Search This Blog

Monday, October 21, 2013

KIBADENI, BRANDTS WOTE WALIA NA HUJUMA SIMBA NA YANGA


UNAWEZA usiamini lakini ndiyo ukweli ilivyo, makocha Abdallah Kibadeni wa Simba na Ernie Brandts wa Yanga kwa pamoja wamesema vikosi vyao vimehujumiwa hadi kutoka sare ya mabao 3-3.

Timu hizo zilipambana jana Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara na hadi mapumziko Yanga ilikuwa ikiongoza kwa mabao 3-0, lakini Simba iliweza kusawazisha mabao hayo katika kipindi cha pili.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza aliyefunga mawili wakati mabao ya Simba yalifungwa na Betram Mombeki, Joseph Owino na Gilbert Kaze.

Muda mfupi baada ya mchezo huo, Kibadeni aliuambia mtandao huu kwamba, kikosi chake hakikucheza kwa maelekezo katika kipindi cha kwanza na wapo wachezaji waliocheza chini ya kiwango kwa makusudi ili wasipate matokeo mazuri.

Kibadeni alienda mbali kwa kusema kuwa, tangu awali alifahamu kuwa kuna wachezaji waliopangwa kuvuruga mechi hiyo kwa makusudi ili Simba ifungwe na ndiyo maana kipindi cha pili aliwatoa na mambo yakawa mazuri.

“Naomba andikeni vizuri kwa manufaa ya soka la Tanzania, hawa watoto wadogo sana wanaanza kurubuniwa hivi wanataka soka la Tanzania liende wapi? Sisi tupo kambini watu wanapita pita ili kuhonga wachezaji.

“Mpaka mapumziko kweli tulikuwa tumeshafungwa mabao 3-0, nilipoenda katika vyumba vya kubadilishia nguo nikawaambia mabao mliyowapa matatu yanatosha sasa rudini mkacheze mpira, na kweli waliporudi walicheza mpira na kupata mabao matatu na kama muda ungeongezeka kidogo tu tungeweza kupata ushindi,” anasema Kibadeni.

Pengine Kibadeni alikuwa akiwazungumzia wachezaji Harun Chanongo na Abdulhalim Humud ambao aliwatoa muda mfupi baada ya kuanza kwa kipindi cha pili na nafasi zao kuchukuliwa na Said Ndemla na William Lucian ‘Gallas’ ambao waliweza kubadili mchezo na kuifanya Simba itawale kiungo.

Muda mfupi baada ya Kibadeni, Kocha wa Yanga, Brandts naye alisema alishangazwa na hali aliyoikuta katika chumba cha kubadilishia nguo ilimshangaza kwani wachezaji walikuwa wakishangilia kama mpira umeisha huku wakishindwa hata kumsikiliza wakati mwingine.

“Haikuwa hali nzuri, nilipofika katika chumba cha kubadilishia nguo niliwakuta wachezaji wanashangilia nikastaajabu hali ile na niliwaonya kutojiamini sana na kitendo kilichotokea kipindi cha pili hakikuwa cha kiungwana, hawakucheza kama wachezaji wa kulipwa na walicheza kiwango cha chini hadi tukafungwa mabao matatu, huwezi kuzungumza lolote kwa timu kama hii,” anasema Brandts raia wa Uholanzi.

Brandts anasema hakukuwa na sababu ya wachezaji wake kucheza soka la madoido walipokuwa mbele kwa mabao 2-0 kipindi cha kwanza kwani Simba walionekana kuzidiwa na walikuwa na uwezo wa kufunga mabao mengi zaidi lakini wakaona mechi imeisha.

Matokeo ya mchezo huo yameifanya Simba kushika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 19 baada ya mechi tisa wakati Yanga ina pointi 16 kwa idadi kama hiyo ya mechi. Azam FC ndiyo inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 20 sawa na Mbeya City inayoshika nafasi ya pili. Azam na Mbeya hata hivyo zimecheza mechi 10.

No comments:

Post a Comment