Search This Blog

Monday, March 31, 2014

MECHI YA AZAM, SIMBA YAINGIZA MIL 26/-


Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Azam na Simba iliyochezwa jana (Machi 30 mwaka huu) Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam imeingiza sh. 26,455,000.

 

Watazamaji 4,741 walikata tiketi kushuhudia pambano hilo ambapo Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-1. Viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

 

Mgawanyo kwa mapato ulikuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 4,035,508.47, gharama za kuchapa tiketi sh. 3,908,686 wakati kila klabu ilipata sh. 5,460,687.63.

 

Uwanja sh. 2,776,620.83, gharama za mechi sh. 1,665,972.50, Bodi ya Ligi sh. 1,665,972.50, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 832,986.25 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 647,878.19.

 

 

WANACHAMA TFF KUANDALIWA KATIBA MFANO YA MAREKBISHO

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekutana Machi 30 mwaka huu kujadili utekelezaji wa maagizo ya TFF kwa wanachama wake kurekebisha Katiba zao ili ziendane na Katiba ya TFF pamoja na ile ya FIFA kabla ya Machi 30 mwaka huu.

 

Vyama vya mikoa Lindi na Dar es Salaam na Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) viliomba kuongezewa muda wakati vingine vimeomba Katiba mama kama angalizo lao la mabadiliko hayo. Klabu ya Simba Sports ndiye mwanachama pekee aliyewasilisha mabadiliko ya Katiba.  TFF inawapongeza viongozi na wanachama wa klabu hiyo kwa kufanya mkutano wao kwa utulivu.

 

Kamati itatangaza nyongeza ya muda wa kufanya mabadiliko hayo baada ya kuviandalia vyama vya mikoa na vyama shiriki katiba mfano kwa ajili ya kurahisisha shughuli hiyo.

 

Baada ya kupitia uamuzi wa wanachama  wa Simba S.C. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeamua ifuatavyo:

 

(i)           Kwa kuwa pendekezo la wanachama wa Simba kubadili kipengele na 26 kuhusu sifa za mgombea kinapingana na kipengele na 29 (4)  cha Katiba ya TFF, hivyo basi Kamati imeagiza kipengele cha Katiba ya Simba kibaki vilevile bila kubadilishwa.

 

(ii)         Vipengele vingine vyote vimepitishwa na vitapelekwa kwa Msajili wa Klabu na  Vyama vya Michezo kwa ajili ya kusajiliwa.

 

(iii)       Mchakato wa uchaguzi wa Klabu ya Simba uendelee kama ulivyopangwa wakizingatia uamuzi huu wa Kamati.  TFF inaitakia Klabu ya Simba uchaguzi mwema.

 

Pia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeshauri TFF kuwasiliana na FIFA kupata mwongozo kuhusu katazo la watu wenye rekodi ya kifungo kugombea.

 

TFF imepokea ushauri huo na itaufanyia kazi na kama kuna mabadiliko yoyote kiutaratibu yataanzia katika Katiba ya TFF kupitia Mkutano Mkuu.

 

RAMBIRAMBI MSIBA WA DK HEMED MZIRAY

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha daktari wa tiba ya michezo, Dk. Hemed Mziray kilichotokea juzi jijini Dar es Salaam.

 

Dk. Mziray ambaye alikuwa mfanyakazi wa Hospitali ya Manispaa ya Temeke na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) amesafirishwa kwenda kwao mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.

 

Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Dk. Mziray ameshirikiana na TFF na wadau wengine wa mpira wa miguu katika masuala ya tiba na uongozi.

 

Alikuwa kiungo kati ya Uwanja wa Taifa ambapo mechi za kimataifa, za ligi na za kirafiki zimekuwa zikichezwa na Hospitali ya Temeke kwa wagonjwa wanaohitaji huduma zaidi, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

 

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Dk. Mziray, TASMA na wafanyakazi wa Hospitali ya Temeke na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Pia TFF inatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

 

Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina

 

BONIFACE WAMBURA

OFISA HABARI NA MAWASILIANO

SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

  

 

1 comment:

  1. TFF wamekosea kukataa marekebisho ya katiba ya Simba sc hasa kipengele cha sifa za wagombea uongozi.TFF ilipaswa kuwa mfano kwa kutowajumuisha watu wasio na sifa kwenye uongozi.Ni TFF hiyo hiyo imemteua Hanspope kuwa mjumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji huku ikijua kwamba Hanspope alishawahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai na kufungwa gerezani .Sina hakika kama unaweza kukosa sifa za kugombea uongozi na papo hapo ukawa na sifa za kuteuliwa kwenye nafasi za uongozi.Hata kama Simba wamemteua Hanspope kwenye Kamati yao ya UtendajiTFF ilipaswa kuwa mfano wa utekelezaji wa dhamira(spirit) ya Katiba,lakini badala yake imeendelea kuvunja katiba.Hata Madega hakupaswa kupewa uongozi TFF kwa kurejea makosa aliyoyafanya akiwa mwenyekiti wa Yanga kwa kukataa kupeleka timu uwanjani katika mechi ya mashindano ya kagame dhidi ya simba mwaka 2008

    ReplyDelete