Search This Blog

Tuesday, February 11, 2014

JEZI YA DIDA NOMA YANGA

Na Arone Mpanduka,Radio Tumaini
GOLIKIPA wa klabu ya soka ya Yanga Deogratius Munishi ndiye mchezaji pekee katika timu ya Yanga anayevalia jezi yenye nambari kubwa kuliko yeyote kwenye timu hiyo.
 
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti la Tumaini Letu, Munishi maarufu kama Dida anatumia jezi nambari 30 mgongoni pindi anaposimama kwenye milingoti ya timu ya Yanga ambayo ndiyo yak mwisho katika klabu hiyo kwa sasa.
Wachezaji wengine wanaomfuatia Dida kwa kuwa na jezi yenye nambari kubwa mgongoni ni pamoja na mlindamlango namba moja Juma Kaseja ambaye anatumia jezi namba 29.
 
Mbali na Kaseja mchezaji mwingine wa timu hiyo ni Simon Msuva mwenye jezi nambari 27 akifuatiwa na mchezaji Hassan Dilunga mwenye jezi nambari 26 mgongoni.
Mshambuliaji mpya Emmanuel Okwi yeye anavalia jezi nambari 25 huku kiungo mahiri Athuman Iddi Chuji akitumia jezi nambari 24 tangu ajiunge na timu hiyo miaka saba iliyopita.
Beki Nadir Haroub Canavaro naye ni mmoja wa wachezaji wanaovalia jezi yenye nambari kubwa mgongoni akiwa na jezi nambari 23 huku kinda Hamis Nyige akiwa na jezi nambari 22 na mshambuliaji Hussein Javu jezi nambari 21.
NAMBA NA TAFSIRI ZAKE
Wapo baadhi ya wachezaji katika klabu ya hiyo ambao wamechagua namba za jezi kwa sababu maalum akiwemo mshambuliaji Emmanuel Okwi.
Okwi ameamua kuchagua jezi nambari 25 kwasababu alizaliwa Disemba 25 mwaka 1992 huko nchini Uganda hivyo ameona ni bora atumie nambari hiyo ili kuipa heshima tarehe yake ya kuzaliwa.
 
Si Yanga pekee ambako aliweza kufanya hivyo bali hata katika klabu alizopitia ikiwemo Sc Villa, Simba SC na hata timu yake ya taifa amekuwa akitumia jezi nambari 25.
Kwa upande wake Juma Kaseja ambaye sasa ana umri wa miaka 30 mwaka jana wakati alipojiunga na Yanga alipewa rasmi jezi nambari 29 ambayo ilikuwa ikiendana na umri wake.
 
Awali jezi hiyo namba 29 ilikuwa ikivaliwa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, raia wa Kenya, Boniface Ambani, kabla ya kustaafu kucheza soka la kulipwa.
JEZI NAMBA 9 NA IMANI POTOFU YANGA
Wachezaji mbalimbali wa Yanga wamekuwa na imani potofu kwamba jezi namba tisa mara nyingi haimpi mchezaji mafanikio anayoyataka ndani ya uwanja.
Imani hiyo imeibuka kufuatia wachezaji kadhaa waliowahi kupita katika timu hiyo kushindwa kufanya vizuri na kupeleka hata wengine kuishia kwenye benchi la wachezaji wa akiba na kushuhudia wenzao wakicheza mechi kadhaa.
 
Awali jezi nambari tisa Yanga ilikuwa ikivaliwa na Mkenya, Boniface Ambani ambaye baadaye aliachana nayo na kuhamia namba 24 na kumfanya awe mfumania nyavu hatari katika timu hiyo.
Baadae jezi namba 9 ikaenda kwa Mcameroon, Jama Mba, ambaye naye alijikuta kama ana mikosi baada ya kuonekana si lolote si chochote na kuishia benchi kabla klabu kumfungashia virago na kurejea kwao.
Baada ya Mbuyu Twite kujiunga na Yanga mwaka 2013, uongozi ukampatia jezi nambari tisa lakini aliikataa na kupewa namba 6 baada ya kusikia tetesi kwamba namba hiyo ina mikosi klabuni hapo.
 
Mchezaji mwingine wa Yanga Omega Seme aliitumia jezi hiyo lakini taratibu makali yake yakapungua na mwishowe Yanga ikamchoka na kumtoa kwa mkopo kwenda klabu ya Tanzania Prisons ya jijini Mbeya.
Kwa sasa jezi hiyo inatumiwa na mshambuliaji Renatus Lusajo Mwakasabule ambaye mara zote amekuwa akiishia kukaa benchi huku akiwaachia nafasi kina Mrisho Ngassa,  Kavumbagu na Tegete wakicheza katika safu ya ushambulizi.
 
Kasumba hiyo mbovu pia imewakumba watani wao wa jadi Simba ambao nao wanaikimbia jezi namba tisa.
Mchezaji Ramadhani Salum ndiye anavaa jezi hiyo huku akiwa hana nafasi katika kikosi cha kwanza.
Katika kipindi cha nyuma namba hiyo alikuwa nayo mchezaji Kago Gervais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambaye alijiunga na klabu hiyo kwa mbwembwe nyingi.
Hata hivyo kiwango chake kilikuwa duni na kuishia katika benchi la wachezaji wa akiba na mwishowe akafungashiwa virago na uongozi wa klabu ya Simba.
 
0786160643

No comments:

Post a Comment