Search This Blog

Wednesday, March 19, 2014

TFF MSIKUBALI TENA KULIPA MILIONI 15 UWANJA WA TAIFA, KUNJUENI MAKUCHA KWA WAHARIBIFU WA VITI!!


Ligi kuu soka Tanzania bara inatarajia kuendelea leo  machi 19 mwaka huu kwa mechi kali ya vuta ni kuvute kati ya mabingwa watetezi, Young Africans dhidi ya makamu bingwa Azam fc , itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni.
Shirikisho la soka Tanzania kupitia kwa Afisa habari wake, Boniface Wambura Mgoyo limesema tiketi kwa ajili ya mechi hiyo zitaanza kuuzwa saa 2 asubuhi katika magari maalumu .

Vituo vilivyotajwa ni  Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Ubungo Terminal, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Samora/Ohio, OilCom Ubungo, Buguruni Shell, Dar Live- Mbagala, kituo cha daladala Mwenge na Uwanja wa Taifa.
Wambura aliongeza kuwa  baada ya saa 6 mchana mauzo yote yatahamia Uwanja wa Taifa ambapo milango kwa ajili ya mechi itakuwa wazi kuanzia saa 7.30 mchana.
 Pia afisa habari huyo alibainisha  viingilio katika mechi hiyo kuwa ni sh. 30,000 kwa VIP A, sh. 20,000 kwa VIP B na C wakati viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani kiingilio ni sh. 7,000.

Wambura alimtaja  mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam kuwa ndiye atakayechezesha mechi hiyo, huku  akisaidiwa na Anold Bugado (Singida), Florentina Zablon (Dodoma) na Lulu Mushi (Dar es Salaam).
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa ni Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya wakati mtathimini wa waamuzi ni Alfred Rwiza wa Mwanza.
Wakati mechi hiyo ikisubiriwa kwa hamu, kuna baadhi ya mambo yanatakiwa kuangaliwa kwa jicho la tatu.

Siku za karibuni mashabiki wa klabu za Simba na Yanga wamekuwa wakifanya vurugu ndani ya uwanja wa Taifa, huku wengine waking`oa viti kuashiria kupinga baadhi ya mambo yakiwemo maamuzzi ya waamuzi.
Mashabiki wa timu hizi kubwa wamekuwa wakikosa ustaraabu na uvumilivu pale timu zao zinaposhindwa kupata matokeo.
Pia maamuzi ya waamuzi yamekuwa chanzo cha vurugu hizi ambapo mashabiki huwa wanawalaamu marefa kuvurunda.
Kuna wakati kweli waamuzi wanakosea kwa sababu za kibinadamu,  kwani hakuna aliyeumbwa mkamilifu.

Linapokuja suala la baadhi yao kufanya maamuzi nje ya sheria 17 za soka, hapo inakuwa ngumu kutafsiri kwanini inakuwa hivyo.
TFF wanatakiwa kuwakumbusha waamuzi kuwa mechi ya kesho ina uzito mkubwa mno katika harakati za ubingwa wa Tanzania bara.
Yanga wanahitaji kushinda ili kupunguza pengo la pointi baina yao na vinara Azam fc.
Mpaka sasa Yanga wao nafasi ya pili kwa pointi 39 nyuma ya Azam waliopo kileleni kwa pointi 43.

Kama Azam fc atashinda kesho inawezekana ikawa mguu ndani- nje kutafuta ubingwa wake wa kwanza tangu kuingia ligi kuu msimu wa 2008/2009.
Kwa upande wa Yanga kushinda kutawafanya warudi katika hadhi yao ya kutetea ubingwa msimu huu.
Kama watapoteza, watakuwa katika mazingira magumu kuwachomoa Azam fc waliopo kwenye reli kwasasa.

Kwa mazingira hayo, mchezo wa kesho una uzito mkubwa mno kwa wachezaji wa Yanga, Azam fc, viongozi na mabenchi ya ufundi na mashabiki kwa ujumla.
Mashabiki wa Yanga wanahitaji kuona timu yao inashinda, nao wa Azam fc wanahitaji kuona wanaendelea kutesa kileleni.
Kiuhalisia Yanga wana mashabiki wengi zaidi kuliko Azam fc, lakini kuna kundi la wapinzani linaweza kuingia uwanjani kwa kuwashangilia wana Lambalamba.
Kutokana na uzito wa mchezo huu, waamuzi wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha amani inatawala uwanjani na nje ya uwanja.

Machi 10, mwaka 2012, Israel Mujuni Nkongo alipigwa na wachezaji wa Yanga kwa sababu ya kutoridhishwa na maamuzi yake.
Nao mashabiki walifanya vurugu uwanjani kuashiria kuunga  mkono maamuzi ya wachezaji wako kumshambulia Nkongo.
Kwa haya yaliyowahi kutokeo nyuma, ndio maana waamuzi wanaaswa kulinda sheria 17 za mchezo wa soka  ili kutowaamusha mashabiki majukwaani kufanya vurugu.
Vurugu pia zimewahi kushuhudiwa katika mechi ya Coastal Union dhidi ya Yanga uwanja wa Taifa, pamoja na ile ya Simba dhidi ya Kagera Sugar.
Viti vingi viliharibiwa  na kuitia hasara serikali, hivyo kuilazimu kuchota kodi za wananchi kufanya matengenezo.

Machi mosi mwaka huu, pia sinema ya vurugu iliendelea baada ya mashabiki wanaodaiwa kuwa wa Simba kufanya vurugu dhidi ya mashabiki wa Yanga ambao walilazimika kukaa jukwaa moja wakati wa mechi ya ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya National Al Ahly ya Misri kwasababu sheria za CAF zinawataka wenyeji kukaa kushoto na wageni kulia mwa uwanja.
Kwa sheria hiyo, Yanga walitakiwa kuondoka kulia mwa uwanja wa Taifa na kwenda kushoto ambako ni ngome ya mashabiki wa  Simba siku zote. Hapo ndipo zengwe likaibuka.

Kimsingi vurugu hizi hazikuchangiwa na mpira wa uwanjani, bali ni uhasama usiokuwa na miguu wala kichwa baina ya Simba na Yanga.
Viti vingi vilinyofolewa, na machi 10 mwaka huu  Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lililaani vikali fujo na uhabirifu wa mali unaofanywa na washabiki viwanjani wakati mechi mbalimbali zikiwemo zile za kimataifa na ligi za hapa nchini.
 Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, TFF waliiomba radhi Serikali kwa uharibifu wa viti uliotokea kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga ya Tanzania na Al Ahly ya Misri .

Kwa mujibu wa TFF, uharibifu ule  wa viti ulisababisha hasara ya sh. milioni 15 kwa wamiliki wa uwanja huo ambao ni Serikali.
TFF walisema watalipa fedha hizo kwa Serikali kutokana na uharibifu huo.
Kwa mujibu wa Serikali, katika mechi hiyo, viti kumi viling’olewa na kutupwa ovyo ovyo uwanjani wakati vingine 40 viliathirika kutokana na vurugu za watazamaji hao.
Aidha, TFF walikazia zaidi kwa kusema,  kwa vile sasa baadhi ya washabiki, wapenzi na wanachama wa klabu mbalimbali nchini wanataka kufanya suala la uharibifu kuwa la kawaida na mazoea, Serikali inakusudia kuchukua mapato yote ya mchezo husika endapo kutatokea uharibifu.

Taarifa hii ya TFF ilionesha jinsi gani wameguswa na suala la uharibifu wa viti uwanja wa Taifa.
Si kwamba mashabiki wote wanafanya vurugu hizo, bali kuna kundi fulani la mashabiki wanaokosa uunngwana na kuwashawishi wenzao kufanya uovu huo.
Tayari mtihani mwingine upo kesho, kama mambo hayataangaliwa kwa umakini tunaweza kuona mambo mabaya.
Hatuombei, lakini hatuachi kutoa tahadhari kwa TFF kuwa hatua za mapema zichukuliwe kutokana na uzito wa mchezo wenyewe.
Kama mashabiki kwa asilimia zote wamejiandaa kupata ushindi na kusahau kuwa mpira wa miguu una matokeo matatu, kushinda, kufungwa na kutoa sare au suluhu, basi tunaweza kuona vurugu endapo matokeo yatakuwa tofauti na matarajio yao.
TFF wawasiliane na jeshi la polisi mapema  ili kupanga mikakati ya  kudhibiti hali ya mambo uwanjani.

Walishatangaza  kuwachukulia hatua kali mashabiki wanaofanya vurugu kwani tayari wameshaingia hasara ya milioni 15.
Pesa hizi zingetumika kufanya mambo mengine, lakini kwasababu ya upuuzi wa baadhi ya watu, zinafidia uharibifu wa viti.
Hatua kali zianzie kesho endapo kutatokea sintofahamu. Japokuwa hatuna imani kama vurugu zitatokea.
Mashabiki wa Yanga na Azam watambue kuwa soka ni mpira wa ajabu ambao hutegemea zaidi umakini uwanjani.
Ni mchezo wa nafasi, endapo ukipata nafasi na kuitumia unafaidika, lakini kama unapata nafasi na kuichezea, unajutia.

Mashabiki wafahamu kuwa kufungwa kupo na lazima ukubali matokeo.
Pia wakumbuke waamuzi ni binadamu, kama kuna makosa watafanya, viongozi wanajua taratibu za kufuata ili kupata haki.
Kupigana, kuvunja viti hakusaidii kitu zaidi ya kuilipisha klabu faini zisizokuwa na kichwa wala miguu.
TFF msikubali kulipa milioni 15 kwasababu ya wachache. Kamwe msione kama fedha hizo ni chache. Wachukulieni hatua kali watakaohusika kwa uharibifu kama mlivyotangaza.

Mshabiki nendeni uwanjani mkashangilie mpira kwa amani bila kujihusisha na utovu wa nidhamu.
Wachezaji chezeni mpira bila kutegemea maamuzi ya waamuzi. Unesheni ufundi wenu na kuwakosha watazamaji watakaofurika kesho uwanja wa Taifa.
Kila la kheri Yanga na Azam fc kuelekea ngwe muhimu ya kesho.

No comments:

Post a Comment