Search This Blog

Tuesday, April 8, 2014

AZAM FC KUANZA KUJENGA HISTORIA MUHIMU KESHO MABATINI, YANGA, KAGERA SUGAR KUWASHA MOTO TAIFA!!


Mtashangilia hivi hivi hapo kesho uwanja wa Taifa dhidi ya wana TamTam Kagera Sugar?

Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam

0712461976

MZUNGUKO wa 24 wa ligi kuu soka Tanzania bara  kuwania ubingwa  unatarajia kuendelea kesho kwa mechi mbili kupigwa katika miji ya Dar Es salaam na Pwani.
Mabingwa watetezi Dar Young Africans chini ya kocha mkuu,  Mholanzi Hans Van Der Pluijm watatupa karata yao muhimu dhidi ya wakata miwa wa Kagera Sugar katika dimba la Taifa jijini Dar Es Salaam.
Nao vinara wa ligi hiyo, Azam fc chini ya bosi, Mcameroon, Joseph Marius Omog watakuwa na kibarua kizito katika dimba la Mabatini Mlandizi mkoani Pwani dhidi ya wenyeji wao, Ruvu Shooting wanaonolewa na Mkenya Tom Alex Olaba.
Timu za Yanga na Azam fc zipo katika kinyan`anyiro cha ubingwa na mechi za kesho ni muhimu zaidi kwa timu zote.
Azam fc wanahitaji ushindi kwa nguvu zote ili kuendelea kujiwekea mazingira mazuri ya kuweka rekodi yao ya kutwaa taji la ligi kuu kwa mara ya kwanza tangu wapande msimu wa 2008/2009.
Mpaka sasa matajiri hao wa Bongo wapo kileleni kwa pointi 53 baada ya kushuka dimbani mara 23.
Yanga wanatakiwa kushinda mechi tatu zilizosalia ili angalau kuwa na matumaini ya kulibakisha kombe la maeneo ya makutano ya Twiga na Jangwani.
Mpaka sasa kikosi hicho cha Pluijm kimecheza mechi 23 na kujikusanyia pointi 49 kibindoni.
Ushindi kwa Yanga SC katika mchezo wa kesho ni muhimu mithiri ya dhahabu kwasababu kutawafanya waongeze pointi tatu, huku wakisikilizia matokeo ya Mabatini.
Kagera Sugar wanaingia katika mchezo wa kesho wakiwa hawana  malengo ya kutwaa ubingwa wala kushika nafasi ya pili katika msimamo.
Mpaka sasa wamepiga kambin nafasi ya tano wakiwa na pointi zao 34 baada ya kucheza mechi 23.

Wazee wa kuamua matokeo msimu huu kwa Azam fc, je, kesho watafua `dafu` kwa Ruvu Shooting Mabatini?

Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Murage Kabange aliueleza mtandao huu kuwa malengo yao ni kushinda mechi zote zilizosalia ili kuipata nafasi ya nne.
Kama kweli watashinda mechi zote tatu watafikisha pointi 43  ambazo Mbeya City wameshapita wakiwa nafasi ya tatu.
Kwa maana hiyo Kagera Sugar kwasasa wanaitaka nafasi ya nne ambayo imekaliwa na Simba SC yenye pointi 37.
Endapo Mnyama Simba sc atashinda mechi mbili zijazo dhidi ya Ashanti United na Yanga sc atavuna pointi sita na kufikisha pointi 43 kutoka 37 alizonazo sasa.
Msimu wa mwaka jana, Simba sc walishika nafasi ya tatu, na nafasi ya pili walikuwepo Azam fc, na ubingwa ulichukuliwa na Yanga sc.
Kagera Sugar wakiwa chini ya kocha mkongwe, Abdallak Kibadeni `King Mputa` walishika nafasi ya nne baada ya ushindani wa muda mrefu baina yake na aliyekuwa kocha wa Simba sc kwa wakati ule, Mfaransa Patrick Liewig.
Kama Kagera na Simba sc zitashinda mechi zao zote zilizosalia, zitafungana pointi na itabidi utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa utazamwe.
Safari hii timu hizi zimeshuka chini. Sasa zinagombeana nafasi ya nne kwasababu nafasi ya tatu ipo mikononi mwa Mbeya City ambao pia wanaweza kushika nafasi ya pili kutegemeana na matokeo ya timu za Yanga na Azam fc.
Kikosi Kagera Sugar kilichotoa sare ya 1-1 na Simba Kaitaba mechi iliyopita

Mchezo wa Kagera Sugar hapo kesho dhidi ya Yanga utakuwa na changamoto kubwa kwa timu zote kwasababu kila klabu ina malengo tofauti.
Yanga wanahitaji ubingwa na Kagera Sugar wanahitaji nafasi ya nne msimu huu.
Yanga wamekuwa wakiutumia vyema uwanja wake wa nyumbani, hivyo mpira mzuri unategemewa kuonekana  uwanjani.
Hata hivyo itakuwa mechi ngumu kwao kwasababu Kagera Sugar wana watu wanaoweza kuamua matokeo kwa wakati wowote akiwemo  mshambuliaji wao namba moja, Them Felix `Mnyama`.
Huyu ni mtu wa kuchungwa sana hapo kesho, kwasababu ukiachiwa nafasi moja anaweza kuwafanya Yanga wawe watumwa.
Hatutegemei mabadiliko  makubwa kwenye kikosi cha Yanga kwenye mchezo huo.
Bila shaka Pluijm atamuanzisha mlinda mlango wake chaguo la kwanza Deo Munish `Dida`.
Nafasi ya beki wa kulia itategemeana na mipango ya Mholanzi huyo. Kama Kelvin Yondani ataanzishwa beki ya kati, basi beki wa kulia anaweza kuanza Mbuyu Twite.
Endapo Yondani hatacheza kesho, basi beki wa kulia anaweza kuanza tena, Juma Abdul.
Nadir Haroub `Canavaro` kama kawaida lazima ataanza beki namba nne, huku kitasa akimaliza Mbuyu Twite.
Frank Domayo `Chumvi` atakalia nafasi ya kiungo wa ulinzi, huku winga wa kulia akianza Saimon Msuva.
Kiungo namba nane anaweza kuanzishwa kinda Hassan Dilunga.
Mshambuliaji wa kati anaweza kuanza Didier Kavumbagu, na namba kumi ikiwa mikononi mwa mzee wa `Hat Trick`, Mrisho Khalfan Ngasa.
Winga wa kushoto, Mganda, Hamisi Kiiza `Diego` anaweza kuanza katika mechi hiyo yenye umuhimu mkubwa kwa Pluijm.
Hata hivyo Jerryson Tegete, Hussein Javu, Hamis Thabit ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuanzishwa hapo kesho kutegemeana na mipango ya kesho.
Lakini kama Haruna Niyonzima atakuwa fiti, basi tutegemee mabadiliko kwenye kikosi hasa sehemu ya kiungo.
Kwa mechi ya Mabatini, Azam fc watakuwa kwenye wakati mgumu wa kuwafunga Ruvu Shooting ambao wametamba kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuwafunga Azam fc msimu huu.
Ruvu Shooting wapo nafasi ya  6 wakiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 23.
Wao hawana haja ya kutafuta ubingwa wala nafasi tatu za juu, bali ni kujiwekea heshima kubw aya kukifunga kikosi bora cha Mcameroon Omog.
Azam fc mpaka sasa hawajafungwa mechi yoyote, na wanahitaji kushinda mechi mbili tu kati ya tatu walizosaliwa nazo ili kujitangazia ubingwa msimu huu.
Kama watashinda mechi ya kesho, watahitaji kupiga hesabu katika michezo miwili ijayo dhidi ya Mbeya City na JKT Ruvu.
Mechi ya Mbeya City sokoine jijini Mbeya itakuwa ngumu kwa Azam fc kutokana na mazingira ya uwanja huo na rekodi ya wenyeji wao.
City ni washindani wa nafasi ya pili msimu huu, hivyo mikakati yao ni kuhakikisha wanawafunga Azam fc.
Endapo Azam watawafunga katika mchezo huo, watavunja rekodi ya Mbeya City ya kutofungwa uwanjani wa Sokoine.
Matokeo kwa Azam ni muhimu kuanzia hapo kesho, kwasababu hawana uhakika wa kule Mbeya.
Lakini wakirudi Chamazi Aprili 19 dhidi ya JKT Ruvu wanaweza kuwa na faida ya kushinda kwani huo ndio uwanja wao na wamekuwa na rekodi nzuri hapo.
Tutegemee ushindani mkubwa hapo kesho kutokana na ubora wa Ruvu Shooting.
Matokeo yatakayokuwa yanapatikana kadri muda utakavyokuwa unakwenda katika viwanja hivi viwili, Taifa na Mabatini, ndivyo ugumu wa mechi utakavyokuwa unaongezeka kwa Yanga na Kagera Sugar.
Kila la heri timu zote katika michezo ya kesho na waamuzi watakaopangwa kuchezesha wazingatie sheria 17 ili kuepuka tafrani uwanjani.
Hizo ni mechi muhimu sana kwa klabu zote. Ugumu wake hautokana na majina ya timu pinzani kwa Yanga na Azam fc, bali ni namna matokeo yalivyo muhimu kwao.

No comments:

Post a Comment