Search This Blog

Friday, October 4, 2013

Mbeya City ikikubali kuwa tawi la Simba au Yanga, imekwisha



KATI ya timu tatu mpya katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu wa 2013/ 14, Mbeya City ndiyo imeanza kwa moto mkali kuliko Rhino Rangers ya Tabora na Ashanti United ya Dar es Salaam.
City imekuwa gumzo nchi nzima na sababu yake ni moja tu, ilizitoa jasho Yanga katika mechi yake mjini Mbeya na Simba katika mchezo wao Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kocha Ernie Brandts wa Yanga hana hamu na Abdallah Kibaden ameivulia kofia timu hiyo.

Katika kipindi hiki ambapo Tukuyu Stars ‘imepotea’, Mecco imekufa na Prisons ikichechemea, City ndiyo imewaunganisha wapenzi wa soka katika mkoa wa Mbeya. City ikicheza katika dimba la Sokoine huunganisha hata pande hasimu za kisiasa na kuishangilia timu hiyo ambayo ilinunuliwa na jiji la Mbeya kutoka kwa Rhino ya Arusha.

Kimsimamo, City iko nafasi ya nane ikiwa na pointi nane kutokana na mechi sita ilizocheza, pointi moja nyuma ya Yanga iliyoko nafasi ya tano. Mbeya City imeshinda mechi moja na imetoka sare tano, haijafungwa hata mechi moja.
City ikishinda mechi ya keshokutwa dhidi ya Oljoro JKT na Yanga ikafanya vibaya dhidi ya Mtibwa Sugar, inaweza hata kuchupa nafasi ya pili. Hata hivyo itategemea matokeo ya mechi nyingine kati ya Kagera Sugar na JKT Ruvu.

City iliifunga Ruvu Shooting mabao 2-1 na kutoka sare na Yanga (1-1), Simba (2-2), Azam (1-1), Coastal (1-1) na Kagera (0-0). Kiuchezaji Mbeya City huonekana wakipambana kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
City namilikiwa na kusimamiwa vizuri na Halmashauri ya Jiji la Mbeya. Mashabiki wa Simba na Yanga sasa ‘wamepungua’ jijini Mbeya na wote huishabikia na kuiunga mkono City kutegemea inacheza na timu ipi. Iko huru haijajipambanua kuwa tawi la Yanga au Simba, jambo linalosababisha klabu nyingi za mikoani kusambaratika.

Mmoja wa wachezaji wa City, kiungo mshambuliaji Richard Peter anathibitisha kwa kusema hawana ushabiki wala uhusiano na timu yoyote ya ligi kuu ndiyo maana wameweza ‘kuzibania’ timu zote walizokutana nazo.
“Hatuna urafiki wala undugu na timu yoyote hata hizo Simba na Yanga hatuna urafiki nazo, ndiyo maana tumeweza kuzibana na kutoka nazo sare. Hatuwezi kuwa tawi la Simba au Yanga, sisi tunatazama zaidi katika ushindi na kufanya vizuri katika ligi na si vinginevyo,” anasema Richard.

Jijini Mbeya, kila unapokaribia mchezo wowote wa  City, jiji la Mbeya hupambwa kwa rangi ya zambarau ambazo ndizo zinazotumiwa na timu hiyo na hata unapoingia uwanjani, mashabiki wa timu ni wengi na wakati mwingine hufikia hatua ya kukaa sehemu zilizozoeleka kukaliwa na mashabiki wa Simba au Yanga.

Idadi ya mashabiki wanaojitokeza uwanjani kutazama mechi za City na ushahidi ni mapato ya mlangoni. Mechi ya City na Yanga hivi karibuni iliingiza zaidi ya Sh. 93 milioni wakati Yanga na Prisons kilipatikana kiasi chini ya hicho. Hii ina maana mvuto wa City ni mkubwa kuliko Prisons.
Nje ya uwanja, Mbeya City ni timu yenye mashabiki wenye hamasa kubwa ya kuishangilia na hata matajiri hujisikia raha kuichangia na kusafiri nayo kutoka Mbeya hadi Dar es Salaam kuipa nguvu.

Ndani ya uwanja, Mbeya City ni timu yenye nidhamu kubwa ya mchezo na hata kocha wake, Juma Mwambusi anakiri kuwa wachezaji wake ni wasikivu na wenye hamasa ya hali ya juu kutaka kuona timu yao inafanya vizuri.
“Tupo kama kitu kimoja na tunasikilizana wakati wote, tumekaa pamoja kwa muda mrefu na ndiyo maana leo hii tunafanya vizuri katika ligi. Hakuna kitu kingine cha ziada ukiacha hilo na wananchi kuiona ni timu yao hivyo wanapaswa kuiunga mkono wakati wote,” anasema Mwambusi aliyewahi kuinoa Prisons.

Wachezaji wanaonekana wenye pumzi na wanaocheza kwa malengo kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo jambo ambalo Mwambusi anasema ni matokeo mazuri ya mazoezi ya kujiandaa kwa msimu huu wa ligi.
City inaonekana imejipanga zaidi ndani na nje ya uwanja, lakini inaweza kuingia katika matatizo na kupoteza mwelekeo wake endapo itaingia katika mkumbo wa kukubali kutumiwa na moja ya klabu za Simba na Yanga.


2 comments:

  1. Hii timu haitachukua muda kabla haijaelekea zilipoelekea timu nyingine. Subiri usajili utaona

    ReplyDelete
  2. Ligi inatimu 13 pinzani na mbeya city kwa nini uiombee au uilinganishe na yanga kama ikifungwa.

    ReplyDelete