Search This Blog

Saturday, March 29, 2014

AZAM FC, YANGA, PENGO LA POINTI LIGI KUU KUBAKI 1 AU 4 JUMAPILI?

Na  Baraka Mpenja, Dar es salaam


0712461976


KITENDAWILI cha klabu gani itatwaa taji la ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu hakichateguliwa kwasasa, na hapo kesho kutakuwa na  mechi muhimu kwa timu zinazopigiwa upatu  wa kutwaa ubingwa, Yanga na Azam fc.

Vinara Azam fc watakuwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kukabiliana na kikosi cha Simba, wakati mabingwa watetezi, Young Africans watakuwa na kibarua kizito mbele ya wapiga kwata wa Mgambo JKT, kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga.

Mechi ya Azam fc dhidi ya Simba sc itakuwa ngumu kwa klabu zote, lakini kwa Wana Lambalamba ina uzito wa hali ya juu katika mbio zao za kutwaa ubingwa.

Kama watapoteza mechi hiyo, halafu Yanga wakapata ushindi jijini Tanga, Azam watajiweka mazingira magumu zaidi ya kubeba mwari wao wa kwanza tangu waingie  ligi kuu msimu wa 2008/2009.

Yanga nao watatakiwa kuwa na mipango mizuri ya uwanjani dhidi ya Magambo kesho, kwasababu rekodi ya nyuma inaonesha wapinzani wao wamekuwa wagumu kufungwa Mkwakwani.

Hukutakuwa na sababu yoyote kwa kikosi cha Yanga kuwadharau Mgambo kwakuwa wapo katika mstari mwekundu wa kushuka daraja.

Maskari hawa wa  Jeshi la kujenga Taifa wanahitaji ushindi kwa nguvu zote kwasababu ndio matokeo pekee yanayowafaa kwasasa.

Taarifa kutoka Tanga zinaeleza kuwa kocha mkuu wa Young Africans,  Mholanzi Hans Van der Pluijm amewasifia vijana wake kwa kumuelewa vizuri na kushika vilivyo mafunzo yake.

Sababu kubwa inayotumiwa na  Pluijm ni matunda yaliyoanza kuonekana katika michezo miwili iliyopita kwa timu kuweza kujikusanyia pointi 6 na magoli nane ya kufunga, huku safu ya ulinzi ikizuia timu pinzani kuziona nyavu zao.

Kweli hayo ni mafanikio kwa klabu hususani wakati huu muhimu kwao kutetea ubingwa.

Lakini kesho Yanga watatakiwa kuingia kwa tahadhari kubwa dhidi ya Mgambo JKT.

Kocha msaidizi wa Mgambo JKT, Moka Shaban Dihimba aliueleza mtandao huu kuwa matokeo ya kufungwa mabao 2-0 na Azam fc jumatano yamezidi kuwafanya wawe na kazi kubwa ya kupambana kubakika ligi kuu.

“Tumefungwa na Azam fc. Hii imetupeleka mazingira mengine magumu zaidi  kwa wakati huu. Tunafahamu ugumu wa mechi ijayo dhidi ya Yanga. Hakika tumekaa chini na kuandaa mikakati ya kutofungwa na mabingwa hao watetezi”. Alisema Moka.

Si rahisi kujua mikakati ya Mgambo kuelekea mchezo huo, lakini kwa asilimia kubwa itakuwa mikakati ya ndani ya uwanja ambayo itaonekana hadharani Mkwakwani hapo kesho.

Wataalamu wanasema timu inayowania ubingwa ikikutana na timu inayokwepa mkasi wa kushuka daraja, mechi inakuwa ngumu zaidi.

Hivyo Yanga wanatakiwa kujipanga kwa kutumia uzoefu wao na ukongwe wa wachezaji wao kupata matokeo hapo kesho.

Hakuna cha muhimu zaidi kwa Yanga, ushindi pekee ndio itakuwa silaha yao katika mbio za kutetea ubingwa wao.

Ukiyatazama majina mawili ya Yanga na Mgambo JKT, hayana ufanano kabisa.

Yanga ni timu kubwa, kongwe, yenye wachezaji wakubwa na mashabiki lukuki, hivyo wanapewa asilimia kubwa ya kupata matokeo mazuri.

Lakini mpira huwa una mambo yake, si ajabu kuona Mgambo wanashinda kirahisi mchezo wa kesho.

Kwa mazingira ya timu zote mbili, ushindani utakuwa mkubwa, na itawalazimu wachezaji wa timu zote kuwa makini kutumia nafasi zao.

Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 46 baada ya kucheza mechi 21.

Kama watashinda kesho watafikisha  pointi 49 katika nafasi hiyo hiyo ya pili, bila kujali matokeo ya Azam fc yatakuwaje.

Wachezaji waliopo jijini Tanga  ni Magolikipa: Juma Kaseja na Ally Mustafa "Barthez"

Walinzi: Mbuyu Twite, Juma Abdul, Oscar Joshua, David Luhende, Kelvin Yondani na Nadir Haroub "Cannavaro".

Viungo: Frank Domayo, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Nizar Khalfani na Athuman Idd "Chuji"

Washambuliaji: Emmanuel Okwi, Mrisho Ngasa, Saimon Msuva, Didier Kavumbagu, Jerson Tegete, Hamisi Kizza na Hussein Javu.

Kwa mechi ya Dar es salaam, timu zote mbili, Azam fc na Simba zimeonekana kuogopana.

AZAM FC kupitia kwa katibu wake mkuu, Nassor Idrisa ‘Father’ imesema mechi dhidi ya Simba SC Jumapili itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao bado ni timu bora na watataka kurejesha heshima baada ya kucheza mechi tano bila kushinda.
“Simba SC ni moja ya timu bora msimu huu, haipo kwenye mbio za ubingwa kwa sababu ya bahati tu, lakini si kama ni timu mbaya. Kumbuka tulikuwa na Simba SC katika Kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu, sisi tukatolewa Nusu Fainali, wao wakaingia Fainali,”alisema Father.

Kwa upande wa Simba sc, Afisa habari wake, Asha Muhaji alisema kuwa wanaiheshimu zaidi Azam fc kwasababu msimu huu imekuwa na kikosi bora ambacho hakijafungwa hata mechi moja.

“Mechi itakuwa ngumu sana. Wapinzani wetu wako bora na wamepata matokeo mazuri kuliko sisi. Lakini haina maana kuwa hatuwezi kufanya vizuri. Tumejiandaa kwa lolote na malengo yetu ni kutafuta ushindi”. Alisema Asha.

Mechi hii itakuwa na umuhimu mkubwa kwa Azam fc kwasababu inaweza kuamua hatima yao endapo Yanga atashinda Mkwakwani.

Kama wataibuka na ushindi dhidi ya kikosi cha Dravko Logarusic itakuwa faida kubwa kwasabu wataendelea kuweka pengo  la pointi 4 baina yao na Yanga, hata kama Pluijm atawaongoza wanajangwani kushinda.

Kama Azam watapoteza, Yanga atawasogelea zaidi kileleni na kutofautiana kwa pointi moja tu, kitu  ambacho kitakuwa hatari zaidi.

Kocha wa Azam fc, Mcameroon, Joseph Marius Omog anatakiwa kutuliza kichwa chake hapo kesho kwasababu Simba hawatakubali kufungwa kirahisi.

Japokuwa mengi yanasemwa kuwa Simba wapo tayari kuwapa ushindi Azam fc, lakini si Yanga aprili 19, Omog na kikosi chake wasibweteke kwa maneno hayo ya mitaani.

Hatudhani kama benchi la ufundi la Simba linaweza kuwa na mawazo mabovu kiasi hicho.

Lazima wataingia kutafuta ushindi, kwasababu kufungwa tena kwa mara ya pili uwanja wa Taifa, itakuwa fedheha kwao na watawaumiza zaidi mashabiki wao.

Simba sc hawapo katika mbio za ubingwa, lakini si sababu ya kukubali kupoteza mechi kirahisi.

Azam fc wajiandae kupambana, ila nao Simba sc lazima wajipange zaidi kukabiliana na vinara hao kutokana na ubora wa kikosi chao.

Kwa matokeo ya uwanjani, Azam fc ni bora zaidi ya Simba, hivyo Loga lazima atulize akili yake.

Mechini nyingine za kesho ni baina ya Mbeya City  fc dhidi ya Tanzania Prisons , uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Kagera Sugar watakuwa nyumbani kuwakaribisha Ruvu Shooting katika dimba la Kaitaba, mjini Bukoba, mkoani Kagera.

Mtibwa Sugar watakuwa Manungu Complex kuumana na wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga.

Nao maafande wa JKT Ruvu watakuwa Azam Complex kuoneshana kazi na maafande wa JWTZ, Rhino Rangers kutoka mkoani Tabora.B

No comments:

Post a Comment