Search This Blog

Thursday, April 10, 2014

AZAM YAZIDI KUWANYIMA USINGIZI YANGA, YAITANDIKA RUVU SHOOTING 3-0, MWAIKIMBA, MAO, TCHETCHE WANG`ARA!!Na Baraka Mpenja, Dar Es salaam


0712461976


AKIWAANZISHA washambuliaji wake watatu, Gaudence Mwaikimba, Kipre Herman Tchetche na John Rapahel Raphael Bocco `Adebayor`, kocha wa Azam fc Mcameroon, Joseph Marius Omog amefanikiwa kuongeza pointi tatu muhimu baada ya kuwafumua maafande wa Ruvu Shooting mabao 3-0 katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara, kwenye uwanja wa Mabatini , Mlandizi mkoani Pwani.

Lengo la Omog lilikuwa ni kufunga mabao mengi katika mchezo huo ili kuendelea kujiweka mazingira mazuri ya kuiongoza Azam fc kuandika historia mpya ya kutwaa ubingwa wao wa kwanza tangu wapande ligi kuu mwaka 2008/2009.

Mipango yake ilianza kuzaa matunda dakika ya 8 ya mcheza ambapo mshambuliaji wake ambaye mara nyingi hukalia benchi, Gaudence Mwaikimba kufunga bao la kuongoza.

Azam fc walionekana kuwa na uchu wa kupata mabao zaidi,  na katika dakika ya 37 kipindi cha kwanza, winga machachari, Himid Mau Mkami alitia kambani  bao la pili kufuatia krosi nzuri iliyochongwa na beki wa kulia, Erasto Edward Nyoni.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa Azam fc kuwa kifua mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilipoanza, Azam fc walionekana kuendelea kuwepo mchezoni ambapo dakika ya kwanza tu, Kipre Herman Tchetche aliandika bao la tatu na kuwanyanyua mashabiki waliofurika uwanjani.

Kwa matokeo hayo Azam fc wamezidi kujikita zaidi kileleni kwa kufikisha pointi 56, pointi nne mbele ya mabingwa watetezi Yanga SC katika nafasi ya pili.

Yanga walikuwa wanaufuatilia mchezo huo  kwa makini ili kujiridhisha kama wataweza kutetea ubingwa wao msimu huu.

Jana wanajangwani hawa walishinda mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar na kuwasogelea Azam fc kileleni, lakini leo mambo yamezidi kuwa magumu zaidi kwao kutokana na matokeo ya Mabatini.

Ili kutetea ubingwa wao, Yanga wanahitaji kushinda mechi mbili walizobakiza dhidi ya JKT Oljoro na Simba sc, wakati huo huo wakiiombea mabaya Azam fc ipoteze michezo yote miwili.

Wakati Yanga wakiwa katika presha kubwa, Azam fc wao wanahitaji pointi tatu tu kuwavua ubingwa Yanga.

Wakishinda mechi moja kati ya mbili walizobakiza, wana Lambalamba watafikisha pointi 59 ambazo Yanga hawataweza kufikisha hata kama watashinda mechi zote walizosaliwa nazo kwa mabao 50.

Yanga wakishinda mechi mbili zijazo watafikisha pointi 58 kibindoni  ambazo Azam fc wataweza kuzivuka kama watashinda mechi moja tu kati ya mbili walizonazo mkononi.

Mechi ijayo, Azam fc watashuka dimbani dhidi ya Mbeya City katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Hii itakuwa mechi muhimu sana kwa Azam fc, lakini watahitaji kutumia nguvu kubwa kuwafunga wagonga nyundo hawa wa Mbeya kwasababu ya rekodi yao nzuri ya kutofungwa katika uwanja huo.

Mbeya City mpaka sasa wapo nafasi ya tatu katika msimamo wakiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi 24.

City wameshapoteza nafasi mbili za juu kwasababu wakishinda mechi mbili zilizobaki watafikisha pointi 52 ambazo zimeshafikiwa na Yanga, huku wakiwa na michezo miwili mkononi.

Hata kama Yanga watapoteza mechi mbili zijazo, kama Mbeya City watahitaji kuwa wa pili watahitaji kushinda mechi mbili zilizobaki kwa ida kubwa mno ya mabao.

Ukiangalia wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, Yanga wametia kambani mabao mengi mno zaidi ya Mbeya City. Hivyo bado nafasi ya pili kwao ni ngumu kuipata.

Hata hivyo kushika nafasi ya tatu si haba kwao kwasababu ni msimu wao wa kwanza.

Wakati Azam fc wakijiandaa kwenda Mbeya, tayari zipo tuhumu kwa wenyeji wao Mbeya City kuwa wamehongwa na wana Lambalamba ili kucheza chini ya kiwango.

Madai ya kuuzwa kwa mechi hiyo yamesambazwa kuhusu mambo matatu;
ambayo ni Timu ya Mbeya City kununuliwa basi na Klabu ya Azam,  Kocha wao Juma Mwambusi amejengewa nyumba maeneo ya Chamazi, na  wachezaji wao wamepewa fedha ili waweze kucheza chini ya kiwango dhidi ya Azam
.

Hata hivyo uongozi wa Mbeya City umekanusha tuhuma hizo na kusema watu wanaosambaza taarifa hizo hawana malengo mazuri na klabu yao, zaidi wanawachafua kwa mashabiki wao.

Bingwa atakayepatikana msimu huu atakuwa ni halali kutokana na ushindani mkubwa uliooneshwa na timu za juu.

Azam fc, Yanga na Mbeya City toka mwanzo wa mzunguko wa pili zimefukuziana mno na hatimaye sasa Mbeya City wamejitoa na kuwaacha Yanga na Azam fc wakiendelea kuchuana.

Sasa Yanga na Azam fc ni kutegeana tu, atakayepoteza mechi atamnufaisha mwenzake.

Lakini Yanga ndio watumwa kwa Azam fc kwasababu wanahitaji kutetea ubingwa wao, wakati huo huo wakihenyeka kutaka kusawazisha pengo la pointi nne dhidi ya  Azam fc.

Ligi hiyo itaingia raundi ya 25 Aprili 12 na 13 mwaka huu ambapo timu zote 14 zitakuwa viwanjani. Aprili 12 mwaka huu itakuwa Mtibwa Sugar vs Ruvu Shooting (Manungu, Morogoro), Coastal Union vs JKT Ruvu (Mkwakwani, Tanga), na Tanzania Prisons vs Rhino Rangers (Sokoine, Mbeya).

Aprili 13 mwaka huu ni Mgambo Shooting vs Kagera Sugar (Mkwakwani, Tanga), Simba vs Ashanti United (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Mbeya City vs Azam (Sokoine, Mbeya) na Oljoro vs Yanga (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha).

No comments:

Post a Comment