Search This Blog

Tuesday, March 18, 2014

MAONI: SIMBA, YANGA, AZAM, USAJILI ZAIDI YA MILIONI 200 KWA MSIMU, KWANINI MTUHUMIWE KUTAFUTA MATOKEO NJE YA UWANJA?


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam

MPIRA wa miguu ni mchezo unaochezwa hadharani. Mipango ya timu uwanjani, umakini wa wachezaji kutumia nafasi na juhudi za timu, bila kusahau mchezaji mmoja mmoja huamua matokeoa kirahisi.
Kuna mchezo mchafu unaotajwa kuchezwa na viongozi wa timu, waamuzi na makocha wa timu zinazoshiriki ligi kuu.
Si rahisi kufahamu mambo haya kwasababu hufanywa kwa mtandao mkubwa na kwa siri kubwa.
Kibaya zaidi wapo viongozi wanaoendesha mpira na hutuhumiwa kushiriki katika njama za kutafuta matokeo nje ya uwanja.
Ni kawaida kuona kiongozi wa mpira kitaifa ana unazi na timu fulani, hivyo anajihusisha na mchezo mchafu.
Kila zinapokuja mechi muhimu zaidi, tabia ya mashushu kuzingira miji ambayo mechi zitachezwa husikika.
Mara nyingi utasikia kuna jopo la watu limetumwa kutoa rushwa kwa wachezaji wa timu pinzani ili kupata matokeo kirahisi.
Pia wachezaji wengine wanatuhumiwa kuuza mechi ili kujipatia fedha isiyohalali, huku wakisahau kuwa wanawaumiza mashabiki wao.
Wachezaji wanafahamu wazi kuwa kuna watu nyuma yao ambao hupoteza pesa zao, muda wao kwa kuwafuata popote walipo kuwashangilia.
Unadhani mtu anayetoka Tunduma-Mbeya Mpaka Dar es salaam, au kaitaba mjini Bukoba anafaidika na nini?.
Huyu mtu anatumia pesa zake ambazo hazirudishwi na mchezaji wala kiongozi wa timu, bali inakuwa hasara kwake.
Anafika kukushangilia, halafu kwa tamaa zako unachukua `vijisenti` na kucheza hovyo.
Ukiwa mwanandinga unafurahia kuona kuzirai au kazimia kwa mashabiki uwanjani?. Unafaidika nini sasa?.
Najua huwezi kuwalipa mashabiki wako kwa kukushangilia. Fadhila pekee ya kuwarudishia ni kuucheza mpira kwa kiwango cha juu na kuwafurahisha.
Huu mchezo wa kupanga matokeo na kuhonga timu pinzani unatajwa sana na bila shaka upo na wanaohusika wapo.
Nao waamuzi wameshaingia katika sakata hili. Ni kawaidia kumuona mwamuzi akivurunda kwa makusudi kabisa.
Yapo makosa ya kibinadamu, lakini kuna wakati mwamuzi anazidisha , na kwa bahati mbaya hatuna mfumo mzuri wa kupitia maamuzi baada ya mechi.
Wenzetu huwa wanarekodi mechi, baada ya hapo jopo la waamuzi hukutana na kuitazama, makosa yote hubainishwa na mwamuzi husika huulizwa.
Je, ulikuwa sahihi kutoa adhabu kwa makosa haya?. Mwenyewe utamsikia akisema ile haikuwa kadi kabisa, hivyo wanao uwezo wa kufuta maamuzi na kumchukulia hatua kama alifanya yale kwa makusudi.
Kwetu hapa hatujafikia hatua hiyo zaidi ya kusubiria ripoti ya makamisaa wa mechi ambao pia hutajwa kuhusika katika rushwa.
Nakumbuka wakati Simba sc wakijiandaa kukabiliana na Mbeya City uwanja wa Sokoine, viongozi wa Mbeya City walisikika wakisema kuna mashushu wa Simba wametumwa Mbeya.
Katibu mkuu wa klabu hiyo, Emmanuel Kimbe alihojiwa na mtandao huu na kueleza kuwa kuna vikao vilikuwa vikifanyika na mashushu hao kuihujumu klabu ya Mbeya City.
Haiku rahisi kuthibitisha habari hizi, kwani Simba kupitia kwa Afisa habari wake, Asha Muhaji walikanusha vikali taarifa hizo na kudai Mbeya City ni timu ndogo ambayo haiwezi kuwahangaisha nje ya uwanja.
Sinema ikaishia hapo.  Hata mchezo wa Yanga na Mbeya City, mzunguko wa kwanza jijini Mbeya, kuna watu walikamatwa katika kambi ya Mbeya City, chuo kikuu cha Mzumbe Tawi la Mbeya wakitajwa kuwa ni mashushu wa Yanga.
Watu hao walidhibitiwa na mashabiki wa Mbeya City na kunusurika kupigwa baada ya watu wenye busara kuwaombea msamaha.
Watu hao walitajwa kuhusika na njama za kuwahonga wachezaji wa Mbeya City ili wasiwabanie Yanga.
Kwa upande wa Yanga walikanusha taarifa hizo na kusema hawahusiki na hilo.
Si rahisi kwa mtu kukubali kuwa anahusika na masuala haya, labda imtie mbaroni na kumuweka hadharani.
Najua wapo watu wenye kazi hiyo ili kuzisaidia timu zao kupata matokeo nje ya uwanja.
Mbaya zaidi mambo haya hutokea kwenye michezo muhimu inayohusisha klabu kubwa za Tanzania, Simba, Yanga na sasa Azam fc.
Siwezi kusema kuwa kweli wanafanya haya, lakini kiuhalisia kuna mambo yanatendeka na huweza kukusukuma ukaamini kirahisi kuwa kuna mchezo mchafu unafanywa.
Inaeleweka wazi kuwa kwasasa timu za juu, Azam fc, Yanga, Mbeya City na Simba kwa mbali zipo katika mbio za kuwania ubingwa.
Ligi inaelekea ukingoni, hivyo kila mchezo umekuwa muhimu zaidi kwa timu za juu.
Yanga wanacheza na Azam fc keshokutwa uwanja wa Taifa. Matokeo ya ushindi kwa timu zote yanahitajika sana.
Wikiendi, Mbeya City watakuwa wanacheza na JKT Ruvu uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Mchezo huu hauna mvuto kutokana na mpinzani wa Mbeya City.
Lakini utakuwa mgumu zaidi kwani wagonga nyundo wa Mbeya watakuwa wanahitaji ushindi ili kusonga mbele katika msimamo.
Msemo wa adui muombee njaa, sasa ndio mahala pake. Mbeya City wanawaombea mabaya Azam fc na Yanga.
Mtandao huu umefanya mahojiano marefu na msemaji wa Mbeya City, Freddy Jackson.
Katiki mahojiano hayo, Freddy alisema kikosi chao kinaendela vizuri, huku akisisitiza kuwa wachezaji wao wawili walioumia mchezo uliopita dhidi ya Rhino Rangers, Mwagane Yeya na Richard Peter wanaendelea vizuri.
Suala la kuendelea vizuri kwa kambi haikuwa `ishu` kubwa, lakini kuna kauli alitamka ambayo imenivutia kuandika makala hii.
Namnukuu; “unajua bwana, sasa kila timu inahitaji pointi. Sisi tunapambana na Yanga, Azam fc kutafuta ubingwa. Mechi yetu na JKT Ruvu tutacheza zaidi ya timu moja”.
“Tutatumia uwanja wa Azam, huo ni uwanja wa wapinzani wetu na huwezi jua wamejipangaje. Kuna michezo michafu inafanywa kwa timu za juu. Tumejiandaa kwa yote na tunafahamu kuwa hujuma zipo sana ili kutushusha”. Alisema Freddy.
Ukiyapima maneno yake unagundua kabisa, Mbeya City wanahofia mchezo mchafu wa timu za juu.
Inaonekana kuna mambo wanayafahamu kabisa ndio maana wanajiandaa kupambana na hujuma hizo.
Nilisema mapema kuwa kucheza mpira nje ya uwanja ni habari za uhakika. Wapo viongozi wanaohusika na si rahisi kuwafahamu.
Hoja ya msingi ni kuwa, endapo wanawekeza katika timu zao kwa kusajili wachezaji wakubwa, kuna maana gani ya kutafuta matokeo ya nje ya uwanja.
Waswahili husema, lisemwalo lipo, na kama halipo basi linakuja. Masuala ya rushwa michezoni yapo sana.
Hata kwa wenzetu tunasikia na kuona watu wanapewa adhabu kwa kupanga matokeo.
Kwa mfano, Yanga na Simba zinatumia zaidi ya shilingi milioni 250 kusajili wachezaji kwa msimu mmoja. Kwa pesa hii kuwa bingwa si ajabu.
Unawezaje kutumia pesa nyingi kiasi hiki na usiwe bingwa?. Maana ya hapa ni kuwa lazima utakuwa na wachezaji wazuri.
Azam fc wamewekeza mno, kwasababu hiyo wanastahili kuwa mabingwa kwasababu wanatumia pesa nyingi kutengeneza timu yao.
Linapokuja suala la kuhangaika nje ya uwanja, naona hakuna maana ya kumwaga fedha nyingi kiasi hicho, halafu unataka udhindi kwa mlango wa nyuma.
Kama haya yanayolalamikiwa na baadhi ya klabu yanasababishwa na mchezo mchafu wa timu kubwa, basi ipo haja ya viongozi wa soka kulitazama kwa umakini.
Timu zinakuwa zinaishia kupata ubingwa wa Tanzania, lakini zikifika kwa wenzetu ambao hawahongeki kirahisi na wanawekeza nguvu zao uwanjani, basi kipigo kitabaki palepale.
Rushwa humaliza soka letu, lazima ipingwe kwa nguvu zote.
Naomba kuwasilisha…………

2 comments:

  1. Hakika makala ni ndefu.na nzuri imejaa mifano mizuri ila ni ya upande mmoja na ya kufikirika zaidi lkn inavutia.kwangu mimi naona mwandishi anaungana na viongozi wa mbeya city wanaolalamika mechi zao kuingiliwa bila kufafanua maana kuna kuingiliwa kwa kuhonga waamuzi.au kuhongwa wachezaji au timu pinzani kuandaliwa kwa kuahidiwa mshiko endapi watashinda (kitu ambacho si dhambi) ikumbukwe pia mbeya city kama ni timu ya mfano ktk makala hii nao pia walilalamikiwa saana kwa vitendo vyao wakiwa mbeya ktk kulazimisha ushindi mwanzoni mwa league.vilevile hata yanga mwanzoni mwa ligi ililalamika saana juu ya uchezeshaji mbovu lkn iliishia kubezwa hata simba mwishoni mwa round ya kwanza nayo ililslamikia waamuzi nayo ikabezwa azam wananafuu kidogo nadhani sababu mechi nyingi zinachezwa ktk uwanja wao.ila tu maandalizi ya mechi mwanzo wa msimu mpaka mwisho wa msimu hutoa matokeo bora.vinginevyo barcelona.real madrid.mancity psg.juventus.yanga.chelsea.azam.na timu zooooote zenye kufanya maandalizi mwanzo mwisho zitapewa jina la wanunua mechi na zile timu ambazo maanalizi yao ni zimamoto na pale zinapooona hazishuki daraja wala hazipati nafasi tatu za juu maandalizi yao huwa ni sawa na kuvunja kambi hivyo kuonekana kuwa wamenunuliwa ni rahisi wakati ukweli hawans morali teena

    ReplyDelete
  2. Kiwango cha uwekezaji katika timu na maandalizi ndio kinaamua nafasi ya timu kwenye msimamo wa ligi,Tujifunze kwamba mafanikio ya timu kwenye ligi hayapimwi kwa mechi moja bali mechi zote kwenye msimu husika..Sasa hapa Tanzania Yanga ikitoka sare na Mtibwa au ikiifunga Mbeya City 1-0 watu wanaanza kuponda kambi ya Uturuki haikuwa na mafanikio.Halafu timu zinzotakiwa kautoa upinzani kama Mtibwa nayo inaridhika na matokeo ya sare dhidi ya Yanga badala ya kutafuta ushind kwenye uwanja wa nyumbani,labda kama sare hiyo ilikuwa kwa ajili ya kuwafurahisha watu fulani nje ya Mtibwa.Tuliona mechi ya juzi jinsi wachezaji wa Mtibwa walivyokuwa wanapoteza muda utadhani hawakuwa wanahitaji pointi tatu,na hivyo kuwanyima raha watazamaji waliolipa viingilio kuangalia mechi ya dakika 90 wakaishia kuangalia kwa dakika 70.Hata kocha Maxime alionekana kuridhika na hali hiyo wakati ukweli ni kwamba Mtibwa ilihitaji ushindi ili isogelee nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi

    ReplyDelete