Search This Blog

Sunday, March 16, 2014

WACHEZAJI BONGO KUTOLIPWA MISHAHARA, POSHO KWA WAKATI KUSIWAFANYE MCHEZE VIBAYA, SIMBA, YANGA IWE DARAJA TU!!

Na Baraka Mpenja , Dar es salaam


INAFURAHISHA sana kuona mtu anatumia miguu yake kuingiza mabilioni ya fedha katika akaunti yake.
 Ukifuatilia `mkwanja` wanaoingiza wanasoka wanaocheza ligi kubwa ulimwenguni, hakika utaona jinsi gani kipaji kinaweza kumfanya mtu kuwa na heshima kubwa katika jamii.
Ukienda Ivory Coast hakuna asiyemheshimu Didier Drogba, Yaya Toure na wengine wengi. Ukifika Cameroon unakutana na Samuel Eto`o mwenye utajiri mkubwa zaidi, lakini wapo wengine wenye fedha  za kutosha.
Utajiri alionao Cristiano Dos Santos Aveiro Ronaldo unamfanya Ureno imheshimu,  pia Lionel Andrew Gorge Messi nchini Argentina anaheshimika sana.
Wapo wengine kama vile  Neymar,  Wayne Rooney na wengine wengi ambao wamejijengea heshima kubwa zaidi katika jamii kutokana na miguu yao.
Ukikaa chini na kufuatilia historia za wanasoka hawa mashuhuri, hakika utajifunza mengi, kubwa ni uvumilivu na bidii katika kazi zao.
Nidhamu waliokua nayo, juhudi zao katika mazoezi na kujitambua kumewafanya wawe hapo walipo.
Lengo langu si kuandika historia yao, lakini nikipata muda siku nyingine nitagusia ili kuwafahamisha wengi wetu kuwa mafanikio hayana njia mkato, malengo, juhudi, maarifa na kujitambua ndio silaha kubwa.
Nchini Tanzania, soka limekuwa na ubabaishaji mkubwa mno kuanzia viongozi, wachezaji na makocha wanaofundisha klabu mbalimbali.
Imekuwa ngumu kupata mafanikio kwa wachezaji wa kitanzania kutokana na sababu mbalimbali.
Naheshimu sana vipaji vilivyopo nchini. Ukipita mitaani  maeneo mengi ya mijini na hata vijijini ambapo yawezekana hata Televisheni za kuwaona wanasoka wakubwa hakuna, utaona vipaji vikubwa mno kwa vijana.
Inawezekana sisi ni miongoni mwa nchi zenye vipaji zaidi duniani, lakini kinachotutafuna ni mfumo wetu wa uendeshaji wa soka na aina ya wachezaji tulio nao.
Wachezaji wengi wanaocheza ligi ya Tanzania ukiongea nao, wanapenda sana kucheza klabu kubwa mbili, Simba na Yanga.
Sikatai kuwa Simba na Yanga ni klabu zenye mvuto zaidi nchini, na ndio maana kila mchezaji anatamani kuzichezea.
Sio wazo baya kufikiria kuzichezea timu hizi mbili kwasababu  zina nafasi kubwa ya kushiriki mashindano ya kimataifa.
Japokuwa Azam fc nao wameingia katika ushindani huo, lakini bado Simba na Yanga ndio habari ya mjini kwa Tanzania.
Imekuwa kawaida sana kwa mchezaji kuwa na kiwango kikubwa anapocheza nyingine  mfano Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Coastal Union, ila akigusa Simba na Yanga, yapo mawili. Anaweza kung`ara zaidi au kupotea.
Ukiangalia timu hizi mbili, moja ya tatizo kubwa linalozitafuna ni Viongozi. Watu wengi wanapopewa dhamana ya kuongoza klabu hizi, huwa wanaishia kuwa wachumia matumbo kwa faida  yao na familia zao.
Wanaendesha klabu kwa mfumo wa bora liende, huwa hawana mipango ya mbele zaidi.
Ndio maana mwaka huu wanaweza kuwa na timu nzuri na kujitahidi kupambana kimataifa, lakini msimu unaofuata timu inakuwa mbovu kupita maelezo.
Tunafahamu kuwa viongozi wamebeba lawama nyingi za kuwaharibu wachezaji wao, kwani malalamiko ya kutowalipa mishahara na posho wachezaji yanasikika kila kukicha.
Wachezaji wengi wanazidai klabu hizi na malimbikizo ya madeni ni makubwa .
Kwa haraka huwezi kuamini kama Simba na Yanga wanaweza kushindwa kuwalipa wachezaji wao kutokana na rasilimali walizonazo.
Wanao mtaji mkubwa wa mashabiki na wanachama. Hivi wakiamua kutengeneza jezi na kuziuza kwa kusimamia vizuri si wanaweza kufika mbali.
Mbali na kuwepo kwa matatizo ya viongozi katika klabu hizi, suala la msingi ni kuangalia jinsi wachezaji wa timu hizi wanavyoshindwa kujielewa .
Sina shaka kabisa na malengo ya wachezaji wetu. Kila ukiwauliza wanakwambia wanatamani kucheza ligi kubwa duniani.
Mpaka sasa hajatokea mchezaji wa Tanzania katika ligi kubwa mfano Uingereza, Hispania, Italia, Ujerumani.
Bado tunajivunia Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Mwinyi Kazimoto ambao wanaonekana kwa wenzetu waliotuzidi kidogo.
Mafanikio waliyopata vijana hawa wawili wa TP Mazembe  si haba. Hii  ni klabu kubwa Afrika. Wana fedha za kutosha, ndio maana huwezi kuwasikia wachezaji wakilia njaa.
Wiki chache zilizopita, nimekuwa nikisikia kuwa Simba sc kuna matatizo baina ya viongozi na wachezaji wake.
Haijawa rahisi kujua hili kwasababu hakuna mchezaji yeyote aliyejitokeza hadharani kusema matatizo yao, wala viongozi kueleza kama kuna mvutano.
Lakini kwa taarifa za chini ambazo wachezaji  wanasema ni kuwa kumekuwepo na tabia ya kucheleweshewa mishahara na posho zao.
Nadhani kama hili lipo, basi kuna watu ambao wanashindwa kuwajibiki ndani ya uongozi.
Pia suala la kocha wao kuwa mkali na kufuatilia nidhamu limekuwa gumzo miongoni mwa watu wengi. Najua  Dravko Logarusic ni mkali na huwa hana mchezo.
Nimewahi kukutana na kocha huyo mara kadhaa, ni kweli anapenda nidhamu na kama hujitumi lazima ile kwako.
Kuhusu malalamiko kwa kocha huyu kuwa mkali, napata wasiwasi kama wachezaji wanajua wapi wanatakiwa kwenda.
Ukienda Ulaya wanakokutaka, nidhamu imekuwa nguzo ya kila klabu. Kama unamchukia kocha kwa kufuatilia nidhamu na kuwa mkali kulinda uwezo wako, hakika unatupa shaka kama kweli una malengo.
Nafahamu kuwa wachezaji wengi wa Kitanzania nidhamu ipo chini. Matumizi ya pombe, sigara, dawa za kulevya, anasa na kusahau mazoezi imekuwa kawaida.
Kwa mfumo huu ni ngumu sana kufika mbali kwani huko mbele kuna mambo magumu zaidi kama una tabia za ajabu.
Sipendelei sana kuona wachezaji wanacheza chini ya kiwango eti kwasababu hawajapewa mishahara au posho.
Najua vijana wetu wapo kusaka mafanikio na wanataka kufika mbali. Kwa maana hiyo, Simba na Yanga ni kama daraja kwao.
Pale sio mahali wanapohitaji. Wanataka kusonga mbele zaidi. Kutolipwa mishahara au posho isiwe sababu kubwa kuwafanya wao wafanye vibaya.
Kuna faida kubwa ya kujituma kazini hata kama mazingira ni magumu. Naelewa ugumu wa maisha. Ukiwa na njaa ufanisi wa kazi unapungua.
Lakini kuwepo kwa changamoto kazini kwako kusikufanye uharibu kwasababu ndoto zako sio kukaa pale milele.
Kama Simba na Yanga ni daraja, basi wachezaji wanatakiwa kucheza mpira kwa nguvu, wasitumie kigezo cha kutolipwa mishahara kuharibu kazi.
Sifurahii tabia ya viongozi kutowajali wachezaji kwa hili. Lakini bado najiamini ninaposema, wachezaji wawe na malengo ya kwenda mbele.
Sidhani kama Mwana Samatta alikuwa analipwa mshahara mnono alipokuwa Simba. Alilipwa hela ya kawaida, lakini kwakuwa timu yake ilikuwa imepata nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa, hapo ndipo TP Mazembe walipomuona na kumchukua.
Leo hii sidhani kama ana shida wanazolia wachezaji wetu. Ni kosa kubwa kucheza chini ya kiwango kwa sababu ya kutolipwa mshahara.
Hebu fikiria, Simba wanapokosa nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa Afrika kwa misimu miwili, mchezaji ataonekana wapi?.
Timu kubwa inakosa ubingwa eti kwasababu wachezaji hawajitumi uwanjani.
Hainiingii akilini kama kweli wanayo malengo ya kufika mbali katika maisha yao ya soka.
Wao wanatakiwa kutimiza majukumu yao ili wafanikiwe kufuzu kucheza michuano ya kimataifa. Wakifika huko na wakaonesha soka zuri, wanaweza kuneemeka.
Nawashauri wachezaji wa Tanzania, wasiwe wepesi wa kukata tamaa kwasababu za nje ya uwanja.
Ukiingia uwanjani fanya kazi yako kwa ufanisi. Mambo ya kutolipwa mshahara au posho yasikufanye uwa `galasa`.
Fanya kazi ili uonekane na watu ufike huko ambapo hakuna kilio kama hicho.
Lini umewahi kusikia Yaya Toure, Drogba, Eto`o akilia kutolipwa mshahara.
Huko ni mbali. Nenda tu Kongo kwa Samatta na Ulimwengu. Kuna siku wamesikika wakisema hawajalipwa mshahara au posho?.
Wachezaji fanyeni kazi yenu. Kucheza chini ya kiwango mnawaumiza mashabiki wenu. Au mnafurahia kuona mashabiki wanazira au kuzimia uwanjani?. Mnapenda kuona wanapoteza maisha kwa ajili yenu?.
Fanyeni kazi yenu kwa bidii ili mtoke hapo mlipo. Mkienda kucheza soka la kulipwa mtaachana na shida hizi.
Ukiwasikia watu wachezaji wengi waliofanikiwa, hakika wametoka mbali na matatizo kama yenu ya kutolipwa posho na mishahara yalikuwepo.
Lakini kwa kuwa malengo yao yalikuwa ya mbali, hawakucheza chini ya kiwango.
Chezeni mpira ili mzifikishe mbali klabu zenu. Mkifanya hivyo mtajitangaza kimataifa.
Mchezaji yeyote aliyefikia mafanikio, aliaminiwa, akapewa nafasi, akacheza kwa kiwango cha juu, akaonekana, akachukuliwa, akaendelea kujituma na kufanya kazi kwa bidii, leo hii ni mtu muhimu katika jamii yao.
Nawatakieni kila la heri wachezaji wetu ili mfanikiwe malengo yenu.

No comments:

Post a Comment