Search This Blog

Tuesday, March 25, 2014

YANGA WAANZA JALAMBA LA NGUVU, PRISONS WATINGA DAR KWA JEURI KUBWA!!


Na Baraka Mpenja , Dar es salaam


MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Young Africans wameweka kambi makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam kujiwinda na mchezo wa kesho kutwa  (jumatano) wa ligi kuu dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons kutoka Mbeya.
Yanga imeanza mazoezi yake jioni ya leo chini ya kocha mkuu, Mholanzi, Hans Van Der Pluijma akisaidiwa na Mzalendo, Charles Boniface Mkwasa `Master`.
Wakati huo huo, Prisons wamewasili jijini Dar es salaam jioni ya leo wakitokea Mkoani Morogoro walipoweka kambi yao.
Katibu mkuu wa Wajelajela hao, Inspekta Sadick Jumbe amesema maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yamekwenda vizuri na wamefika mapema ili kesho wajiweke sawa tayari kwa shughuli ya jumatano.
 “Yanga wanaonekana kuwa na mikakati mizito juu yetu kwasababu ya misemo yetu ya `Hatoki mtu hapa` na `moto hauzimwi kwa petroli`. Kweli lazima waogope kwani tumejipanga kuchukua pointi tatu”. Alisema Jumbe.
Jumbe aliongeza kuwa kwasasa wanahitaji pointi zaidi ya nne katika michezo yao iliyosalia, hivyo Yanga lazima wajipange vizuri.
“Niwaombe mashabiki wetu kuwa na imani na kikosi chetu. Tumejipanga vizuri na wajitokeze kuishangilia timu yao hapo kesho kutwa”. Alisema Jumbe.
Prisons wapo nafasi ya 10 wakiwa wamejikusanyia pointi 22, huku Yanga wakiwa nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi 43.
Mbeya City wapo nafasi ya tatu kwa pointi 42 na nafasi ya nne inakaliwa na Simba wenye pointi 36.

No comments:

Post a Comment