Search This Blog

Wednesday, April 9, 2014

KWA HAYA, SIMBA SC HONGERENI NA KILA MTU AWAJIBIKE KWA NAFASI YAKE!!


Na Baraka Mpenja, Dar Es salaam

0712461976

SIMBA SC ni klabu kongwe ambayo watu wengi wanategemea ipate mafanikio waka wowote, lakini msimu wa mwaka jana na msimu huu imesuasua sana na kuwanyong`onyesha mashabiki wake waliokuwa na matarajio makubwa na kikosi chao.
Hata katika maisha ya kawaida, kuna wakati mambo yanakuwa safi na kuna wakati mambo yanakuwa magumu.
Kipindi cha mpito huwa kinatokea, na ndio maana kuna muda unaweza kuwa na pesa nyingi na kufurahia maisha, lakini ikafika wakati ukakosa hata mie moja.
Kimsingi inapotokea hali mbaya kwako ndio kipimo chako, na jamii itahitaji kuona jinsi unavyokabiliana na changamoto yako.
Mtandao huu ulifanya mahojiana na katibu mkuu wa Simba sc, Ezekiel Kamwaga ambaye kwa asilimia kubwa ndiye mtendaji mkuu wa shughuli zote za klabu.
Katika mahojiano hayo, Kamwaga aliwatoa hofu mashabiki wa Simba kuwa klabu haina mgogoro wowote baina ya benchi la ufundi na wachezaji, au viongozi na benchi la ufundi au viongozi na wachezaji.
Kamwaga alibainisha kuwa hali iliyowatokea Simba katika misimu miwili mfufulizo ni matokeo ya kimpira kwani wakati fulani upepo mbaya unaweza kuvuna kwa klabu yoyote.
Pia alisema hali kama hiyo inaweza kuipata klabu yoyoye katika mpira.
`Mr. Liverpool` aliitolea mfano klabu yake ya Liverpool inayoishabikia kuwa imekaa miaka 24 bila kutwaa kikombe.
Pia alisema kwasasa Manchester United imekuwa katika wakati mgumu zaidi, lakini hawana sababu ya kushuka morali.
Kamwaga alisema kama klabu kubwa namna hii huwa zinapitia wakati mgumu, basi ni fundisho hata kwa Simba.
Wakati Kamwaga akizungumza hayo, nilikuwa na shauku kubwa ya kusikia sasa wanafanyeje baada ya kuwa katika hali ngumu.
Mosi; niligundua kuwa Simba wamekubaliana na matokea. Katika maisha ya soka, kukubaliana na kile kinachotokea  uwanjani ni muhimu sana. Mpira huwa una kupanda na kushuka.l
Klabu inaweza kuwa bora na ikasheheni nyota wakubwa, lakini ikashindwa kufikia malengo yake.
Nilishawasikia makochwa wengi wakiwemo akina Pep Guardiola, Jose Mourinho, Alex Fergusons na wengine wengi wakisema kuwa hawaelewi kwanini wamepoteza mechi.
Kocha anasema kwa asilimia nyingi timu yake imemiliki mpira na kupata nafasi nyingi za kufunga, lakini imeshindwa kupata ushindi.
Mfano timu inapata nafasi saba za wazi, lakini inashindwa kutumia hata moja. Timu pinzani inapata nafasi moja inafunga na kushinda bao 1-0.
Kocha anaibuka na kusema timu bora imepoteza mchezo. Timu yake ulikuwa bora kwa idara zaole, lakini wamefanya kosa moja na kufunga.
Kumbe kuna wakati mpira huenda na bahati uwanjani.
Hili la Simba sc kukubali kuwa matokeo wayapatayo uwanjani ni ya kimchezo,  ni hatua nzuri.
Mengi yamezungumzwa  kuwa Simba kuna mgogoro baina ya viongozi na wachezaji, na wakati fulani ilisemwa kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, Dravko Logarusic hana mahusiano mazuri na wachezaji wake.
Sababu nyingi zilitolewa ni kuwa kocha huyo ni mkali mno kwa wachezaji wake, hivyo wanapocheza wanahofia kukosea na kutolewa.
Lakini kuna wakati liliibuka suala la kuchelewesha mishahara na posho kwa wachezaji.
Hapa yalisemwa mengi na wengine wakafika mbali na kusema mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage ameshindwa kuendesha klabu.
Kama kweli wachezaji wanacheleweshewa chao, ni jambo mbaya kwasababu linaweza kuwaathiri kiutendaji.
Unapotokea kiongozi wa juu wa Simba, Ezekiel Kamwaga na kuusemea uongozi wake kuwa hakuna mgogoro wowote ndani ya klabu bali ni matokeo tu, basi ni jambo jema katika kukabiliana na tatizo.
Hakuna haja ya kushikana uchawi, ilimradi wamekubali ukweli, basi ni jambo la kukaa chini na kutafuta mwarobaini wa tatizo lao.  Kwahili naipongeza Simba sc.
Pili; Simba sc baada ya kukubali matokeo, wamezungumzia jambo la pili na la msingi la mashabiki wao kutokataa tamaa na kuendelea kuiunga mkono timu yao.
Hapa Kamwaga alisema mashabiki wao wasiwe na hofu kabisa, wawe na imani na wachezaji wao, benchi la ufundi na uongozi wao.
Mashabiki wa mpira ni mchezaji wa 12 uwanjani.
Hakuna kocha wala kiongozi anayeweza kudharau mchango wa mashabiki katika maendeleo ya klabu.
Mashabiki ni msingi wa kufikia mafanikio kwasababu ni washauri wazuri na wanajenga morali kwa wachezaji wanapokuwa uwanjani.
Kuna raha kubwa kwa mchezaji anaposakata kabumbu na kusikia makelele mengi ya kumshangilia kwa kazi yake nzuri aifanyayo uwanjani.
Na ndio maana kumzomea mchezaji kunaweza kumpunguzia ufanisi wake hasa kama hajajengwa kisaikolojia kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa hiyo mashabiki ni muhimu sana katika mpira. Kwa kutambua hilo, uongozi wa Simba unawaangukia mashabiki wake, hasa katika wakati huu mgumu walionao.
 Kama ni shabiki wa kweli, huna haja ya kususia kwenda uwanjani kwasababu ya timu yako kukosa matokeo mazuri mechi za nyuma.
Lazima uendee kutoa mchango kwa nafasi yako ili kuifanya timu ijikwamue katika mazingira magumu.
Ipi ni sababu ya mashabiki wa Simba kupunguza kujaa uwanjani? Sidhani kama kuna nyingine zaidi ya matokeo mabaya kwa klabu.
Kamwaga anaposema mashabiki wasiwe na hofu na waendelee kuiunga mkono timu yao, basi mashabiki wa Simba wamsikie kiongozi wao na kubadili fikira zao kuelekea michezo miwili ya kufunga msimu.
Kuwakalisha mashabiki wao na kuwaomba waendelee kuwa karibu na timu ni hatua nyingne ya pili kwa Simba kutatua matatizo yao. Nawapongeza kwa hili pia.
Tatu; Simba sc wameonesha kuwa na mipango ya kuimarisha kikosi chao baada ya kushindwa kutamba kama miaka ya Nyuma.
Kamwaga alisema kwasasa timu inajiandaa na mchezo wa jumamosi dhidi ya Ashanti United ndani ya uwanja wa Taifa.
Baada ya mechi hiyo watakuwa wanajiandaa na mechi ya mwisho dhidi ya Yanga aprili 19 mwaka huu.
Hii ni mechi muhimu ambayo pengine inaweza kuleta umoja miongoni mwa wana Simba.
Kuna raha kubwa kwa Simba kuifunga Yanga au Yanga kuifunga Simba sc.
Mechi baina ya timu hizi huwa hazitabiriki hata kidogo na huwezi kutumia sababu ya timu moja kuwa na kikosi kizuri kusema itaifunga timu nyingine.
Mambo huwa yanabadilika kabisa na timu ya kawaida inaweza kupambana na kila mtu akabaki, ooh! Walikuwa wapi mechi za nyuma kucheza kama hivi?.
Kwa kutambua hilo, uongozi wa Simba umeanza mikakati ya kuelekea mechi hiyo kwa malengo ya kulinda heshima.
Baada ya mechi hiyo, Kamwaga alisema watakuwa na kikao kizito cha viongozi wa timu hiyo kujadili matatizo yaliyowasibu msimu huu.
Hapa wanatarajia kubaini mapungufu na makosa waliyoyafanya na kuambulia walichovuna msimu huu.
Bila shaka lengo la kikao hiki ni kutafuta njia ya kuboresha timu na si kushikana uchawi.
Kamwaga alisema msingi wa kikao hicho utajengwa kupitia ripoti ya benchi la ufundi.
Bila shaka Logarusic na Matola wana sababu nzuri zaidi ya mtu yeyote juu ya sababu za Simba kufanya vibaya.
Wao ni makocha na wanakaa na wachezaji wao kwa muda mwingi, hivyo kutumia taaluma yao wanafahamu kwanini Simba inapata matokeo mabaya.
Ripoti  yao itabainisha mapungufu ya kikosi na nini kifanyike ili kubadili hali ya hewa msimbazi.
Sina hakika kama watakuwepo, lakini nadhani bado uongozi wa Simba unawaamini makocha wao na watawapa nafasi nyingine.
Simba wanahitaji kutuliza akili katika kikao hiki ili wapate mwarobaini wa tatizo lao.
Kama watahitaji kusajili wachezaji wengine ili kuimarisha kikosi chao, basi litakuwa wazo zuri, lakini walimu waachiwe mpango huo.
Yupo Logarusic, Matola, Basena na watu wa kamati ya ufundi ambao wanao uwezo wa kutafuta wachezaji wazuri.
Masuala ya viongozi wasiohusika na mambo ya ufundi kuingilia usajili, itakula kwao na watashindwa kufikia malengo yao.
Cha msingi uongozi na kamati ya usajili inayoendeshwa na kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe, kazi yao pekee iwe ni kusainisha mikataba wachezaji waliochaguliwa na makocha wao.
Itakuwa jambo bora zaidi kuwaachiwa makocha wasajili wachezaji wanaowataka na kuwaacha wanaoona hawana faida kwa timu.
Makocha wanazunguko katika mechi 26 wakiongoza vikosi vyao. Wanawafahamu wachezji wao na kuwaona wachezaji wa timu nyingine, hivyo wanajua nani anawafaa na nani hawafai.
Wakiwaamini walimu hawa, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika klabu.
Nawapongeza Simba kwa mambo haya matatu niliyosema hapo juu ambayo kwa kifupi ni kukubali matokeo, kuwatoa hofu mashabiki na kuwataka waendelee kuiunga mkono klabu yao na tatu ni kuwa na mipango ya kuboresha kikosi chao kwa msimu ujao.
Kuishia nafasi ya nne kwa timu kama Simba, lazima inaumiza roho za mashabiki wengi waliopo nyuma ya klabu.
Kila mtu kwa nafasi yake akubali kuwajibika ili kufikia malengo yao.

Kila la kheri Simba sc katika mikakati yenu ya kuimarisha kikosi chenu ili Simba ya zamani urudi ulingoni.

2 comments:

  1. Nafikiri matokeo waliyoyapata Simba sc msimu huu yawe fundisho kwao kwamba ligi ina mechi 26 wawe wanajiandaa kwa mechi zote sio msimu mzima wanajiandaa kwa mechi mbili tu za simba na yanga ili wakitoka sare watambe mwaka mzima

    ReplyDelete
  2. We Uliye comment hapo juu utakuwa na STRESS sii bure!

    ReplyDelete