Search This Blog

Thursday, April 3, 2014

SIMBA YAWAVUTIA PUMZI YANGA, YAENDA KAITABA BILA TAMBWE, OWINO, MAYANJA ACHEKELEA UAMUZI WA LOGA!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam


SIMBA SC ya Dravko Logarusic imesafiri leo hii kwenda mjini Bukoba, mkoani Kagera kuwafuata wenyeji wao, `Wanankulukumbi` Kagera Sugar katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara utakaopigwa jumamosi uwanja wa Kaitaba.
Simba isiyohitaji ubingwa msimu huu wala nafasi ya pili, itacheza mchezo huo dhidi ya Kagera Sugar yenye malengo ya kushika nafasi ya tatu au nne msimu huu. 

Kocha Loga atawaingiza dimbani vijana wake akiwa na kumbukumbu ya kupigwa mabao 2-1 na Azam fc mechi iliyopita, wakati Kagera walitoka suluhu pacha ya bila kufungana na Ruvu Shooting uwanja huo huo utakaotumika jumamosi.

Katika kikosi cha Simba kilichoondoka leo, baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza wameachwa kwa madai ya kupumzishwa kusubiri mechi ya mwisho ya aprili 19 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Young Africans.

Kocha mkuu wa Kagera Sugar, Mganda Jackson Mayanja alikaririwa katikati ya wiki akisema kuwa Simba haimtishi sana, lakini anamuogopa sana mshambuliaji wake hatari, Mrundi, Amisi Tambwe.

Mayanja amepumua baada ya kusikia kuwa mshambuliaji huyo pamoja ba beki matata, Joseph Owino wameachwa katika kikosi kilichosafiri kuelekea mjini Bukoba.

Mbali na nyota hao wa kimataifa, wegine waliochwa ni mshambuliaji Betram Mwamboke, Kiungo  Abdulhalim Humud ‘Gaucho’  na beki wa kushoto Issa Rashid `Baba Ubaya”.

Sababu iliyoelezwa na benchi la ufundi la Simba sc, kupitia kwa kocha msaidizi, Suleiman Matola `Veron` ni kuwa Simba ina wachezaji wengi vijana ambao wanawaamini sana na watawapa matokeo mazuri  jumamosi.

Pia alisema wameamua kuwapumzisha nyota hao ili kuwaandaa kwa ajili ya mchezo muhimu dhidi ya Yanga.

Simba inajiwinda dhidi ya Yanga katika mchezo wa mwisho aprili 19 siku ambayo pazia la ligi kuu soka Tanzania bara litafungwa.

Timu hizi mbili zina upinzani mkubwa, hivyo Simba licha ya kuwa katika hali mbaya msimu huu watahitaji kushinda ili kulinda heshima yao.

Mzunguko wa kwanza zilitoka sare ya mabao 3-3 ambapo Yanga walifunga mabao yao kipindi cha kwanza na Simba kusawazisha yote kipindi cha pili.

Wakati wachezaji hao wakiachwa, Simba bado wamesema wanajiandaa vizuri kwa ajili ya  mechi zilizosalia kuhakikisha wanafanya vizuri.

Afisa habari wa klabu hiyo, Asha Muhaji alisema kupoteza mechi mbili mfululizo haikuwa mipango yao bali soka wakati mwingine linatoa matokeo kama hayo.

“Mashabiki wetu wana uchungu sana wa timu yao kufungwa mara kwa mara, lakini ni upepo mbaya kwetu msimu huu. Kikubwa tuendelee kuwa pamoja na kukubali matokeo yanayotokea uwanjani. Tutajipanga msimu ujao kwa kuimarisha kikosi chetu”. Alisema Asha.

Wakati hayo yakijiri kwa upande wa Simba, duru za habari kutoka ndani ya kikosi cha Kagera Sugar zinasema kuwa kikosi chao kimejiandaa vizuri kuwakabili Simba.

Murage Kabange, Kocha msaidizi wa Kagera Sugar aliuambia mtandao huu kuwa wanawaheshimu Simba licha ya kutokuwepo katika mbio za ubingwa mwaka huu.

“Tunajiandaa kupambana sana. Malengo yetu ni kuhakikisha tunawafunga na kujiweka mazingira mazuri ya kushika nafasi ya pili au tatu. Mashabiki wajitokeze kwa wingi jumamosi kutuunga mkono”. Alisema Kabange.

Mpaka sasa, Simba sc wapo nafasi ya nne baada ya kucheza mechi 23 na kujikusanyia pointi 36 pekee.

Msimu umekuwa mgumu kwa Simba ambao waliwafukuza Abdallah Kibadeni na Jamhuri Kiwhelo na kuwaleta Mcroatia,  Dravko Logarusic na Mtanzania, Suleiman Matola kwa lengo la kupata matokeo mazuri zaidi ya mzunguko wa kwanza.

Hata hivyo Logan na Matola wameshindwa kuwapa Simba mafanikio msimu huu na kuifanya kuwa timu ya `tia maji tia maji`.

Kagera Sugar wenyewe wameshuka dimbani mara  22 na kujikusanyia pointi 33 katika nafasi ya 5 ya msimamo.
Wamebakiza kiporo kimoja dhidi ya Yanga aprili 9 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Pia wamebakiza mechi dhidi ya Simba sc, Mgambo JTK  na Coastal Union.

Kwa upande wa Simba, mechi walizosaliwa nazo ni tatu ambapo ataanza kesho kutwa dhidi ya Kagera Sugar , atakutana na Ashanti aprili 13, na atahitimisha msimu kwa kuivaa Yanga ya Mholanzi, Hans Van Der Pluijm aprili 19 mwaka huu, uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment