Search This Blog

Thursday, November 21, 2013

MASHABIKI WA SIMBA NA YANGA KUCHUANA NANI MTANI JEMBE DODOMA, MUSOMA NA SINGIDA

Na Mwandishi Wetu

Kampeni ya Kili Nani Mtani Jembe itaendelea kuunguruma tena Jumapili wiki hii na kuwapa nafasi mashabiki wa Simba na Yanga walioko Dodoma, Musoma na Singida na kuchuana vikali katika michezo mbalimbali huku wakihakikisha timu zao zinaibuka na kitita cha shilingi milioni mia moja zilizotengwa na Kilimanjaro Premium Lager kwa ajili ya Watani wa Jadi kupitia kampeni hiyo.

Mratibu wa mabonanza hayo, Lawrence Andrew amesema jijini Dar es salaam jana kwamba mashabiki watapata fursa ya kushiriki katika michezo mbalimbali kama vile foosball, kuvutana kamba, soka la wachezaji saba kila upande maarufu kama “Seven aside” na kuongeza kuwa ili kuhakikisha mashabiki hao wanafurahia ipasavyo burudani mbalimbali za muziki zitakuwepo pamoja na Nyama choma.
Andrew alisema kuwa katika mji wa mji wa Dodoma bonanza la Kili Nani Mtani Jembe litafanyika katika uwanja wa shule ya Dodoma Sekondari ambapo bendi maarufu ya The TNC Band itatumbuiza. Na huko Musoma bonanza litafanyika katika uwanja wa Mukonde na kupambwa na bendi ya Musoma Stars huku mkoani Singida likifanyika katika Uwanja wa Namfua na burudani kabambe ikishushwa na Wana Pamba Music Band aka Watoto wa Mujini bendi ambayo imejizolea umaarufu mkubwa sana mkoani humo.

Andrew pia amesema kuwa vilevile kuwa michezo mbalimbali ya kujifurahisha kama vile kufukuza kuku wa kienyeji, kukimbia na gunia na kupiga penati ukiwa umefungwa kitambaa usoni itapamba mabonanza hayo ambayo yatafanyika katika mikoa hiyo kwa mara ya kwanza kupitia Nani Mtani Jembe. Kampeni hii ya aina yake inatoa fursa ya kipekee kwa mashabiki hao kujumuika pamoja na kuburudika na vile vile imeongeza chachu ya ushindani na utani wa jadi kati ya mashabiki hao huku ikiwapa fursa ya kipekee kuonyesha mapenzi kwa timu zao.

Mabonanza hayo yanalotarajiwa kuanza saa tatu asubuhi ni mwendelezo wa kampeni ya Nani Mtani Jembe ambayo inafanyika nchi nzima ikiwashirikisha mashabiki wa timu kongwe za Simba na Yanga. Kupitia kampeni hiyo, Kilimanjaro Premium Lager inayozidhamini timu za Simba ya Yanga imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 na kisha kuzigawanya kwa timu hizo ambapo kila timu inazo shilingi milioni 50 ambazo zinashindaniwa na mashabiki wao.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro George Kavishe alisema kuwa mashabikiwa Simba na Yanga wanatakiwa kushindana kwa kushiriki kwenye kampeni hiyo ili kuhakikisha kuwa timu mojawapo inapata fedha nyingi zaidi ya timu nyingine.
Akielezea namna ya kushiriki, Kavishe alisema kuwa mpaka kila timu imetengewa shilingi milioni 50 na kuwa mshiriki wa shindano hilo la Nani Mtani Jembe ambaye ni shabiki wa Simba au Yanga anachotakiwa kufanya ni kununua bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambayo kwenye kizibo chake kuna namba ya kushiriki.

Alisema baada ya shabiki kununua bia ya Kilimanjaro na kuona namba ya kwenye kizibo, anachotakiwa kufanya ni kuchukua simu yake ya kiganjani na kuandika ujumbe mfupi wa maneno akianza na jina la timu anayoshabikia kisha anaandika namba iliyo kwenye kizibo na kuituma kwenye namba 15440.

Alisema baada ya shabiki kutuma namba hiyo, atakuwa amepunguza shilingi 10,000 kutoka kwa timu pinzani yaani ikiwa shabiki aliyetuma ujumbe huo ni wa Simba atakuwa amefanikiwa kupunguza shilingi 10,000 kutoka kwenye fungu la Yanga na ikiwa shabiki ni wa Yanga pia atakuwa amepunguza shilingi 10,000 kutoka kwa Simba.

Kwa mujibu wa Kavishe matokeo ya uwiano wa fedha zinavyopungua kutoka Simba au Yanga yatangazwa kila siku hadi siku ya mwisho wa shindano hilo Desemba 14, mwaka huu siku ambayo watani wa jadi Simba na Yanga watacheza mechi ya kuhitimisha kampeni hiyo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment