Search This Blog

Wednesday, March 12, 2014

PHILLIP COCU- KIUNGO FUNDI WA UHOLANZI ALIYEGEUKIA UKOCHADunia na wapenzi wa soka kiujumla wamepata fursa ya kuona na kushuhudia vipaji na ufundi mbalimbali unaoonyeshwa au uliowahi kuonyeshwa na wanasoka mbalimbali ulimwenguni kiasi ambacho baadhi ya majina ya wanasoka ambao wameamua kutundika daruga la kusakata mchezo huo wa kabumbu ulimwenguni yakiendelea kukaa vichwani na kutajwa midomoni mwa wapenzi na mashabiki wa soka ulimwenguni.
Miongoni mwa wachezaji ambao licha ya kuamua kupumzika na mikikimikiki ya mchezo wa soka bado wamebakia kuwepo katika ubongo wa wapenzi wa soka ulimwenguni ni kiungo fundi wa ushambuliaji wa vilabu vya Barcelona na PSV Eindhoven, Phillip John William Cocu ambaye dunia ilimtambua kwa kifupi cha jina lake Phillip Cocu.

KIPAJI TOKA EINDHOVEN

Phillip Cocu alizaliwa mnamo tarehe 29,Oktoba 1970 katika kitongoji cha Zevenaar kilichopo katika jii lenye wanazi sugu wa soka la Eindhoven. Ikumbukwe kwamba jiji la Eindhoven ndipo inapotoka timu iliyoweza kutikisa nchini Uholanzi na Ulaya kwa ujumla mwishoni mwa miaka ya tisini na mwanzoni mwa miaka ya elfu mbili ya PSV Eindhoven.
Kama ilivyo ada kwa watoto wengi wanaozaliwa wakiwa na vipaji vya soka, Cocu alijiunga na timu ya watoto ya mtaani kwao ya DCS  kabla ya baadae kujiunga na timu nyingine iliyopo katika mtaa huo ya De Graafschap ambayo aliichezea mpaka mwaka 1988 ambapo alijiunga rasmi na soka la kulipwa katika timu ya AZ Alkmaar ambayo aliichezea kwa muda wa miaka miwili tu ambapo baadaye alijiunga na klabu ya Vitesse .
Akiwa Vitesse, Cocu alipata majeruhi mwanzoni tu mara baada ya kujiunga na klabu hiyo jambo lililopelekea kutishia kipaji chake lakini alifanikiwa kupigana na majeruhi hayo ya goti ambayo na kurudi uwanjani kwa kishindo na kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

AJIUNGA  NA KLABU YA NDOTO ZAKE

Baada ya kuichezea timu ya Vitesse kwa muda wa miaka mitano katika michezo 137 na kufanikiwa kuifungia timu hiyo jumla ya magoli 25, Cocu alisajiliwa rasmi na klabu maarufu ya PSV Eindhoven ambayo inatoka katika jiji alilozaliwa la Eindhoven mnamo mwaka 1995.
Cocu aliuelezea uhamisho huo kuwa ni ukamilisho wa ndoto zake za muda mrefu za utotoni huku akiishukuru klabu ya Vitesse na mashabiki wake kwa kumsapoti katika matukio shida na furaha aliyowahi kukutana nayo ikiwemo majeruhi ya muda mrefu aliyopata pindi alipojiunga na timu hiyo huku wakimchukulia kama miongoni mwa mashujaa wao klabuni hapo.

APIGA SOKA LA UHAKIKA PSV, ATUA BARCELONA

Mara baada ya kujiunga na klabu ya PSV Eindhoven, Cocu alifanikiwa kupata alifanikiwa kujitengenezea namba ya kudumu katika timu hiyo akicheza katika nafasi ya kiungo mshambuliaji nafasi ambayo alikuwa akiimudu vilivyo na kufanikiwa kutwaa mataji mawili maarufu nchini humo ya KNVB na lile la ligi kuu nchini humo lijulikanalo kwa jina la Eredivisie mnamo mwaka 1997.
Akiwa hapo, Cocu alifanikiwa kucheza jumla ya mechi 95 huku akifanikiwa kuifungia timu hiyo jumla ya magoli 31 katika mechi hizo alizocheza.
Kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusakata kabumbu, vilabu mbalimbali barani Ulaya vilianza kuinyemelea saini yake lakini ilikuwa ni klabu ya Bercelona iliyofanikiwa kuinasa saini yake mnamo mwaka 1998.

ATESA BARCELONA , APEWA UNAHODHA

Cocu katika misimu yote aliyoichezea klabu hiyo ya Hispania inayotokea katika kitongoji cha Catalan, alifanikiwa kuteka nyoyo za wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kucheza soka jambo ambalo lilipelekea Mdachi huyo kupewa unahodha klabuni hapo, huku akifanikiwa kuisaidia timu hiyo kutwaa taji la nchi hiyo maarufu kama La Liga, huku Barcelona ikifanikiwa kucheza katika nusu fainali mbili za mashindano makubwa na maarufu ya vilabu barani Ulaya yajulikanayo kama Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pia akiwa Barcelona, Cocu alifanikiwa kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kuweza kuichezea mechi nyingi timu ya Barcelona, ambapo aliichezea timu hiyo jumla ya mechi 205 huku akifunga jumla ya magoli 31

AAMUA KURUDI NYUMBANI

Baada ya miaka  sita ya mafanikio ndani ya Barcelona, Phillip Cocu aliamua kurudi katika klabu aliyoipenda ya PSV Eindhoven ambako aliweza kuisaidia timu hiyo kushinda jumla ya mataji matatu ya ligi kuu nchini humo huku pia akiisaidia timu hiyo kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, huku ikiwa ni nusu fainali yake ya tatu katika mashindano hayo.
Inasemekana, Cocu aliamua kurudi zake nyumbani Uholanzi ikiwa ni kama njia ya kumpisha nyota wa Kihispania aliyekua anachipikia klabuni hapo ambaye baadae ametokea kuwa staa na nahodha wa tim hiyo, na huyu si mwingine bali ni Xavi Hernandez.

AMALIZIA SOKA UARABUNI,ANG’ARA TIMU YA TAIFA

Mara baada ya awamu ya pili ya mafanikio ndani ya klabu ya PSV,Cocu aliamua kutimkia zake Uarabuni ambako alikwenda kumalizia soka lake katika klabu ya Al Jazira.
Kutokana na soka lake la uhakika alilolionyesha katika timu mbalimbali, Cocu alifanikiwa kujiwekea nafasi ya kudumu katika timu ya Taifa ya Uholanzi ambayo aliichezea jumla ya mechi 101 na kuifungia jumla ya magoli 10.
Miongoni mwa matukio ya kusisimua ya Phillip Cocu akiwa na timu ya Taifa ya Uholanzi, ni kuifungia timu hiyo magoli mawili katika Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Ufaransa mwaka 1998 lakini baadae akaja kukosa penati muhimu dhidi ya Brazil katika mchezo wa nusu fainali ambapo Uholanzi iliondolewa kwa mikwaju ya penati na miamba hiyo ya soka ulimwenguni.

AGEUKIA UKOCHA

Mara baada ya kuamua kutundika daluga la kucheza soka, kama ilivyo kawaida ya wanasoka wengi waliostaafu kucheza soka, Cocu aliamua kujikita katika ukocha wa mchezo huo wenye mashabiki wengi ulimwenguni ambapo hivi sasa anainoa klabu anyoihusudu ya PSV Eindhoven ambayo ameiwezesha kufika katika hatuanya mtoano ambayo walitolew na timu ya AC Milan hivi karibuni, huku wakipata nafasi ya kushiriki katika mashindano ya Europa League.


Imeandaliwa:
CHARLES ABEL-SAUT
0713 923276
Email: charlesabel46@yahoo.com

                                                                                              

No comments:

Post a Comment