Search This Blog

Monday, April 7, 2014

NUHU AKWEA PIPA KWENDA BONDENI KUFANYIWA UPASUAJI WA GOTI, KIMWAGA AANZA MAZOEZI MDOGO MDOGO!!

Pichani kulia ni Nuhu ,  Dk Mwankemwa (katikati) na Karim Mapesa (kushoto) wakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam. 

(Picha na Tovuti ya Azam)

Na Baraka Mpenja, Dar Es salaam

IKIWA ni sehemu ya kuwajali wanandinga wake, vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc,  alfajiri ya leo wamemsafirisha beki wao wa pembeni Samih Hajji Nuhu kwenda Cape Town, Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa goti la mguu wa kushoto.
Taarifa iliyotolewa na Azam fc kupitia Tovuti yake, Nuhu ameongozana na Daktari Mkuu wa klabu hiyo, Dk Mwanandi Juma Mwankemwa pamoja na Mweka Hazina wa timu, Abdulkarim Shermohamed Bahadour.
Nuhu  atafanyiwa upasuaji katika hospitali ya Vincent Palocci mjini Cape Town na Mtaalamu, Dk. Nicholas, ambaye ameweza kuwarudisha uwanjani wachezaji wengi wa Afrika Kusini waliopata maumivu makubwa.
Hii itakuwa mara ya tatu kwa Nuhu kufanyiwa operesheni ya goti hilo, baada ya awali kufanyiwa mara mbili nchini India, kwanza katika hospitali ya Mumbai chini ya Dk. Tanna na ya pili hospitali ya Pune.
Nuhu amekuwa nje ya Uwanja tangu mwaka jana na msimu huu wote hajagusa mpira kwa sababu ya maumivu hayo.
Wakati huo huo Taarifa njema kwa mashabiki wa Azam fc ni kwamba  mshambuliaji wake, Joseph Kimwaga Lubasha ameanza mazoezi mepesi baada ya kupata ahueni ya maumivu ya goti yaliyokuwa yakimsumbua.
Kimwaga amepewa programu maalum na dawati la tiba la Azam FC, chini ya Daktari Mkuu, Mwanandi Mwankemwa ambayo anaendelea hivi sasa.
Mchezaji huyo anatarajiwa kurejea rasmi uwanjani msimu ujao, baada ya kuwa nje kwa miezi miwili ya mwisho ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
Mbali na Kimwaga, wachezaji wengine majeruhi Azam FC ni beki wa kati, Ismail Gambo ‘Kussi Jr’ ambaye ataendelea kuwa nje kwa miezi miwili zaidi, viungoFarid Mussa na Ibrahim Mwaipopo ambao wote watakuwa nje kwa zaidi ya mwezi mmoja, maana yake kwa msimu huu hawatacheza tena.
Azam fc wanajiandaa na mchezo wa kesho kutwa ligi kuu soka Tanzania bara kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani dhidi ya Ruvu Shooting.
Hii itakuwa mechi muhimu kwa Azam fc katika mechi tatu zilizosalia kuhitimisha msimu huu wa 2013/2014.
Mpaka sasa Azam fc wapo kileleni baada ya kujikusanyia pointi 53 kwa kucheza mechi 23.
Kama Azam fc wanataka kutwaa ubingwa msimu huu wanahitaji kushinda mechi mbili kati ya tatu walizobakiza ili kufikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani wao wakubwa,  Yanga SC.
Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 49, na wamebakiza mechi tatu ambazo wakishinda zote watafikisha pointi 58 ambazo Azam fc watazivuka endapo watashinda mechi mbili kati ya tatu walizosaliwa nazo.
Mechi ya jumatano mabatini itakuwa na changamoto kubwa kwa Azam fc kwasababu Ruvu Shooting ina kikosi cha vijana wanaojua kucheza mpira.
Hata kama hawahitaji ubingwa wala nafasi tatu za juu wala kukwepa kushuka daraja, Shooting wataingia kwa lengo la kuvunja rekodi ya kutofungwa kwa Azam fc msimu huu.
Afisa habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alinukuliwa na mtandao huu kuwa wao watakuwa wa kwanza kumfunga Azam fc baada ya kushindikana katika mechi zake 23 alizocheza mpaka sasa.
“Azam ni kisiki cha mpingo. Timu zote zimeshindwa kuwang`oa. Sisi Ruvu Shootinga tutawang`oa hata kwa gereda. Tunajianda vizuri kuwaonesha Lambalamba kuwa sisi si timu ya kubeza hata kidogo”. Alisema Masau.
Wakati hayo yakijiri kwa Ruvu Shooting, Jafar Idd Maganga, Afisa habari wa Azam fc,  aliueleza mtandao huu kuwa kazi bado ipo mbele yao na wanashindana mpaka mechi ya mwisho.
“Hatuwezi kuwaza ubingwa kwa sasa, kwasababu mechi bado zipo. Ligi bado. Mpaka tutakapocheza mechi zote na kushinda ndio tutajihesabia kutwaa ubingwa”. Alisema Jafar.
Wakati Azam fc wakijiandaa na mchezo wa keshokutwa, nao mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Dar Young Africans watakuwa na kibarua kizito dhidi ya `Wanankulukumbi` Kagera Sugar katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Huu utakuwa mchezo muhimu kwa Yanga kwani watahitaji ushindi tu na si matokeo ya aina nyingine.
Hans Van Der Pluijm anayesemekana kuwa na kikosi bora zaidi msimu huu, atakuwa anakabiliana na Kagera Sugar ambao hawahitaji ubingwa wala nafasi ya pili.


Mpaka sasa Kagera Sugar wapo nafasi ya  5 baada ya kushuka dimbani mara 23 na kujikusanyia pointi 24.

No comments:

Post a Comment