Search This Blog

Monday, November 4, 2013

KILICHOIPONZA ASHANTI MWANZO HIKI HAPA

WAKATI inaanza Ligi Kuu ya Bara, Ashanti United ya Ilala jijini Dar es Salaam ilianza vibaya baada ya kupata matokeo yasiyo ya kuridhisha hivyo kujikuta ikiwa mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo kwa muda mrefu kidogo, lakini nyuma ya pazia kuna vitu vilikuwa vimejificha.
Kwa mujibu wa mmoja wa wachezaji waandamizi wa klabu hiyo, kitu kikubwa kilichoifanya Ashanti isifanye vizuri ni uwapo wa  

WACHEZAJI WENGI WASIO NA UZOEFU wa kucheza ligi kuu.

Tangu ilipopanda msimu huu, Ashanti haikuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu wa maana kuweza kuhimili mikiki mikiki ya ligi hiyo ambayo ina timu zenye wachezaji wa hali ya juu.
“Hatukuwa na wachezaji wenye uzoefu wa maana kuweza kupambana na wachezaji wa kulipwa kama Haruna Niyonzima au Didier Kavumbagu wa Yanga, pia hata Kipre Tchetche wa Azam, hivyo tulikuwa tunacheza na watu ambao unawajibika kuwaelekeza kila mara kuhusu nini cha kufanya.
“Hali hii ilitufanya kutofanya vizuri katika mechi za mwanzoni lakini sasa naona tumetulia na mambo yanaenda vizuri,” kinasema chanzo chetu.

WACHEZAJI HAWAKUWA WAKIMWELEWA KOCHA

Inadaiwa wachezaji wengi wa Ashanti hawakuwa wakimwelewa kocha aliyeondoka Hassan Banyai kiasi cha kushindwa kucheza ipasavyo katika kila mchezo waliokuwa wanacheza.
“Tulikuwa tunacheza kila mechi kutokana na maelekezo ya mwalimu na kila mchezo ulikuwa na maelekezo yake, sasa utakuta mchezaji anaelekezwa hivi halafu anapoingia uwanjani anacheza vile, hili lilikuwa tatizo kwetu.
“Lakini sasa hali imetulia kwani wachezaji wenyewe wametulia baada ya kukutana wenyewe kwenye kikao chao na kuwekana sawa kuhusu mwenendo wa timu na mustakabali wake katika ligi.

“Siwezi kuzungumza sana kuhusu POSHO kwani kuna wakati wachezaji wanaweza kuona timu imeingiza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na mapato ya milangoni lakini wao wanaambulia kiasi kidogo hapo lazima kutakuwa na maneno, lakini sasa kila mchezaji anajua namna viongozi wanavyotumia fedha nyingi katika kuiendesha timu na kuna wakati fedha inaingia lakini inalipwa madeni.

“Ukitazama vizuri utaona kuna mechi mbili tu ambazo tunaweza kuingiza kiasi kikubwa cha fedha, hizo ni dhidi ya Simba na Yanga pekee lakini mechi zote zilizobaki hakuna fedha ya maana inayopatikana, sasa wachezaji wanaelewa kuhusu hali hiyo na mambo yanaenda vizuri,” kinasema chanzo chetu.     
 Wakati Simba ikishika nafasi ya nne ikiwa na pointi 21 baada ya mechi 12, Ashanti yenyewe ina pointi 10 ikiwa katika nafasi ya 11 baada ya kucheza mechi 12 pia.
Ashanti ni miongoni mwa timu tatu zilizopanda msimu huu wa Ligi Kuu huku nyingine zikiwa ni Mbeya City na Rhino Rangers ya Tabora.

No comments:

Post a Comment