Search This Blog

Tuesday, November 26, 2013

KILIMANJARO STARS YATUA SALAMA NAIROBI TAYARI KUWANIA CHALLENGE CUP

Timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) imewasili salama Nairobi, Kenya tayari kwa mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoanza kesho (Novemba 27 mwaka huu) katika Uwanja wa Nyayo.

Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iliwasili saa 3 usiku kwa ndege ya RwandAir, na imefikia katika hoteli ya Sandton iliyoko katikati ya Jiji la Nairobi.

Kwa mujibu wa programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen, Kilimanjaro Stars leo (Novemba 26 mwaka huu) ni mapumziko ambapo kesho itafanya mazoezi kujiandaa kwa mechi yake ya kwanza dhidi ya Zambia itakayochezwa Novemba 28 mwaka huu Uwanja wa Machakos.
   
MECHI YA TANZANITE SASA KUCHEZWA DAR
Mechi ya kwanza ya raundi ya michuano ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa wanawake chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Tanzanite) na Afrika Kusini iliyokuwa ichezwe Mwanza sasa itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Baada ya ukaguzi uliofanywa na maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imebainika uwanja huo unatakiwa ufanyiwe marekebisho ambayo hayawezi kuwahi Desemba 7 mwaka huu, siku ambayo ndiyo mechi hiyo inatakiwa kuchezwa.

Vyumba vya wachezaji vya uwanja huo ndilo eneo ambalo linatakiwa  kufanyiwa marekebisho makubwa.


WANNE WASHINDA UCHAGUZI CECAFA
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limepata wajumbe wapya wa wanne wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi uliofanya leo (Novemba 26 mwaka huu) hoteli ya Hillpark jijini Nairobi.
Uchaguzi huo ulifuatiwa na Mkutano Mkuu wa CECAFA ulioongozwa na Mwenyekiti wake Leodegar Tenga na kuhudhuriwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Kalusha Bwalya na ofisa wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Emmanuel Maradas.

Rais wa zamani wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa ndiye aliyeongoza katika uchaguzi huo ambapo wasimamizi walikuwa Bwalya na Maradas.

Mulindwa alipata kura zote 12 na kufuatiwa na Tariq Atta wa Sudan (10), Abdigaani Saeb Arab wa Somalia (9) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8). Atta, Arab na Gisanura walikuwa wakitetea nafasi zao.

Walioshindwa ni Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Sudan Kusini (SSFA), Alei Chabor aliyepata kura tano na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya aliyepata kura nne.

MICHUANO YA UHAI YAHAMIA CHAMAZI
Michuano ya Kombe la Uhai imeingia hatua ya robo fainali ambapo sasa mechi zinachezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Uamuzi wa kuhamisha mechi hizo kutoka viwanja vya Karume na DUCE ni kuziwezesha zote kuoneshwa moja kwa moja (live) na Azam Tv.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunaomba radhi kwa washabiki ambao watakuwa wameathirika kutokana na uamuzi huo.

No comments:

Post a Comment