Search This Blog

Thursday, January 2, 2014

JICHO LA TATU: HOFU YANGU KWA MBEYA CITY MZUNGUKO WA PILI LIGI KUU TANZANIA BARA!!

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam.WAKATI nasoma shule ya Msingi miaka ya nyuma, familia yangu ilifurahia sana matokeo yangu ya mitahani kwasababu mara nyingi nilikuwa nashika nafasi ya kwanza kwenye darasa la wanafunzi zaidi ya 80.Nakumbuka furaha ilikuwa inaongezeka zaidi pale ninaposhika nafasi ya kwanza katika mitahani ya ujirani mwema iliyonikutanisha na zaidi ya shule mbili.Hata mimi nilikuwa nafurahia mafanikio yale na kusahau kuwa kuna upande wa pili wa shilingi. Ikafika wakati mambo yakaenda vibaya sana, nikashuka uwezo kutokana na kuvimba kichwa na kuacha kujisomea kama awali.Kilichonipa kiburi ni kwamba, kuna siku nilienda kufanya mtihani bila hata kusoma, nilipasua `pepa` vizuri sana. Nikapunguza kasi ya kujisomea na kujiamini zaidi. Balaa lilitokea baadaye ni siri yangu, lakini nikajipanga upya na kurudi mchezoni.Mbali na kuacha kujisomea, wanafunzi wenzangu kumbe walikuwa wananionea wivu sana, hakika walikuwa wanapiga kitabu sana ili kunishusha. Walifanikiwa kwa kipindi kifupi sana.Kwa kipindi kile, baba yangu alichukia sana kushuka kiwango katika masomo. Alinigombeza kila wakati kwanini nimebadilika. Niliumia na kumwona kama `anazingua` tu.Baadaye alinivumilia na kunipa muda wa kurekebisha makosa yangu,  nikajipanga vizuri zaidi kurudi kwenye mchezo ule wa ushindani na kufanikiwa.Kutokana na hali ile, nikajifunza kuwa mimi nilikuwa sawa na mchezaji niliyopo kwenye kiwango cha juu. Familia yangu iliyokuwa ikifurahia mafanikio yangu ni sawa na mashabiki wa soka. Wanafunzi waliopambana na mimi ni timu nyingine za ligi.Nikiyakumbuka haya, nafananisha matokeo ya klabu ya Mbeya City waliyoyapata ligi kuu soka Tanzania bara mzunguko wa kwanza.

Hakika timu hii ilikonga nyoyo za watu kutokana na kasi yake, morali kubwa kwa wachezaji na mfumo bora wa kocha wake Juma Mwambusi kuwaamini vijana wadogo ambao baadhi ya timu zisingethubutu kutoa nafasi kwao.

Wakiwa katika kiwango cha juu, walifanikiwa kumaliza mzunguko wa kwanza bila kufungwa mchezo wowote. Walifanya vizuri ugenini na nyumbani , hivyo kujikusanyia pointi 27 katika nafasi ya tatu sawa na Azam fc katika nafasi ya pili, huku kileleni akiwepo Bingwa mtetezi, Dar Young Africans kwa pointi 28.Kutokana na ubora wa Mbeya City kuanzia wakati inacheza ligi daraja la kwanza mpaka inapanda ligi kuu kwa msimu huu kwa mara ya kwanza, timu hii ilijizolea umaarufu na mashabiki wengi mkoani Mbeya na nje ya Mbeya.

Kama ni mshale kusoma, basi idadi ya mashabiki ilikuwa inaongezeka kwa kasi ya mwanga wa rad, lakini hali hii ilitokana na mafanikio ya klabu kwa wakati ule.

Niliwahi kufanya mahojiano marefu na makocha wa timu hii, yaani kocha mkuu Juma Mwambusi na msaidizi wake, Maka Mwalwisyi.

Mwambusi kwa upande wake aliwahi kunieleza kuwa Mbeya City ni timu yenye falsafa mpya kabisa kulinganisha na timu nyingine.

Nilipomuuliza ni falsafa gani?, alijibu kirahisi sana kuwa wanaamini katika soka la vijana na kutengeneza mfumo wa kuibua makinda na kuwapandisha timu A ambayo pia huwezi kusema ni ya wakubwa kwani  imejaza vijana.
Nilichukuu moja ya nukuu muhimu kutoka kwa Mwambusi ambayo ni; 

“Mchezaji yeyote unayemsikia duniani iwe kitaifa au  kimataifa, anawika kwasababu aliaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza mpira”. “Najua ni ngumu na inahitaji kuvumilia kutokana na makosa makubwa ya wachezaji vijana, lakini lazima uwape nafasi ili sikuikifika  waje kuitwa wachezaji wenye uzoefu”.

Yalikuwa maneno mazito kwangu na ndipo nilipoanza kukichunguza kikosi chake. Niligundua ni kweli amewapa nafasi vijana wadogo sana ambao hawana majina. Mfano,; Alex Seth, Deus Kaseke, Hassan Mwasapili, Peter Richard, Jeremiah John, Kenny Ally, Deogratius Julius na wengine wengi.
Pia nikagundua kuwa kilichokuwa kituo cha cha soka la vijana cha `Forest Youth Soccer Academy` (FOYSA) chini ya mkurugenzi wake Maka Mwalwisyi ambaye kwa sasa ndiye msaidizi wa Mwambusi , kilibadilishwa na kuwa mradi wa Mbeya City. Vijana wa kituo hiki wameunda kikosi B cha Mbeya City na sasa klabu imekuwa na uhakika wa kupata vijana kwa wakati wote.

Kwasababu vijana waliaminiwa na kocha Mwambusi, basi nao waliucheza mpira na kumlipa fadhila wakati wa mzunguko wa kwanza.

Imani kubwa na kujitoa mhanga kwa Mwambusi ndiko kulimfanya awe maarufu zaidi, ingawa alikuwa maarufu kutokana na rekodi yake akiwa na Tanzania Prisons pamoja na timu ya mkoa wa Mbeya,  Mapinduzi Stars iliyokuwa inashiriki kombe la Taifa ambalo kwasasa halipo.

Baada ya kupata mafanikio ngwe ya kwanza, mashabiki waliongezeka zaidi na kuanza kumpenda kocha huyu na timu yake.

Lakini kuna wakati nilikuwa Uwanja wa sokoine kushuhudia mchezo wa ligi kuu baina ya Mbeya City dhidi ya Ruvu Shooting uliomalizika kwa ushindi wa 2-1 kwa Mbeya City. Katika mchezo huu City walipata bao la ushindi dakika za mwisho.

Kabla ya bao hilo, mashabiki walikuwa wanazomea wachezaji na kusogea eneo la benchi la ufundi na kumwimbia Mwambusi nyimbo za kejeli wakimtaka mchezaji anayeitwa Kenny Ally, huku wakisema kama atatoa sare hapataeleweka na wengine wakisema wachezaji watakula mboko.
Niliporejea kwenye orodha ya wachezaji wa kikosi cha kwanza na wa akiba, niligundua Kenny hakuwepo kabisa katika mipango ya mwalimu katika mechi ile.
Nilishituka sana kwasababu ilikuwa mapema sana. Baadaye Mwambusi aliwaita mashabiki wanywa pombe na hawatumia akili. Wengi walimshangaa kocha huyu kwa kitendo kile cha kuonesha ishara ya kuwaambia hawatumii akili.

Baadaye timu ikapata ushindi, walewale waliokuwa wanazomea wakageuka kuwa wa kwanza kushangilia na kumsifu Mwambusi.
Binafsi nilipata fundisho kubwa kuwa inawezekana mashabiki wa Mbeya City ni watu wa kufurahia mafanikio kama ilivyokuwa kwa familia yangu wakati nasoma shule ya Msingi.

Utoafuti ni kwamba wazazi wangu walinigombeza kwa lugha nzuri na kunipa matumaini, lakini si kama wao kuzomea na kutishia kuwapiga wachezaji kama watapata sare nyingine nyumbani.

Kama walichukia sare mapema vile na timu yao ilimaliza vizuri mzunguko wa kwanza,  endapo mambo yatageuka kwao , watavumilia kweli?.

Mashabiki wa Mbeya City unaweza kusema wamezoe kushangilia matokeo na hawajapata zahama kama ilivyokuwa kwa wenzao, Rhino Rangers na Ashanti United ambao walichezea vichapo vingi.

Sisemi Mbeya City watafanya vibaya, lakini najaribu kutafakari kama watavumilia matokeo mabaya kwa timu yao au ndio itakuwa mwisho wa kukodi mabasi madogo ya abiria na kusafiri kuifuata timu yao popote pale.
Wataendelea na kasi ile au watachoka?, Majibu ni magumu kupata kwani kitendo kile kilichotokea kwenye mchezo wa Shooting kilinipa  shida na mpaka sasa wasiwasi ni mkubwa kwangu.

Sina hakika kama mashabiki hawa wanaelewa kuwa mpira wa miguu ni mchezo unaobadilika. Leo unaweza kufurahi, kesho ukainamisha kichwa chini.

Sawa na mashabiki wa Manchester United waliozoea ushindi wakati wa Sir Alex Ferguson, lakini kwa sasa mambo yamebadilika wakati wa David Moyes. Kwa wale wenye mioyo laini, wameshakata tamaa, lakini mashabiki wa kweli bado wanaendelea kuishabiki timu yao.Vipigo kwenye soka vipo. Ulijua Arsenal kwa ubora wao wangelala 6-3, au Tottenham Hotspurs kula 5-0 kutoka kwa Manchester City?. Ndio mpira ndugu zangu na huwa iko hivyo.Kwa hawa mashabiki wa Mbeya City ambao wanafura na hasira kama mbogo pale timu inapoelekea kupata  sare tena mechi za mwanzo kabisa tangu waingie ligi kuu, hakika ninakuwa na wasiwasi mkubwa kuwa wanaweza kusambaratika kipindi timu yao ikianza kula vipigo.Sitaweza na sitawahi kuitabiria mabaya timu yoyote, lakini kwa utamaduni wa mashabiki wa Tanzania kushindwa kutoa muda kwa wachezaji wao na kukosa uvumilivu katika ujenzi wa timu, nakuwa na wasiwasi kama mashabiki wa Mbeya City watavumilia endapo wataanza kufungwa.

Labda wafanye kitu kimoja. Wanatakiwa kukaa pamoja na kuelezana, kupeana semina, kujengana kisaikolojia kuwa si kila wakati watakuwa wanapata matokeo ya ushindi.Wakubali kuwa soka lina kupanda na kushuka. Wajifunze kuwa na subiri na kujenga imani kwa wachezaji wao pamoja na makocha wao.

Mipango ya Mwambusi na Mwalwisyi iko wazi, wanatakiwa kupewa muda wa kutosha kwani wanaonekana kuwa na mawazo tofauti na timu zetu za Simba  ambazo hazina uvumilivu.Kinachotakiwa ni kujiandaa kwa lolote lile, kama mipango yao itashindikana mzunguko wa pili, mashabiki wanatakiwa kuendelea kuisapoti timu kwa namna ile ile ya Chamazi kwenye mechi ya mwisho mzunguko wa kwanza dhidi ya Azam fc iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3, huku Mwagane Yeya akipiga matatu `Hat- Trick`.Kama wataendekeza  fitina na majungu, maneno makali kwa makocha na wachezaji, itabaki kuwa historia tu kuwa waliwahi kutamba. Mashabiki waelimishwe na kubadilu fikira za kufurahia ushindi na kusahaua upande wa pili wa shilingi.Bado nina imani na kikosi cha Mbeya City kuwa kinaweza kufanya vizuri mzunguko wa pili. Lakini rekodi ya kutofungwa  `unbeaten` sina hakika kama itaendelea.Naamini mipango yao ni sahihi,  wapo katika maandalizi mazuri. Kikosi ni kile kile, hakuna mabadiliko yoyote. Wachezaji wakiendelea kujituma na kucheza kwa kasi ile ile, bila shaka wataweza kupambana kwa wakati wote.Wachezaji watatakiwa kuendelea kuucheza mpira bila kujali kelele za kushangiliwa au kuzomewa. Ije kuwa mwiko kwao kucheza na jukwaa huku wakilewa sifa za mzunguko wa kwanza kwani ni ngumu kwao  kuja kutambua  timu nyingine zimeandaaje majeshi yao.Kuna siku aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Yanga, Fredy Felix Minziro aliniambia mzunguko wa pili Mbeya City watayeyuka mithiri ya barafu juani.

Akaniambia timu nyingine ikiwemo Yanga, zitaingia kwa kasi, zitapambana na Mbeya City kwa kufuta fikira kuwa ni timu changa na ngeni  katika michuano ya ligi kuu.Maneno ya Minziro yalimaanisha, timu zenye uzoefu zilikuwa zinaingia uwanjani kwa kuzidharau timu mpya za Mbeya City, Ashanti United na Rhino Rangers.Kwa Ashanti na Rangers timu zenye uzoefu zilifanikiwa kushinda, lakini Mbele ya Mbeya City, mambo yalikuwa magumu zaidi na hakuna timu iliyofua dafu.Kama Mbeya City wamekaa chini na kugundua kuwa watakuwa na  changamoto kubwa  mzunguko wa pili, basi yawezekana maneno ya Minziro yakabaki kuwa ndoto.Lakini kama wamebweteka na kujiona wameweza, basi yanaweza kuwakuta ya JKT Oljoro ambao walikuja kwa kasi misimu ya nyuma na kuongoz aligi, lakini wakageuka kitowea mpaka sasa.Cha msingi mashabiki, wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wakae pamoja kuunda nguvu ya kuanza nayo mzunguko wa pili.Kama watashindwa kukaa na kujipanga, halafu wakaingia kirahisi na kufungwa zaidi, hapo ndipo hofu yangu inaibuka kuwa Mbeya City inaweza kupotea.Vizuri zaidi, makocha wake wameonekana kugundua kuwa wapo katika changamoto kubwa na ndio maana waliingia kambini mapema na sasa wanaenda kucheza kombe la Mapinduzi huko Zanzibar.Tusubiri wakati ufike, ili tujiridhishe na uwezo wao na maneno yao.  Mpira sio siasa za mdomoni bali unachezwa hadharani Uwanjani. Aliyewahi kuwa kocha wa mabingwa wa zamani wa Afrika, timu ya Taifa Zambia, Chipolopolo, Mfaransa, Herve Renard,  wakati akijiandaa na mchezo wa fainali ya AFCON dhidi ya Ivory Coast alisema mpira wa miguu ni mipango, mwenye kujipanga na kuwa makini anaweza kuibuka na ushindi.Akasema Ivory Coast na Zambia hakuna ushindani ukiangalia majina ya nchi katika viwango vya ubora vya FIFA , hata aina ya  wachezaji waliopo, lakini akasema anaenda kutafuta matokeo mbele yao. Kweli walifanikiwa.

Hata Mbeya City licha ya uchanga wao wanaweza kupambana na klabu za  Simba sc, Yanga na Azam fc katika kinyang1anyiro cha ubingwa na kutwaa taji kwa mara ya kwanza, hivyo kuvunja rekodi ya Tukuyu Stars iliyowahi kupanda ligi kuu na kutwaa ubingwa msimu huo huo.

No comments:

Post a Comment