Search This Blog

Saturday, March 15, 2014

RAGE FIKIRIA AJENDA ZA WANACHAMA MKUTANO WA KESHO, MATATIZO YA SIMBA YATATULIWE NA WANASIMBA WENYEWE!!


Mpira ni mchezo unaogusa hisia za watu wengi zaidi Duniani. Ipo michezo mingi, lakini unapozungumzia soka unagusa mamilioni ya watu kuliko mchezo wowote unaoujua.

Wapo mashabiki wengi ambao kila muda wanajadili soka. Hata hapa Tanzania, ukipita kwenye vijiwe mbalimbali, baa, ofisi za watu na maeneo mengi ambayo watu wanakutana kupiga gumzo, hawaachi kuzungumzia kabumbu.

Nchini Tanzania, klabu za Simba na Yanga zina wapenzi wengi zaidi ya klabu yoyote. Unapotaja klabu hizi, unagusa hisia za Watanzania wengi.

Ndio maana kwenye mechi zao, ni rahisi kwa watu kuzirai au kupoteza fahamu pale matokeo mabaya yanapoikumba timu moja.
Kama inafika wakati watu wanapoteza fahamu baada ya timu zao kufungwa na wengine kuamua kujiua, utagundua kuwa timu hizi zina mvuto mkubwa kwa mashabiki wake.

Kama mtu anaweza kukumbwa na matatizo hayo ya kiafya kwasababu timu imefungwa, lazima uwe makini unapopewa dhamana ya kuogoza klabu hizi.
Kuwa kiongozi wa Simba na Yanga, kunahitaji uwe na uelewe mkubwa  wa kutambua kuwa nyuma yako kuna watu wengi wenye mapenzi ya dhati na timu zao.

Unapoleta mchezo na mambo muhimu yanayohusu klabu, unawaumiza watu bila sababu ya msingi.
Nirudi kwenye hoja yangu ya msingi iliyonisukuma kuandika makala hii.

Kesho machi 16 klabu ya Simba  itafanya mkutano wa wanachama wake kwa ajili ya kuifanyia marekebisho Katiba yao.
Kuelekea katika mkutano huo, tayari shirikisho la soka la Tanzania, TFF limewatakia kila la heri Simba katika mkutano huo ambao ni muhimu katika kuhakikisha klabu yao inapiga hatua katika maendeleo ya mpira wa miguu na ustawi wake kwa ujumla.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi katika taarifa yake jana 
aliwakumbusha viongozi na wanachama wa klabu ya Simba kuwa marekebisho hayo ni lazima yafanyike kwa kuzingatia Katiba, Kanuni na maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Afrika (CAF) na Tanzania (TFF).

Aidha taarifa yake ilisema kuwa waraka wa TFF kwa wanachama wake wa Februari 7 mwaka huu uzingatiwe kikamilifu katika marekebisho hayo.
Zaidi Malinzi aliwakumbusha wanachama wa Simba kuzingatia  umuhimu wa kudumisha amani na maelewano katika klabu yao.
Mkutano wa kesho kwa mujibu wa mwenyekiti wa Simba SC, Ismail  Aden Rage utakuwa na ajenda moja ya marekebisho ya katiba.

Lakini tayari yametokea malumbano ambapo wiki hii viongozi  wa matawi ya Simba, walipinga maamuzi ya Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kuitisha mkutano mkuu wa dharura Jumapili ukiwa na ajenda moja tu badala yake wametaka kuwe na ajenda tano.
Viongozi hao walikutana na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya habari (MAELEZO) na kumtaka Rage na kamati yake ya utendaji waongeze ajenda nyingine ili mkutano huo uwe na ajenda tano.

Walisema wanataka kujua uwanja wao  wa kisasa unajengwa lini, mauzo ya jezi, kesi zilizopo mahakamani dhidi ya Simba,  pesa za mauzo ya wachezaji wao na uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti baada ya kujiuluzu kwa Geofrey Nyange.
Mwanachama machachari wa Simba Bi. Chuma Suleiman alienda mbali na kueleza kuwa pasipo kuyafanya hayo, wanaamini kutakuwa na vurugu katika mkutano huo.

Ukifuatalia suala hili, utagundua kuwa Wanachama wana mengi moyoni mwao ambayo wanataka yajadiliwe katika mkutano huo na kujua hatima ya klabu yao.
Rage akiwa mwenyekiti anayo mamlaka kikatiba ya kupanga ajenda za mkutano mkuu wa wanachama.
Kwasababu katiba inamruhusu, basi hakuna jinsi ya kumpinga kama ameamua kuwepo kwa ajenda moja tu katika mkutano.
Katika maisha ya kawaida, kuna wakati unatakiwa kuwa makini unapofanya maamuzi. Sipingi hata kidogo kwa Rage kuwa na ajenda moja ya mabadiliko ya katiba.
Lakini ukitazama kiuhalisia, bado utagundua kuwa Simba wanayo matatizo mengi ya kujadili katika mkutano huo.
Wanachama wanazo ajenda za kuhoji kwa viongozi wao. Wanataka kujua mambo mengi, hivyo wanaamini mkutano huo ndio wenye nguvu kufanya maamuzi.

Nadhani ipo haja kwa kamati ya utendaji chini ya Rage kufikiria upya na kuyaingiza maombi ya wanachama wake.
Mwanzoni mwa makala hii nilisema, kuongoza Simba au Yanga unagusa hisia za watu wengi, hivyo lazima uwe msikivu.
Rage inabidi akae chini na kutathimini, kama atagundua wayatakayo wanachama ni kwa ajili ya faida ya timu,  basi ayaweke katika mkutano huo. Lakini kama anaona hayana maana kujadiliwa kwasasa basi aendelee na ajenda moja tu.

Wanachama ndio waliomuweka madarakani. Wao ndio wenye klabu, wanapohitaji jambo fulani lijadiliwe basi wafikiriwe.
Siandiki haya kwa kujaribu kumshinikiza Rage aongeza ajenda, lakini najaribu kuwaza endapo kutatokeoa vurugu kwenye mkutanao huo kwasababu tu ajenda za wanachama zimekataliwa kujadiliwa, nani atabeba msalaba wa lawama?.

Bado nasisitiza jambo hili, kuongoza Simba na Yanga unagusa maisha ya watanzania wengi. Hakuna tatizo lisilokuwa na chanzo.
Hata kufanya vibaya kwa timu kunachangiwa na viongozi. Jaribu kuwaza mfumo unaotumika kusajili wachezaji kama unaridhisha katika klabu hizi kubwa.
Watu wachache wanakaa chini na kutafuta wachezaji, na wakati mwingine wanasahau hata kupitia ripoti za mabenchi ya ufundi.
Kupigana vikumbo kwa viongozi, kunyang`anyana wachezaji ndio tabia yao. Lakini wanapogundua kuwa walisajili vibaya na benchi la ufundi limeshindwa kuwapa makali `magalasa` wao, basi makocha wanabebeshwa mzigo wa lawama.
Mwisho wa siku timu inacheza vibaya na kuwajeruhi mashabiki moyoni. Watu wanazirai uwanjani kwasababu ya makosa yaliyofanywa na watu fulani.

Hakika baadhi ya viongozi hawawezi kukwepa lawama kwa haya, ifike wakati wawe na moyo wa huruma kwa mashabiki wao. Wachezaji hawalipwi mishahara na posho kwa wakati. Unategemea wacheze mpira gani kama wana njaa. Lakini kuna watu wanaohusika na kukwepa majukumu yao.
Nawaasa viongozi wa Simba wawape nafasi wanachama wao kujadili mambo ya klabu. Nafahamu kuwa uhuru wa kutoa mawazo hauzuiliwi hata kikatiba. Katiba inatoa nafasi kwa kila mtu kutoa mawazo yake.
Wape watu nafasi ya kuzungumza, pima uzito wa hoja zao, chukua mazuri achana na pumba.

Kikubwa kwa Rage ni kutumia busara ya utu uzima ili kuepuka mgogoro usiokuwa wa lazima.
Katika utawala wa kidemokrasia, watu wana nafasi kubwa ya kujadili mambo yao, usijaribu kuwanyima fursa.
Migorogoro haina tija kwa klabu. Watu wamechoka kusikia migogoro. Wachezaji wanaathiriwa nayo hata kama si moja kwa moja.

Viongozi mnapolumbana na wanachama kwa masuala fulani, mnatoa mwanya kwa wapinzani wenu kuwapiga bao.
Kila la heri wana Simba katika mkutanao wenu hapo kesho. Tafuteni mwarobaini wa matatizo yenu.

Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976

No comments:

Post a Comment