Search This Blog

Tuesday, March 18, 2014

NIONAVYO MIMI:PEP GAUDIOLA ANAKUWA NA AKILI ZA KITOTO.

Na Oscar oscar Jr.
0789-784858
Kuna muda huwa nikimkuta mtoto ameshika rimoti ya Runinga,huwa sipendi kukaa sebuleni siku hiyo na sababu yangu kubwa ni moja tu.sipendi kuhangaisha macho yangu.Kila mtoto anavyobonyeza rimoti,ndivyo anavyokamilisha furaha yake.Dakika moja akiweka chaneli inayoonyesha taarifa ya habari,sekunde kadhaa zinazofuata,utamuona kaweka chaneli ya katuni na baadae,atakupeleka kwenye picha la kivita au mieleka.Kadri unavyozidi kukolea kwenye chaneli moja,ndivyo na yeye anavyoongeza manjonjo kwenye kuzibadilisha!

Sioni tofauti ya akili hizi za kitoto na anachofanya kocha wa sasa wa klabu ya Bayern Munich,Pep Gaudiola.Ndiyo,Pep Gaudiola ana akili za kitoto.Wakati ukifurahia kumuona Philip Lahm akifanya vema kama beki wa kulia,yeye anamtumia kama kiungo mkabaji na timu inashinda.wakati dunia ikimkubali kwa sasa Javi Martinez kama moja ya viungo bora,yeye anamtumia kama beki wa kati na timu inapata pointi 3.Unadhani Pep Gaudiola anatofauti gani na mtoto aliyeshika rimoti?

Kuna siku Pep Gaudiola atampanga golikipa wake Manuel Neuer kama mshambuliaji huku Mario Mandzukic akianza golini na sintoshangaa kuona mechi hiyo wanashinda.Unajua kwa nini? Bayern Munich ni timu iliyokamilika kwa sasa,hawakamatiki.Wanapokuwa wanamiliki mpira,timu yote inashambulia na pindi wanapopoteza,wote wanarudi kukaba na kuusaka mpira ulipo.Unataka nini zaidi? Bayern walimuuza kiungo Luiz Gustavo na mshambuliaji wao Mario Gomes,kuna mtu anajali?

Msimu wa 2008/2009 Pep Gaudiola alipewa rasmi mikoba ya kuwa kocha mkuu wa klabu ya Barcelona toka kwa aliyekuwa kocha wa kipindi hicho,Frank Rijkaard na katika msimu wake wa kwanza,Pep Gaudiola alishinda mataji matatu ambayo ni Kombe la Mfalme,La Liga na klabu bingwa Ulaya ambapo aliweza kuandika historia ya kuwa kocha wa kwanza mwenye umri mdogo kuwahi kutwaa kombe hilo la Ulaya.Na kwa ufupi tu,Gaudiola ni moja ya makocha bora duniani huku mwaka 2011 akiibuka mshindi wa Balon D'or na kutangazwa kocha bora wa Dunia.

Baada ya kuachana na klabu ya Barcelona,alijipa muda wa mwaka mmoja kupumzika huko nchini Marekani.Msimu huu amerejea kwenye kazi yake na sasa ni kocha wa mabingwa wa ulaya Bayern Munich.Alianza msimu vibaya huku akipoteza kombe la ufunguzi (German Super Cup)dhidi ya wapinzani wao klabu ya Borussia Dortmund lakini,baadae alifanikiwa kuwatuliza watu kwa kunyakuwa kombe la European Super Cup kwenye mchezo dhidi ya Chelsea na baadae,akatwaa kombe la dunia kwa vilabu kwenye ardhi ya Afrika kule Morocco.

Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria na mchambuzi wa soka Sunday Oliseh,kwenye moja ya makala zake ambayo iliipa jina la "Why Bayern is best" anasema,moja ya sababu za kuifanya Bayern kuwa timu bora ni pamoja na kutoruhusu wachezaji wake inaowategemea kuondoka katika klabu hiyo huku,ikitengeneza mazingira mazuri ya kumshawishi mchezaji yoyote yule bora duniani kujiunga na wababe hao wa Ulaya.

Kwa nyakati tofauti,Bastian Schweinstiger,Arjen Roben,Frank Ribery na Philip Lahm wamewahi kutakiwa na baadhi ya vilabu vikubwa barani Ulaya lakini,Bayern wameendelea kuwashikilia wachezaji hao kwa kuwapatia kila wanachokitaka.Pamoja na kikosi hicho kutikisa dunia msimu uliopita,bado waliingia sokoni na kumnunua kiungo mshambuliaji Mario Gotze kutoka Borussia Dortmund na Thiago Alcantara kutoka klabu ya Barcelona na kwa taarifa zilizopo ni kwamba,mshambuliaji Robert Lewandowski kutoka klabu ya Borussia Dortmund na Julian Draxler kutoka Schalke 04 huenda watajiunga na wababe hao wa Ulaya mapema msimu ujao.

Takwimu zinaonyesha kuwa,klabu ya Bayern Munich inawastani wa mashabiki 71,000 ambao wanahudhuruia kila mechi ya bundesliga ambayo Bayern wanacheza katika uwanja wao wa nyumbani msimu huu.Kutokana na mashabiki wao kuwaunga mkono,ndiyo maana jamaa waliamua kuacha kabisa kuitumia jezi yao namba 12 kwa mchezaji yoyote yule huku wakiamini,inavaliwa na utitiri wa mashabiki wao.

Kuiongoza timu ambayo imetoka kutwaa mataji makubwa matatu kwenye msimu uliopita chini ya kocha bora wa dunia kwa sasa,Juup Heynches,sio kazi ndogo.Heynches alifanikiwa kutwaa kombe la Ligi,Bundesliga na lile la klabu bingwa Ulaya msimu uliopita lakini,Pep Gaudiola anaendelea kuithibitishia dunia kwamba alikuwa mtu sahihi wa kuchukuwa mikoba ya kuinoa timu hiyo ya Ujerumani huku akiwa hajapoteza mchezo wowote wa Bundesliga msimu huu.

Mkongwe wa Bayern Munich,Ruud Gullit amesema "Hata kama wewe ni adui namba moja wa klabu ya Bayern ni wazi kwamba kwa sasa utakubali kwamba hawakamatiki" wakiwa chini ya kocha Gaudiola,wanawastani wa asilimia 68 katika kumiliki mpira huku wakiwa wanafunga magoli mengi sana.kabla ya kucheza na arsenal mechi za ligi ya mabingwa Ulaya,walikutana na klabu za Vfl Wolfsburg,Schalke 04 na Hannover 96 kwenye muendelezo wa michezo ya bundesliga na katika michezo hiyo mitatu,Bayern wameshinda yote huku wakifunga magoli 15 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 2 tu.

Baada ya mechi yao na Vfl Wolfsburg kumalizika kwa Bayern kuibuka na ushindi wa bao 6-1,Pep Gaudiola alionyesha kutoridhika na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake.Sikumuelewa alikuwa anamaana gani lakini,baadae nikagundua kuwa,huyu jamaa aliwahi kumfanya Sir Alex Ferguson atetemeke vidole kwenye fainali ya klabu bingwa pale kwenye dimba la Wembley,nadhani kwa sasa,anatamani kuona makocha wenzie wakiomba kwenda "kuchimba dawa" kabla ya dakika 90 za mchezo kumalizika ndiyo roho yake itaridhika!

Pep Gaudiola ndiye aliyeshika rimoti kwa sasa,kuna muda anatuonyesha picha za kivita na kuna muda,anatuwekea picha za katuni tuangalie.Unadhani nitasema nini sasa? Sehemu pekee inayoonekana ina mapungufu kwa mchezaji mmoja mmoja,ni beki ya kati anapocheza Jerome Boateng na Dante,lakini unawezaje kuwafikia hawa jamaa wakati mbele yao kuna "wanajeshi" Bastian Schweinstiger na Javi Martinez? inabidi tu ukubali kuangalia chaneli anayokuchagulia Pep Gaudiola maana ukileta ubishi,anaweza kumuanzisha Thiago Alcantara na Toni Kroos,ikawa ni balaa lingine!

Kwa mara ya kwanza Bayern wameweza kukusanya alama 68 katika mechi 24 tu za bundesliga,na kuna uwezekano kabla ya kuumaliza mwezi machi,watoto wa Gaudiola wakawa washatangazwa mabingwa wapya wa Bundesliga.Bado unaswali kwa Pep Gaudiola? kwa namna anavyowatesa wapinzani,kuna siku mchezaji ataomba ruhusa kwa mwamuzi ili "akachimbe dawa" kabla ya muda wa mapumziko!

ukirejea mechi zake mbili dhidi ya Arsenal za klabu bingwa Ulaya,utagundua kuwa,yeye ndiye alikuwa ameshika rimoti huku kocha wa Arsenal,Arsene wenger akiwa kwenye kochi akitazama chaneli anazowekewa na Pep Gaudiola.Kwani hili linaubishi? hapana,kila kitu kinajieleza uwanjani.

kwenye mechi ya Emirates,Gaudiola alianza kwa kuweka chaneli ya katuni na arsenal wakapata penati,walipokosa tu,akaweka picha la kivita na mpaka dakika 90 zinamalizika,Arsenal 0-2 Bayern.Mechi ya pili pale Allianz Arena,Gaudiola alifungulia picha la "wanamitindo" burudani kwa kwenda mbele na mwisho wa siku,bayern walipiga pasi 791 huku arsenal wakifikisha pasi 497 na mchezo ulimalizika kwa kufungana bao 1-1 bila kutuonyesha picha la kivita!

Pep Gaudiola alifanikiwa kushinda mataji 14 ndani ya miaka minne alipokuwa anaiongoza Barcelona kwa aina hii hii ya kuwabadilishia wenzie picha za kutazama.Kadri anavyozidi kukaa na timu,ndivyo inavyozidi kuwa tishio na ndivyo anavyozidi kubadilisha chaneli kama mtoto.Rais wa Bayern Munich amefungwa wiki hii miaka mitatu na nusu jela na pengine hali hii inaweza kuiathiri Bayern lakini,bado ninauhakika kwamba rimoti ya runinga iko mikononi mwa kocha Pep Gaudiola.

No comments:

Post a Comment