Search This Blog

Tuesday, March 25, 2014

AZAM FC WAIFUATA MGAMBO TANGA, NUHU, KIMWAGA, MWAIPOPO, FARID, GAMBO NJE!!


Na Baraka Mpenja , Dar es salaam

0712461976 au 0764302956

KIKOSI  cha wachezaji wa vinara wa  ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc kimeondoka leo asubuhi Jijini Dar es Salaam  kwa basi lake kwenda Tanga kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya wenyeji MgamboJKT,  utakaochezwa kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa ya Azam fc, wachezaji ambao wataukosa mchezo huo ambao ni majeruhi na hawajaambatana na timu Tanga ni, SamihHaji Nuhu, Joseph Lubasha Kimwaga, Ibrahim Mwaipopo, Farid Mussa na Ismail Gambo.
Azam fc mpaka sasa wamejikusanyia pointi 47 kileleni baada ya kushuka dimbani mara 21.
Nafasi ya pili wapo Yanga wenye pointi 43 baada ya kushuka dimbani mara 20, lakini kesho timu zote zinakabiliwa na mechi.
Yanga watakuwa na kibarua kizito uwanja wa Taifa dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons, wajelajela.
Azam fc wataingia katika mchezo wa kesho wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0  mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya JKT Oljoro katika uwanja wao wa Azam Complex.
Mabingwa watetezi Yanga wenyewe walikuwa mjini Tabora ambapo walishinda mabao 3-0 dhidi ya waburuza mkia katika msimamo, Rhino Rangers.
Afisa habari wa Azam fc, Jafar Idd Maganga aliuambia mtandao huu kuwa kwasasa kila mechi kwao ni fainali.
“Hatuna cha kuhitaji zaidi ya kuandika historia mpya katika soka la Tanzania. Mpaka sasa hatujafungwa katika michezo 21. Tunatafuta pointi tatu kwa Mgambo hapo kesho ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa Taji kwa mara ya kwanza msimu huu”. Alisema Jafar.
Jafar aliongeza kuwa wachezaji wao wanaelewa wazi majukumu yao na  ndoto za klabu msimu huu, hivyo imekuwa rahisi kwa kocha mkuu, Mcameroon, Joseph Marius Omog kuwaweka mchezoni muda wote.
“Mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono mpaka mwisho. Dhamira yetu ipo wazi. Tunatambua ugumu wa mechi ya kesho kwasababu Mgambo wanakwepa kushuka daraja. Tutajitahidi kuwa bora zaidi yao ili kuibuka na ushindi”. Alisema Jafar.
Naye kocha msaidizi wa Mgambo JKT, Moka Shaban Dihimba aliueleza mtandao huu kuwa wamejipanga vilivyo katika mechi hizi za mwisho ili kubakia ligi kuu.
“Mzunguko wa kwanza tulikuw a katika hali mbaya sana. Lakini ngwe hii ya pili tumejidhatiti na kufikisha pointi 19 katika nafasi ya 11. Malengo yetu ni kufanya vizuri mechi zilizosalia kuanzia ya kesho dhidi ya Azam fc”. Alisema Moka.
Kocha huyo alikiri ugumu wa mechi hiyo kwasababu Azam fc ni timu nzuri ambayo haijapoteza mechi yoyote mpaka sasa.

No comments:

Post a Comment