Search This Blog

Friday, October 18, 2013

COUNTDOWN TO DAR DERBY: MAGARI MAALUMU TU MECHI YA SIMBA, YANGAMagari yenye shughuli maalumu tu ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia uwanja wakati wa mechi ya Simba na Yanga itakayochezwa keshokutwa (Jumapili) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi itaanza saa 10 kamili jioni, na kila timu inaruhusiwa kuingia na magari matatu tu; gari la timu na mengine mawili ya viongozi. Ukaguzi wa kuingia uwanjani ni kwa watu wote, kwani utaratibu huo si wa kumdhalilisha mtu bali lengo lake ni kuhakikisha usalama.

Vilevile watu hawataruhusiwa kuingia uwanjani na mifuko ya aina yoyote ikiwemo mabegi, isipokuwa kwa waandishi wa habari wanaotumia mabegi hayo kwa ajili ya kubebea kamera zao. Pia hakuna wafanyabishara watakaoruhusiwa kufanya biashara katika maeneo yanayozunguka uwanja.

Kwa washabiki watakaokuwa katika mazingira ya kuwa kero kwa wenzao wakiwemo walevi hawataruhusiwa kuingia uwanjani, pamoja na wale wenye silaha kama bastola ambapo wakikamatwa wafikishwa polisi na baadaye kufunguliwa mashtaka kortini.

Barabara ya Uwanja wa Taifa itafungwa kuanzia saa 2 asubuhi upande wa Chang’ombe, hivyo washabiki wanatakiwa kununua tiketi zao mapema kesho (Jumamosi) ambapo zitaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali kuanzia saa 4 asubuhi.

Vituo hivyo ni mgahawa wa City Sports Lounge, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru, mgahawa wa Brake Point uliopo Kijitonyama na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.

1 comment:

 1. SIMBA NA YANGA BADO ZIKO GIZANI.

  Wiki hii imetawaliwa na mbwembwe na mijadala ya pambano la soka kati ya Simba na Yanga,ambalo litafanyika kesho katika uwanja wa Taifa.Sasa tunahesabu masaa tu.Pamoja na msisimko wa mechi kama hii,hasa upande wa mashabiki,timu hizi za Kariakoo bado ziko gizani,pamoja na kuongozwa na watu ambao angalau wanaonekana wanajua kinachotakiwa kufanyika ili timu hizi ziwe na maendeleo ya kisoka ndani na nje ya mipaka yetu.

  Pamoja na kujua wanachotakiwa kufanyika,wao wameamua kufanya kile ambacho hakitakiwi.Ni jambo la kusikitisha na pengine kurudishana nyuma,pale ambapo timu hizi zinaendesha kimiujiza na kishirikina.Mapambano ya Simba na Yanga yanaambatana na mambo ya ajabu ambayo dunia iliyostaarabika imekwenda mbali zaidi.

  Leo tunaambiwa,Yanga wamejichimbia Pemba na Simba sijui wapi eti kujiandaa na mechi hiyo moja.Pambano la Simba na Yanga lina maandalizi speshali.Eti wachezaji wananyang'anywa simu,wekwa chini ya ulinzi mkali,kisa kuogopa hujuma kutoka upande wa pili.Haya yanafanywa na viongozi wetu wa kisasa ambao kila mwisho wa wiki wanaangalia mechi za Ulaya.Uliona wapi,Arsenal inapojiandaa kucheza na Spurs,wanahama London na kuweka kambi maalum,au hata Man United inapocheza na Man City?

  Matokeo yake wachezaji wanatwishwa mzigo mzito na kushindwa kufanya vizuri kwa sababu ya pressure za nje ya uwanja.Kocha naye anakuwa mwoga wa kufanya maamuzi kwa sababu anajua,asipoifunga Yanga/Simba atatimuliwa.Mwisho wa siku tunashuhudia mchezo mbovu ambao hauendani na hadhi ya timu hizi.Kiongozi anahofu ya kuondolewa na wanachama ambao hata hawalipi ada.Kocha anahofu ya kutimuliwa.Mchezaji anahofu ya kusimamishwa kwa madai ya kuhujumu timu.Tumesikia upande wa Simba baadhi ya wachezaji wao kusimamishwa.Inamaana hata wachezaji hawajui wanachotakiwa kufanya,hadi wahujumu timu zao?

  Kesho tutegemee yaleyale ya kurusha njiwa,kuvunja nazi,na baadhi ya wachezaji kivaa hirizi wanazopewa na viongozi wao.Lakini hakuna jipya litakaloonekana uwanjani,kwa sababu timu hizi za Kariakoo zinaendeshwa ki-uswazi zaidi.Na baada ya mchezo,timu itakayofungwa,kesho yake utasikia wanajiita wanachama hawamtaki Mwenyekiti.Tuko kwenye mduara wa ujinga.Tunazunguka mlemle.Sisi ni wa hapahapa.Hata tukioga hatuendi mjini,hadi hapo tutakapobadilisha fikra zetu.

  ReplyDelete