Search This Blog

Tuesday, October 22, 2013

MAKALA: YANGA WALIVYOUKATAA USHINDI DHIDI YA SIMBA


MUDA mfupi tu baada ya mechi ya Simba na Yanga kumalizika, si wachezaji, viongozi, wanachama na hata mashabiki wa Yanga, wote walielekeza lawama zao kwa safu ya ulinzi ya timu hiyo kwamba ilicheza chini ya kiwango.

Lakini wakati haya yanatokea, hakuna aliyefikiri mbwembwe za baadhi ya wachezaji wa timu hiyo walizofanya wakati wakiongoza mabao 2-0.

Mbwembwe za Yanga zilijaa vichwani mwa wachezaji na hata mashabiki ambao kwa hakika waliamini kwamba, tayari timu yao imeshaikamata Simba na wangeweza kufanya lolote ndani ya uwanja hata kipindi cha pili.

Simba wakati inaifunga Yanga mabao 5-0, haikuridhika na idadi ya mabao iliyokuwa ikiyapata na ndiyo maana hadi mwisho wa mchezo huo ilikuwa ikishambulia kama nyuki.

Katika michezo mingi ambayo Yanga imeshinda, inaonekana wazi ilikuwa na uwezo wa kushinda hata idadi kubwa ya mabao lakini ‘ubishoo’ na mbwembwe kwa mashabiki ndizo zinazoigharimu timu hiyo.  

Yanga ilikuwa na uwezo mkubwa wa kuibuka na ushindi wa idadi kubwa ya mabao hasa katika kipindi cha kwanza, lakini kitendo cha wachezaji wake kuridhika na utangulizi wa mabao 2-0, uliiponza timu hiyo na hasa wachezaji wake walipoanza kucheza kwa mbwembwe.

Mrisho Ngassa na Haruna Niyonzima ndiyo walioongoza kwa kucheza kwa mbwembwe walipopata mipira na kushangiliwa na mashabiki wengi wa timu hiyo ambao nao walidhani tayari Yanga ina mkataba wa ushindi wa mechi hiyo isiyotabirika.

Unafiki wa mashabiki, ufalme wa Ngassa na Niyonzima;
Ngassa na Niyonzima wakifanya mbwembwe zao hasa za kutuliza mpira hata kukanyanga na kupanda juu ya mpira, mashabiki walishangilia, lakini tazama beki David Luhende akichelewa kupandisha mashambulizi utaona mashabiki wale wale wanamzomea na kumlazimisha kupiga mpira mbele.
Kiungo Frank Domayo anaweza kupoteza mpira kwa bahati mbaya, lakini mashabiki watamzomea kupita kiasi lakini kosa hilo likifanywa na Niyonzima wakati akitaka kupiga pasi kwa mbwembwe, huyo atapigiwa makofi na mashabiki wakihidhinisha kwamba amefanya kwa bahati mbaya.

Yanga iliposhika kiungo iliridhika,   
Dakika 45 za kipindi cha kwanza Yanga ilishika kiungo hasa wachezaji wake Athuman Idd ‘Chuji’, Frank Domayo na Haruna Niyonzima lakini baada ya kupata bao la pili, kasi yao ya kupeleka mipira mbele ilipungua.
Viungo hawa waliweza kuwatawala Jonas Mkude na Abdulhalim Humud na kufanya watakavyo na kila mara walifanikiwa kufikisha mipira yao kwa washambuliaji.
Kibaya zaidi wachezaji walioonekana na kiu ya kupata mabao zaidi ni Kiiza na Didier Kavumbagu pekee, Domayo alionekana kutii maelezo ya kaka zake ndani ya uwanja, hakuweza kulazimisha ushindi zaidi.

Ndemla, Gallas walivyobadili mchezo,
Simba waligundua mapema kwamba Humud na Haruna Chanongo hawakuweza kuhimili kasi na uwezo wa viungo wa Yanga, moja kwa moja waliwatoa viungo hao na nafasi zao kuchukulwa na Said Ndemla na William Lucian maarufu kama Gallas.
Ndemla na Gallas walimudu kukaba na kupandisha timu haraka haraka na wakati Yanga wakiendelea na mbwembwe zao, wao wakawa wanafanya kazi ya kutibua mipango ya Chuji na Niyonzima huku wakihakikisha mipira inafika kwa Betram Mombeki na Amisi Tambwe.

Yanga yakumbuka shuka asubuhi,
Baada ya kuona maji yanafika shingoni, Yanga ikazinduka na kutaka kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwa Simba lakini ukuta wa Simba ukajiamini na kutoruhusu shambulizi lolote la maana kutoka kwa Yanga.
Lawama zikaanza miongoni mwa wachezaji wa Yanga na hata walipofungwa bao la pili, Cannavaro alikuwa akimlaumu ‘live’ Yondani kwa kutokuwa makini wakati wote walipaswa kuwasiliana namna ya kucheza mpira wa kona.

Sub Yanga haikuwa sahihi,
Kama kuna mtu alikuwa makini na uchu wa kufunga mabao ni Kiiza, huyu alikuwa akiitafuta hat trick muda wote, lakini jitihada zake ziliishia kwenda benchi na nafasi yake kupewa Simon Msuva.
Msuva ni mchezaji mzuri awapo na mpira lakini baada ya hapo si mzuri, huyu si mkabaji kama alivyo Kiiza. Beki ya Simba hailewani na inapoteza mipira kirahisi kama ikikabwa kwa presha, Kavumbagu na Kiiza kazi hiyo wanaiweza.
Matokeo yake mipira mingi iliyokuwa ikienda kwa Msuva pindi inapopotea ilikuwa haipatikani kirahisi. Msuva pia si mtu wa kupambana mwanzo mwisho na ni mwoga kwani kuna wakati alikuwa akishindwa kuwahi mipira na kumpa kazi rahisi Haruna Shamte.

2 comments:

  1. Ni kweli yanga walifanya kosa kubwa sana kujiamini kwa ushindi wa first half,hata hvyo kocha ilibidi awape tahadhari wachezaji wake kwamba simba second half wataingia kwa shauku ya kurudisha magoli na pengine kutafuta ushindi hvyo kuanzia viungo na mabeki wangekuwa makini,ajabu sijui walikuwa wanacheza fomesheni,baada ya kumtoa KIIZA nilitegemea angeingia beki au kiungo,mfano angeingia Juma Abdul ili acheze pembeni na TWITE asaidie ktkt

    ReplyDelete
  2. Tumejimaliza wenyewe yanga, tusimtafute mchawi...tukae chini turekebishe mapungufu yaliyo jitokeza tuendelee na michezo iliyobaki

    ReplyDelete