoka katika klabu tofauti tofauti.

“Katika kikosi chetu mchezaji wa zamani ni mimi peke yangu niliyebaki hadi sasa, wengine hawapo katika timu ya taifa, wapo waliokufa, wengine wanacheza katika timu mbalimbali na wengine wamestaafu na kuachana na mpira kabisa,” Ester.

Ester ambaye ana matarajio ya kucheza kwa miaka mingine zaidi, anasema alipewa jina la mchezaji wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila kutokana na uchezaji wake, anasimulia jinsi alivyolipokea jina hilo.

"Sikuwa na jinsi ya kulikataa jina hilo ambalo lilinipa changamoto zaidi kwa kufananishwa na mchezaji mzuri kama Lunyamila, watu walisema tunafanana uchezaji, nafasi za uwanjani (wote washambuliaji), tunatumia mguu wa kushoto hivyo sikuona sababu ya kulikataa jina hilo," anasema Ester.

Akizungumzia mechi ya Twiga Stars dhidi ya Eritrea itakayochezwa hivi karibuni baada ya kuiondosha Ethiopia katika michuano ya kuwania nafasi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake baadaye huko Afrika Kusini ambapo Twiga ilishinda jumla ya mabao 4-2 katika mechi zote mbili, Ester anasema; "Tulikuwa na uhakika wa kufanya vizuri kwani Eritrea haikuwa timu ya kutisha sana.”

Ester ametoa wito kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka cha Wanawake Tanzania (TWFA) kuanzisha ligi kubwa ya soka la wanawake, ili kutafuta vipaji vipya zaidi huku akiamini wapo wachezaji wa kike wenye uwezo zaidi yake, lakini hawajapata nafasi ya kuonyesha uwezo wao, hivyo kupitia ligi kubwa wataonekana wengi.

Mshambuliaji huyo wa pembeni amewataka wazazi wawape nafasi watoto wao wa kike waweze kucheza mpira wa miguu kwani siyo uhuni kama wanavyodhani pia amewaasa wachezaji wa kike wasiwe na aibu ya kujitokeza kucheza, wajiamini na kuongeza kuwa wakiwa na juhudi watafanikiwa.

No comments:

Post a Comment