Search This Blog

Thursday, October 31, 2013

SIMBA YAVUTWA NA KAGERA SUGAR TAIFA LEO, MABOMU YAPIGWA UWANJANI


PENALTI iliyopigwa dakika za nyongeza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara uliozikutanisha Simba na Kagera Sugar muda mfupi uliopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ilibadili matokeo na kufanya mchezo huo kuisha kwa sare ya bao 1-1.
Huku mashabiki wengi wakidhani mechi hiyo ingemalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0, mwamuzi Mohamed Theofile wa Morogoro aliipa penalti Kagera wakati mwamuzi wa akiba akiwa ameshaonyesha dakika nne za nyongeza na mashabiki kutoamini kilichotokea.
Beki Joseph Owino ndiye aliyesababisha penalti hiyo baada ya kumchezea vibaya Daudi Jumanne wa Kagera ndani ya eneo la hatari ambapo, beki Salum Kanoni wa Kagera alifunga penalti hiyo na sekunde chache baadaye mwamuzi alimaliza pambano hilo.
Awali Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 45 lililofungwa na Amisi Tambwe baada ya mabeki wa Kagera kujichanganya katika kuokoa. Bao hilo lilidumu hadi timu hizo zilipoenda kupumzika.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi lakini hadi dakika ya 85, hakuna timu iliyoweza kupata bao kutokana na safu zote za ushambuliaji kutokuwa makini.
Mshambuliaji wa Kagera, Themi Felix pamoja na winga Paul Ngwai leo hawakuweza kufurukuta mbele ya mabeki wa Simba waliokuwa wakiongozwa na nahodha wao Nassor Masoud ‘Chollo’.
Nao washambuliaji wa Simba, Tambwe na Betram Mombeki hawakuweza kufuruka kutokana na mabeki wa Kagera kucheza kwa nguvu zaidi wakiongozwa na Maregesi Mwangwa ambaye ni nahodha wao.
Muda mfupi baada ya Kanoni kufunga bao, alienda kushangilia akiwa sambamba na wenzake mahala ambapo mashabiki wa Simba wamekaa na kuzua tafrani ya kurushiwa chupa za maji na viti vilivyovunjwa na mashabiki hao.
Kutokana na hali hiyo, askari wa Jeshi la Polisi waliokuwepo uwanjani hapo walilazimika kulipua mabomu matatu ya machozi ili kutawanya mashabiki hao, hali iliyozua hali ya taharuki uwanjani hapo.
Matokeo haya yanaifanya Simba kufikisha pointi 21 na kubaki katika nafasi ya nne baada ya kucheza mechi 12.Nayo Kagera imepanda hadi nafasi ya tano ikiwa na pointi 17.

No comments:

Post a Comment