Search This Blog

Wednesday, February 19, 2014

BODI YA LIGI INAHUSIKA NA UFUJAJI WA MAPATO SOKOINE.

 Mtendaji mkuu wa bodi ya ligi,Silas Mwakibinga
Na Moses Ng’wat,Mbeya.

Katika kile kinachoonekana uvumilivu kumshinda, Meneja wa uwanja wa CCM Sokoine, Modestus Mwaluka, ameamua kutapika nyongo na kuituhumu bodi ya ligi na TFF kuhusika na uvujaji wa mapato.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mwaluka amesema kwa namna moja au nyingine kuna baadhi ya viongozi wa TFF na bodi ya ligi walihusika na hujuma ya mapato katika mchezo wa Mbeya City na Simba.

Amesema katika mchezo huo uliochezwa Februari 15 katika uwanja wa CCM Sokoine na timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1, licha kuvuna kiasi cha shilingi milioni 105 na kuvunja rekodi ya mapato ndani uwanja huo, lakini kiasi kikubwa cha fedha kiliishia mikononi mwa wachache.

Amesema akiwa kama Meneja wa uwanja alipokea taarifa ya kuwepo kwa tiketi feki walizouziwa mashabiki, lakini alipojaribu kutoa taarifa kwa msimamizi  wa kitua aliishia kuambulia majibu yasiyo na tija.

“Zaidi ya tiketi 30 zililetwa kwangu zikiwa hazijagongwa muhuri na nilipolifikisha suala hilo kwa wasimamizi wa mchezo kutoka bodi ya ligi walidai kuwa tiketi hizo hazikugongwa muhuri kwa bahati mbaya ”.

Ameongeza kuwa hata kama kweli tiketi hizo zilipita bila kugongwa wakati wa zoezi hilo la kugonga muhuri, zisingeweza kuwa nyingi kwa kiasi kilichoonekana mlangoni siku hiyo ya mpambano.

Amesema kutokana na hali hiyo, viongozi hao hawana sababu ya kumshika mtu uchawi katika ufujaji wa mapato hususani katika mechi kubwa bali waanze wao kwanza kujitazama.

Amesema ni wazi kwa tukio hilo la mpambano huo wa Mbeya City na Simba hujuma kubwa ya mapato ilifanywa na baadhi ya viongozi wa taasisi hiyo.

Bodi ya ligi hivi karibuni ilionekana kulalamikia ufinyu wa mapato katika michezo mikubwa inayochezwa katika uwanja wa Sokoine, ikiwemo pambano la Mbeya City na Yanga, pamoja na Mtibwa Sugar.

1 comment:

  1. Hii ndio bongo yetu!! Tulikataa tulikataa kutumia tiketi za kielectronic eti kisa mashabiki hawauelewi mfumo!! Yaani sababu za kijinga tuu!! Kwa mechi ya MBY city na simba naamini zilipatikana zaidi ya million 200!!

    ReplyDelete