Search This Blog

Sunday, December 29, 2013

PRISONS MWENDO MDUNDO LIGI KUU, YAANZA KUCHEZA MECHI ZA KIRAFIKI KUSUKA KIKOSI CHAO UPYA!!


Na Baraka Mpenja, Dar es salaam

TANZANIA Prisons `Wajelajela` wameanza kukipima kikosi chao kwa kucheza mechi za kirafiki kabla ya kuanza kujinasua katika mstari mwekundu wa kushuka daraja  ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.

Klabu hiyo iliyomaliza mzunguko wa kwanza katika nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 9 kibindoni, jana imeshuka dimbani kujipima ubavu dhidi ya klabu ya  Njombe mji, mechi iliyopigwa mkoani Njombe.

Mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya kufungana mabao 2-2, lakini mvua ilikuwa nyingin sana na kuharibu ubora wa kabumbu.

Insepkta, Sadick Jumbe, katibu mkuu wa Prisons ameuambia mtandao huu kuwa baada ya mechi ya jana, wanatarajia kukipima uwezo tena kikosi chao desemba 31 dhidi ya Combine ya Kyela mjini Kyela.

“Dirisha dogo tumesajili wachezaji watano, mwalimu Mwamwaja ameanza mikakati ya kusuka upya kikosi chake, huko Kyela atawatumia wachezaji wote ikiwa ni mipango ya kupata kikosi cha kwanza”. Alisema Jumbe.

Jumbe aliwataja wachezaji wapya kuwa ni Dennis Liwanda, Godfrey Pastory, Henry Mwalugal, Jamal Salum na Brayton Mponzi.

“Wachezaji hawa wametuongezea nguvu, hata ukiangalia mazoezi yanavyokwenda, unagundua kwa haraka kuwa kuna mabadiliko makubwa. Timu inacheza mpira mzuri, nadhani Kocha David Mwamwaja ni chaguo sahihi kwetu”. Alisema Jumbe.

Aidha, Jumbe aliongeza kuwa eneo ambalo mwalimu wao mpya anaangalia kwasasa ni safu ya ushambuliaji ambayo mzunguko wa kwanza ilikuwa butu na kuwanyima ushindi katika sare sita walizotoa.

Mzunguko wa kwanza, Prisons ilishinda mechi moja (1) tu na kutoa sare sita (6) na iliambulia kipigo katika mechi sita (6), hivyo kujikusanyia mzigo wa pointi 9 kibindoni.
Mechi za mwishoni katika mzunguko huo, walitangaza kumfukuza kocha wao mkuu, Jumanne Chale na kumuajiri Mkongwe, David Mwamwaja ili kuwanusuru na janga la kuporomoka daraja.

No comments:

Post a Comment